Dar es Salaam. Wakati uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ukiwasimamisha masomo wanafunzi sita wa chuo hicho, mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), John Pambalu amesema wapo tayari kwenda mahakamani kuwatetea.
Wanafunzi hao sita ni viongozi wa Serikali ya wanafunzi ya chuo hicho (Daruso).
Pambalu ametoa kauli hiyo leo Jumatano Desemba 18, 2019 wakati akitoa salamu za Bavicha kwenye mkutano mkuu wa chama hicho unaofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Amelaani uongozi wa chuo hicho kuwasimamisha wanafunzi hao kwa maelezo kuwa wametolewa kafara kwa sababu walikuwa wakiwatetea wenzao.
"Tumeshazungumza na wanasheria wa Chadema na tupo tayari kwenda mahakamani kuwatetea," amesema Pambalu.
Awali wenyeviti wa kanda za Serengeti na Nyasa, Ester Matiko na Mchungaji Peter Msigwa waliungana mkono uamuzi wa Bawacha kuwatetea wanafunzi hao.
Leo uongozi wa UDSM umewasimamisha masomo wanafunzi hao katika kipindi kisichojulikana, kuwataka kusubiri hatima yao watakapoitwa katika kikao cha nidhamu.
Wamesimamishwa ikiwa imepita siku moja tangu Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kuagiza uongozi wa chuo hicho kuwachukulia hatua baada ya kuipa saa 72 Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kushughulikia madai ya mikopo ya wanafunzi.
Profesa Ndalichako alitoa kauli hiyo mkoani Kigoma na kuwashangaa UDSM kukaa kimya dhidi ya walioandika tamko hilo, “nawaagiza uongozi wa chuo kikuu kuhakikishe kinachukua hatua kwa wanafunzi walitoa tamko hilo ndani ya saa 24 kinieleze kimechukua hatua gani.”