Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Utekelezaji Ilani waongeza pato la Mtanzania,

65ae390c256465392211bcc95a8b2f32 Utekelezaji Ilani waongeza pato la Mtanzania,

Mon, 31 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ILANI ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025, imeakisi mambo makubwa yaliyotekelezwa kutokana na Ilani ya mwaka 2015-2020.

Mambo hayo ni pamoja na kuongezeka kwa pato la mwananchi kutoka Sh milioni 1.96 mwaka 2015 hadi Sh milioni 2.45 mwaka 2018, huku Pato la Taifa likiongezeka kwa wastani wa asilimia 6.7.

Hatua hiyo ni moja ya sababu zilizochangia Benki ya Dunia, Julai Mosi mwaka huu kuitangaza Tanzania kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa kipato cha kati.

Aidha, utekelezaji huo wa Ilani ya 2015-2020 kulikochangia upatikanaji wa Ilani mpya ya 2020-2025, kumewezesha wastani wa umri wa kuishi kuongezeka kutoka miaka 61 mwaka 2015 hadi miaka 65 mwaka huu (2020). Hayo ni kwa upande wa Tanzania Bara.

Kwa upande wa Zanzibar, wastani wa pato la mwananchi limekua kutoka Sh milioni Sh 1.66 mwaka 2015 hadi Sh milioni 2.54 mwaka 2019 na Pato la Taifa limeongezeka kwa wastani wa asilimia 6.8 kwa mwaka huku wastani wa umri wa kuishi ukiwa ni miaka 68.4 mwaka huu kutoka miaka 66.6 mwaka 2015.

Katika hatua nyingine, Ilani mpya ya 2020-2025 katika kipengele cha utafiti, teknolojia na ubunifu, imesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM itahakikisha kila shule ya sekondari nchini inakuwa na kompyuta na huduma za intaneti.

Ilani hiyo ya mwaka 2020-2025 iliyozinduliwa juzi kwenye mkutano wa uzinduzi kampeni za chama hicho katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, imeeleza hayo.

Katika kipengele cha matokeo ya mafanikio yatokanayo na Ilani ya 2015-2020 kwa maendeleo na ustawi wa wananchi, pato la mwananchi limekua kutoka Sh 1,968,965 mwaka 2015 hadi Sh 2,458,496 mwaka 2018 kwa Tanzania Bara.

Kwa upande wa Pato la Taifa kwa Tanzania Bara, limeongezeka kwa wastani wa asilimia 6.7 kwa mwaka huku wastani wa umri wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 61 mwaka 2015 hadi miaka 65 mwaka 2020.

"Wastani wa pato la mwananchi limekua kutoka shilingi 1,666,000 mwaka 2015 hadi shilingi 2,549,000 mwaka 2019 na Pato la Taifa limeongezeka kwa wastani wa asilimia 6.8 kwa mwaka. Wastani wa umri wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 66.6 mwaka 2015 hadi miaka 68.4 mwaka 2020," ilieleza Ilani hiyo.

Katika eneo la vipaumbele na kipengele cha utafiti, teknolojia na ubunifu, Ilani mpya ya 2020-2025 imeanisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano ikiwa CCM itapewa tena ridhaa ya kuongoza nchi, itahakikisha shule zote za sekondari nchini zinakuwa na kompyuta na huduma za intaneti.

Katika eneo hilo la utafiri, teknolojia na ubunifu, serikali itaongeza kuwasomesha Watanzania nje ya nchi katika vyuo bora na maalum duniani kwenye masuala ya sayansi, tiba, tekonolojia na maeneo mengine yenye umuhimu.

Hatua hiyo ni kuwezesha kupata maarifa bora na ya kisasa na ujuzi ili kuchochea maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.

Matokeo hayo machache ni sehemu ya mambo mengi makubwa, ambayo Ilani ya zamani imetekeleza, huku Ilani mpya ikikazia utekelezaji wake maradufu ikiwa itapata ridhaa ya kuongoza nchi kwa miaka mingine mitano.

Utekelezaji wa Ilani hiyo mpya ya 2020-2025 utaongozwa na kauli mbiu isemayo: "Tumetekeleza kwa Kishindo, Tunasonga Mbele Pamoja".

Chanzo: habarileo.co.tz