Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upinzani majeruhi katika mchakato uchaguzi mkuu Okt

Act.webp Upinzani majeruhi katika mchakato uchaguzi mkuu Okt

Wed, 6 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKATI ikisalia miezi mitano ili kufanyika uchaguzi mkuu wa 2020, mchakato wa mchujo ili kupata wanachama sahihi wa kuviwakilisha vyama vya upinzani kwenye uchaguzi huo umeanza.

Baadhi ya vyama hivyo vimeanza kupiga hatua mbalimbali zikiwamo za kuruhusu wanachama wake kutuma mapema maombi ya kutaka kuwania ubunge na udiwani ili wapitishwe katika mchujo maalumu.

Chadema na ACT- Wazalendo ni miongoni mwa vyama hivyo, ambavyo kwa nyakati tofauti vimefanya mchakato wa kupata wanachama, ambao wanaamini hawawezi kuwaangusha.

Januari mwaka huu, Chadema ilifungua pazia kwa wanachama wake wanaotaka kuwania ubunge na udiwani kuandika barua za maombi kwenye maeneo yao ili majina wajadiliwe na vikao maalum.

Mchakato huo ulifungwa rasmi Machi 30 mwaka huu, huku joto likipanda kutokana na wingi wa wanachama waliojitokeza kuwania majimbo yenye wabunge wa chama hicho na hata kata.

John Mrema ni Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, ambaye anasema, kujitokeza kwa wingi kwa wanachama wa chama hicho kuwa ni nafasi mbalimbali kunaonyesha jinsi gani kinapendwa.

"Mambo yetu tunafanya kwa uwazi, ndiyo maana tukatangaza mchakato huo wanachama wakajitokeza na sasa tumeshafunga rasmi pazia, zinaendelea taratibu nyingine za kufanikisha mchakato huo," anasema Mrema.

Wakati Chadema imeshafikia hatua hiyo, ACT- Wazalendo nao wametangaza utaratibu utakaotumika kupokea watia nia wa nafasi za ubunge na udiwani kupitia chama chicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu, anasema, chama kitakutana na wadau mbalimbali na kuweka mpango mkakati ya kuwapokea wote wenye nia ya kuwania nafasi za uongozi hasa katika ngazi ya ubunge na udiwani.

"Sisi bado lakini wiki hii ndiyo tutatangaza utaratibu kwa watia nia wa ngazi za ubunge na udiwani kuanza kujitokeza, ili baadaye wapitie kwenye mchakato utakaowezesha kupata wagombea sahihi,” anasema Ado.

MAJERAHA

Hata hivyo, vyama vya upinzani vimeanza mchakato wa kuingia katika uchaguzi mkuu vikiwa vinauguza majereha ya kukimbiwa na wanachama wake wakiwamo viongozi, wabunge na madiwani.

Ilikuwa ni mwaka 2016 kasi ya wapinzani kurudi au kwenda CCM ilianza taratibu na kadri miezi ilivyokwenda, ndivyo kasi hiyo iliongezeka, huku vyama vikuu vya upinzani vikiathirika zaidi.

Hali hiyo imeendelea kuvikumba vyama hivyo na huenda miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu vikakimbiwa, hivyo ni wazi kwamba majeraha ya kukimbiwa yakazidi kuvikumba vyama hivyo.

Ikumbukwe kuwa katika hamahama hiyo, wabunge 10 wakiwamo saba wa Chadema na watatu wa CUF na madiwani 140 kutoka vyama mbalimbali vya upinzani wamejiunga na CCM.

Wote hao wamekuwa na sababu za kufanana, wanadai kukunwa na uongozi wa serikali ya awamu ya tano kwa jinsi inavyofanya kazi ya kuleta maendeleo, hivyo wakaamua waiunge mkono kwa kuhamia CCM.

Uhamaji huo umezusha hisia mbalimbali kutoka kwa wanasiasa huku baadhi wakidai kwamba sasa upinzani unahitaji kufanya uchunguzi wa mienendo ya wanachama wake kimaadili ili kuwapata wale ambao ni sahihi.

Kwamba hatua hiyo itasaidia kuepuka wale wanaotumia upinzani kama kichaka cha kutimiza malengo yao binafsi, bali wanaotambua kuwa upinzani kwao ni falsafa, itikadi, imani na wasioshawishika.

TUME YA UCHAGUZI

Mbali na majeraha ya kukimbiwa na wanachama na viongozi, upinzani pia una kilio cha kutaka tume huru ya uchaguzi, na vimeendelea kutaka ombi hilo lifanyiwe kazi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2020.

Katika kilio hicho, lipo pia suala la wasimamizi wa uchaguzi kuwa wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa na wilaya kwamba wawekwe pembeni kwenye mchakato huo.

Lengo la kilio ni kutaka kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ambayo inakubalika kwa vyama vyote vya siasa kama njia ya kuleta chachu na kukuza demokrasia nchini.

Muundo wa sasa wa tume hiyo umekuwa ukilalamikiwa kutokana na upatikanaji wa viongozi wake, ambapo upinzani unaamini kwamba unasababisha kupendelea upande mmoja.

Mojawapo ya mambo ambayo upinzani unatamani yafanyike ni japo kuweka viraka kidogo kwenye katiba ambayo yatatengeneza mazingira ya kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Tume huru inayotakiwa ni ile ambayo mwenyekiti na mkurugenzi wake hawateuliwi na rais na pia watendaji wake wakuu katika ngazi za halmashauri wasiwe ni wakurugenzi wa halmashauri.

Katika hilo, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, amewahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema, chama kilishamuandikia barua Rais John Magufuli kikimuomba afanye mabadiliko ya sheria yatakayowezesha kuundwa kwa tume huru kabla ya uchaguzi huo.

Kwamba kuna haja ya Rais Magufuli kuunda tume ya maridhiano kwa lengo la kuepusha malalamiko kutoka kwa vyama vya upinzani na wananchi kwa ujumla na kuwa na taifa lenye umoja na mshikamano.

Wakati upinzani ukiwa na ombi hilo, tayari serikali ilishasema kuwa imejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 unafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki.

Aidha, serikali imeshaahidi kwamba wakati ukifika itazikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia uchaguzi ili kujionea jinsi Tanzania inavyokomaa katika nyanja ya demokrasia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live