Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: CCM wakana kufanya mikutano ya hadhara, wadau wataka katazo liondolewe

Thu, 14 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati wadau wa demokrasia nchini wakitaka zuio la mikutano na maandamano ya vyama vya siasa kuondolewa, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekana kukiuka agizo hilo na kudai kinafanya mikutano ya ndani na kukagua utekelezaji wa ilani yake.

Agizo la kutofanyika kwa mikutano ya hadhara na maandamano limekuwa likirudiwa na Rais John Magufuli mara kadhaa, huku akitaka wabunge waliochaguliwa kufanya mikutano kwenye majimbo yao husika.

Agizo hilo pia limeshatolewa na Jeshi la Polisi ambalo pia limechukua hatua ya kuzuia mikutano kadhaa hasa ya vyama vya upinzani.

Hivi karibuni baadhi ya viongozi wa CCM wakiwamo katibu mkuu wake, Dk Bashiru Ally na Humphrey Polepole (Itikadi na Uenezi) wameonekana wakifanya mikutano ya hadhara katika mikoa ya Morogoro na Arusha.

Alipoulizwa kwa simu jana, katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga alisema chama hicho hakifanyi mikutano ya hadhara.Lubinga aliyekuwa safarini kutoka mkoani Njombe kwenda Dodoma, alisema mikutano wanayofanya CCM ni ya ndani kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

“Hakuna anayefanya mikutano, CCM haifanyi mikutano ya hadhara,” alisema Kanali Lubinga. “Siyo mimi, Serikali imesema hivi, wabunge na madiwani wanaweza kuitisha mikutano lakini ile ‘public rallies’ (mikutano ya hadhara) ya kubeba watu kwenye malori ndiyo imekatazwa,” alisema Lubinga.

Alipoulizwa kuhusu mikutano ya hadhara iliyofanywa na Dk Bashiru na Polepole, Lubinga alisema: “Polepole yeye anakwenda kukagua ilani, sasa muulize huyohuyo Polepole, mimi sijamwona. Sisi tunafanya mikutano ya ndani na siyo public rallies, sasa kwa sababu niko Njombe muulize mwenyewe.

“Labda kuna mkutano amefanya mimi sina uhakika, lakini yeye haruhusiwi. Hairuhusiwi kufanya mikutano ya hadhara, ni mikutano ya ndani kwa ajili ya kukagua miradi, tunapokagua miradi ndiyo tunazungumza na watu lakini mikutano ya hadhara hairuhusiwi,” alisema. Polepole alipotafutwa kwa simu hakupokea.

Wadau wataka katazo liondolewe

Baadhi ya wadau wa siasa waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti walisema licha ya CCM kuonekana kukiuka agizo hilo, liko kinyume na Katiba ya nchi.

Mchambuzi wa siasa na maendeleo, Dk Marcosy Albanie alisema CCM imejipambanua kama kundi lenye hadhi kubwa kuliko vyama vingine kiasi cha kutofuata maagizo.

“Inaonekana CCM siyo chama cha siasa ndiyo maana agizo la Rais John Magufuli ni kama haliwahusu. Lakini pamoja na hivyo, katazo lake haliko Kikatiba linaonekana kuvionea vyama vya upinzani vilivyotaka kufanya mikutano na maandamano,” alisema.

Maoni hayo yaliungwa mkono na mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba, Hebron Mwakagenda aliyesema katazo hilo lilitolewa kinyume cha sheria.

“Hilo katazo liko kinyume na Katiba, sasa kama Katiba imeruhusu kwanini izuiwe? Ilikuwa ni kwa ubabe tu. lakini sasa inaonekana mikutano na maandamano yameanza kufanywa kinyemela,” alisema Mwakagenda.

Alisema jukwaa hilo lilizuiwa kufanya maandamano yao mwaka jana na kwa sasa wanajipanga kuifikisha Serikali mahakamani.

Maoni kama hayo pia yametolewa na Mkurugenzi wa uhusiano wa umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya akisema katazo hilo siyo halali.

“Nchi yetu inapitia kipindi kigumu kidemokrasia, kwa sababu amri yenyewe siyo halali kisheria, lakini kwa kuwa ilitolewa na mkubwa tunaheshimu. Sasa tunashangaa kuona Polepole na Dk Bashiru wakifanya mikutano na Polisi wanaangalia nani wa kumkamata,” alisema Kambaya.

Aliongeza, “Aliyetoa amri hiyo aangalie, kwa nini azuie mikutano ya hadhara na maandamano? Rais Mkapa (Benjamin ) alijaribu mwaka 2000 watu wengi wakafa, sivemma yatokee tena katika awamu hii ya tano.”

Soma zaidi: VIDEO: Mikutano ya hadhara na maandamano, Vigogo CCM wamtega Magufuli



Chanzo: mwananchi.co.tz