Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Chadema wazungumzia tuhuma za CAG kuhusu ununuzi wa gari

Mon, 15 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania, Chadema, kimetoa ufafanuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad kwa mwaka wa fedha 2017/18 kuhusu eneo la ununuzi wa gari.

Ripoti hiyo imebaini Machi 30, 2017, Bodi ya Wadhamini ya Chadema iliingia mkataba na kampuni ya AMC Tanzania Limited kwa ajili ya ununuzi wa gari jipya aina ya Nissan Patrol Y61 Series yenye moduli ya GRX kwa Sh.147.7 milioni kwa usajili wa jina la bodi badala yake ikasajiliwa kwa jina la mbunge.

Mkurugenzi wa Oganaizesheni na mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Aprili 13,2019 amesema: “Kilichotokea ni kwamba, mwanachama aliomba kukopa gari, chama kikakubali, kikaamua kulinunua gari hilo kwa usajili wa jina lake.”

“Akiwa ameingia makubaliano ya kurejesha mkopo huo ndani ya miaka mitatu wakati huo gari lilikuwa chini ya chama, baada ya miaka miwili mwanachama huyo alikiri kwamba hawezi kulipa deni, kwa hiyo chama kikaamua kuchukua gari hilo.” amesema Kigaila bila kumtaja kwa jina mwanachama huyo.

Kigaila amesema, “CAG anasema gari lilisajiliwa kwa jina la mbunge, kwani aliyekuwa ananua gari ni nani? Chama hakikuwa na shida ya gari na alipokuja (CAG) alikuta gari lipo likiwa limesajiliwa kwa jina la mwanachama kwa sababu akilipa huo mkopo linakuwa gari lake (mbunge), aliposhindwa gari limerudishwa.”

Kigaila aliyekuwa ameongozana na baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwamo Waziri Kivuli wa Fedha, Halima Mdee amesema kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni kubadili umiliki kutoka jina la mwanachama huyo kwenda Bodi ya Wadhamini, kama ilivyopendekezwa na CAG.

Katika tathmini hiyo ya vitabu vinne kati ya vitano vya CAG, Chadema imehoji eneo la ubadhirifu wa fedha katika kitabu cha mashirika ya umma, Serikali Kuu, miradi ya Maendeleo na Serikali za Mitaa, huku kikiomba Kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC) kuitisha vyama vyote vya siasa ili kujieleza.

Amesema jambo hilo ni kawaida katika taasisi yoyote, akipongeza umakini wa chama hicho katika usimamizi wa malipo ya deni hadi mbunge alipokwama na kubakia mikononi mwa chama.

“Wabunge wanakopeshwa magari kwa kutumia majina yao, si ya Serikali ili wakimaliza mikopo yabakie kuwa mali yao, kwa mfano wewe unaweza kuomba mkopo lakini kampuni lazima iweke utaratibu wa namna ya kurejesha fedha hizo za umma. Chama hakikuwa na shida ya gari,” amesema.

Katika ufafanuzi wake, Kigaila amesema taarifa hizo alielezwa CAG na alionyesha hata makubaliano hayo isipokuwa mkataba kati ya bodi na mwanachama aliyekopa.



Chanzo: mwananchi.co.tz