Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ushirikiano Chadema, ACT wanukia

48009 ACT+PIC Ushirikiano Chadema, ACT wanukia

Mon, 8 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

CHAMA cha ACT-Wazalendo na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vimeonyesha nia ya kushirikiana katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Tayari ACT-Wazalendo imeitikia wito uliotolewa na Chadema wa kushirikiana katika uchaguzi huo kwa kukiandikia barua ya kuanza rasmi mazungumzo ya ushirikiano huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, alisema siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema kutoa wito huo, alimwandikia barua ya kukubali kuingia katika mazungumzo.

“Tumemsikia Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akisema milango iko wazi kwa chama chochote kushirikiana nao katika uchaguzi mkuu, siku moja tu baada ya kutoa kauli hiyo, mimi kama Katibu Mkuu wa chama changu, nilimwandikia barua kumweleza jinsi ambavyo tumepokea wito huo kwa mikono miwili na kumwonyesha utayari wa kwenda katika ushirikiano ikiwamo kuanza mchakato wa mazungumzo,” alisema Shaibu.

“ACT-Wazalendo tunaamini katika ushirikiano kwa sababu ndiyo silaha pekee ya kuhakikisha kwamba CCM itaondoka madarakani mwaka 2020, tukishikamana kwa pamoja na tukaweka tofauti za kiitikadi pembeni tuna fursa kubwa sana ya kuiondoa madarakani.”

Shaibu alisema wanaamini kwamba mazungumzo hayo yatafikia katika hatua nzuri.

“Na jambo kubwa katika mambo ya ushirikiano ni utayari, na kama Chadema wameonyesha hilo na wametangaza kwamba mchakato unaweza kuanza na sisi ACT-Wazalendo… tumeonyesha utayari na tumewajibu kwa barua, hiyo inakupa picha kwamba tunakoenda ni kuzuri,” alisema Shaibu.

Alisema chama hicho kina matumaini kwamba katika muda uliopo wa kujiandaa na uchaguzi mkuu, watafanikiwa kutengeneza vuguvugu kubwa.

“ACT-Wazalendo bado tuna matumaini makubwa katika muda uliopo, kutengeneza vuguvugu kubwa (movement) litakalohakikisha tunakwenda kwenye uchaguzi katika mshikamano,” alisema Shaibu.

Pia alisema kwamba wanahitaji mshikamano huo kwa sasa ili kuwa na nguvu zaidi ya kuwaletea Watanzania maendeleo.

Akizungumzia ratiba ya chama hicho katika kuelekea uchaguzi huo mkuu, Shaibu alisema katikati ya mwezi huu wanatarajia kuzindua rasmi uchukuaji na urudishaji wa fomu za wagombea katika nafasi mbalimbali.

Alisema tayari zaidi ya wanachama 200 wametangaza nia ya kugombea nafasi ya ubunge kupitia chama hicho.

Wiki iliyopita Chadema kilitoa wito kwa vyama vya siasa vyenye nia ya kushirikiana nacho, kupeleka maombi ya kuingia katika mazungumzo rasmi ya ushirikiano huo, kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao.

Chama hicho kilitoa wito wa ushirikiano huo katika ngazi zote kuanzia nafasi ya udiwani, ubunge na urais.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live