Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Usaliti bado mwiba CCM

44052 Pic+usaliti Usaliti bado mwiba CCM

Wed, 27 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kilimanjaro ni moja ya mikoa ambayo tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, umekuwa ukitajwa kama mkoa ambao upinzani umesimika mizizi yake.

Uchaguzi Mkuu 2015, majimbo saba kati ya tisa mkoani humo yalikwenda upinzani, likiwamo la Moshi Mjini ambalo limekuwa ngome ya upinzani kwa zaidi ya miaka 20. CCM iliambulia majimbo mawili – Mwanga kwa Profesa Jumanne Maghembe na Same Magharibi kwa David Mathayo.

Hata hivyo, si kwamba wapinzani wamekuwa yanapata majimbo hayo kwa urahisi, bali ni kupitia mapambano na kuizidi mbinu CCM, ikiwamo kuwashawishi baadhi ya makada wa chama tawala kuwaunga mkono.

Wakati tunakaribia uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani, CCM imeanza harakati za kuyanyatia majimbo hayo.

Wiki iliyopita, Gaudensia Kabaka, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) alifanya ziara ya siku mbili mkoani Kilimanjaro, agenda kuu ikiwa ni kuangalia uhai na kuimarisha chama.

Katika ziara hiyo, Kabaka ambaye pia ni mlezi wa chama mkoani humo, alitembelea majimbo ya Same Mashariki na Moshi Mjini, ambapo pamoja na mambo mengine, alikutana na viongozi kuanzia ngazi za mashina, kata, wilaya na mkoa na kujadili sababu za kufanya vibaya mkoani humo.

Moja ya sababu zilizoibuka katika vikao hivyo, ni usaliti wa baadhi ya wanachama na viongozi wa chama kuwa ndicho chanzo cha chama hicho kufanya vibaya katika chaguzi zilizopita.

Usaliti bado upo

Wakati ikitarajiwa kwamba ‘wasaliti’ wa chama hicho kabla na baada ya mwaka 2015 wameisha baada ya kuchujwa na kuadhibiwa na hata kutimuliwa, suala hilo bado linaisumbua CCM, si Kilimanjaro pekee bali hata mikoa mingine.

Akizungumza na viongozi wa mkoa huo, Kabaka anasema CCM iliambulia majimbo mawili mkoani Kilimanjaro kutokana na usaliti wa baadhi ya viongozi na wanachama, ambao mchana walikuwa katika chama hicho lakini usiku wanabadilika na kuwa wapinzani.

“Niwape pole kwa kuambulia majimbo mawili mwaka 2015, lakini niseme tu kwamba hali hiyo ilitokana na ninyi wenyewe, kwani mchana mnaimba iyena iyena lakini usiku mnageuka. Sasa uamuzi ni wenu, mkitaka mchana muendelee na iyena iyena na usiku mgeuke, mtajua wenyewe, kwani madhara yake mmeyaona.”

Pamoja na hatua zilizowahi kuchukuliwa kwa baadhi yao, Kabaka anasema huu ni wakati wa wana CCM kusameheana, kuondoa makovu na machungu ya uchaguzi uliopita na kujipanga kupata ushindi.

“Katika uchaguzi mkuu ujao 2020, CCM tunahitaji kushinda majimbo yote likiwemo la Moshi Mjini, sasa naomba mjipange. Ondoeni makundi, mshikamane kwa umoja kuusaka ushindi,” anasema.

Kauli ya usaliti iliungwa mkono na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya ambaye anaeleza kuwa mwaka 2015, chama hicho hakikushindwa na upinzani, bali wana CCM ambao waliamua kukisaliti chama.

“Ubinafsi na makundi ndiyo chanzo cha kushindwa kwetu. Mwaka 2020 tutashinda kutokana na mipango na mikakati tuliojiwekea. Historia inatuambia 2015 tulishindwa kwa sababu miongoni mwetu wana CCM wenyewe, ndiyo tulikuwa wasaliti na kusimama kidete, kuwapiga vita wagombea wa chama chetu, lakini pia makundi ya uchaguzi na mawakala wetu kutokuwa waaminifu,

vilichangia sisi kufanya vibaya.

“Ni miaka zaidi ya 20, jimbo la Moshi mjini liko upinzani, na hatushindwi na upinzani, ni sisi wenyewe. Tunakaa na kupanga mipango, baadhi ya viongozi wakitoka wanakwenda kuwauzia viongozi wa upinzani, hili ni tatizo kubwa ambalo limekuwa likitukwamisha.”

Kuhusu wagombea

Katika kusisitiza mshikamano, Kabaka anawataka wagombea ndani ya chama kuacha chokochoko dhidi ya watendaji wa chama ambao kazi yao ni kuratibu na si kuunga mkono wagombea.

Anawataka pia wagombea kuepuka udini katika siasa na kwamba mtu ambaye ataingiza udini, hatua zitachukuliwa dhidi yake kwa kuwa hilo ni kosa katika chama.

Waziri huyo wa zamani wa kazi, anawataka pia wakuu wa wilaya kuwa karibu na chama na kuhakikisha wanakuwa sauti ya chama kwa kusema yale ambayo yametekelezwa katika maeneo yao.

“Nawaomba makamisaa wetu, wawe karibu na chama na kuwasemea wabunge wetu wanachofanya, wanapokaa kimya na kuacha kusema utekelezaji wa ilani hawatutendei haki,” anasema.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM akizungumza na wananchi katika eneo la Kituo cha Afya Pasua, aliwasihi wananchi kuichagua CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2020 kama kurudisha shukrani.

“Ndugu wananchi, serikali imeendelea kutekeleza ilani ya CCM na kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo. Ingawa mnasema ‘vituo vya afya tunapata, maji tunapata, barabara tunapata ya nini kuichagua CCM’, niwaombe muichague kwa kuipongeza na kuishukuru kwa namna inavyowahudumia.”

“Nafikiri wananchi wa Moshi Mjini mmeshaona huyu CCM ambaye mnamkataa kila siku bado yupo na ninyi na mambo yote aliyoahidi anatekeleza bila kujali hajachaguliwa, sasa mpeni shukrani 2019 na 2020, kwa kumpa kura na hatutaacha kuwahudumia.”

Kauli kuelekea 2020

Ili kujihakikishia ushindi, Mabihya anasema kwa sasa watafanya kazi kwa umoja na ushirikiano kuhakikisha wanashinda uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi Mkuu 2020, na kwamba watachukua hatua kwa wale ambao watakiuka kanuni, sheria na taratibu za chama.

Hata hivyo, Alhaji Omari Shamba, mwenyekiti wa CCM Moshi Mjini, anakiri hali ya kisiasa kuwa ngumu na hivyo akaomba kuletewa viongozi wa serikali “ambao wameiva kichama” ili kuwa msaada kwao katika harakati za kulikomboa jimbo hilo.

“Hatusemi mkoa huu ni wa upinzani, lakini mnatambua ni mgumu kisiasa, tunaomba mkituletea viongozi wa serkali, tuleteeni ambao ni vindakindaki wa chama ambao tutakuwa na kauli moja anasema.

Shamba anatumia pia nafasi hiyo, kuomba viongozi wa serikali kukithamini chama na kuhakikisha wanatoa taarifa, pindi kunapokuwa na ujio wa viongozi katika maeneo yao.

Anataka mawaziri wanapofika mkoani humo, wahakikishe wanafika katika ofisi za CCM kutoa taarifa, ili uongozi wa chama nao ushiriki kwa kuwa zipo changamoto wanazozifahamu na wanaweza kuzitolea ufafanuzi.

“Wakati mwingine anakuja kiongozi, kama ilivyo leo kwa waziri mkuu lakini chama hatuna taarifa, tunabaki kupata taarifa mitaani, hii siyo sahihi,” anasema Shamba.

Wakati wengine wakilalamika, Mjumbe wa NEC ya CCM, Joseph Tadayo anasema hali ya siasa kwa sasa mkoani humo ni nzuri.

“Hali ya siasa kwa sasa imeanza kuimarika katika mkoa huu, na hii ni kwa sababu tuliwapata viongozi wazuri katika uchaguzi 2017 na watendaji tuliopewa nao wako vizuri, tukiendelea hivi, tuna imani kubwa ya kuibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu 2020”.

Anasema kazi kubwa wanayotakiwa kuifanya kwa sasa ni kujenga mahusiano mazuri na taasisi mbalimbali zikiwemo za dini na za kijamii kwa kuwa bila hilo watakabiliana na upinzani usio na sababu.



Chanzo: mwananchi.co.tz