Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Upendo Peneza apuuza hoja ya mgombea kutooa

10517 Pic+peneza TanzaniaWeb

Tue, 7 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Wakazi wa Buyungu katika Mkoa wa Kigoma wametakiwa kupuuza hoja zinazotolewa na viongozi wa CCM wanaoshawishi wananchi wasimchague mgombea wa Chadema kwa kigezo cha kuwa bado hajaoa.

Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Ilagilo, Mgunzu, Kiduduye na Nyagwijima katika mikutano ya kampeni, mbunge wa viti maalumu (Chadema), Upendo Peneza alisema hoja ya kuoa au kuolewa ni dhaifu na imepitwa na wakati.

Alisema licha ya kwamba mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo, Eliya Kanjero hajaoa, hiyo haiwezi kuwa sababu ya kushindwa kuwawakilisha watu wa Kakonko ndani na nje ya Bunge.

“Leo hii mimi ni mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Geita lakini sijaolewa bado, lakini nimeaminiwa na naendelea kuwawakilisha wananchi na chama changu bila matatizo yoyote, ndio maana nawaambia hoja ya watu wa CCM kwamba Eliya hajaoa haina uzito na ni dhaifu,” alisema Peneza.

Ndani ya Bunge watu wanajadili masuala ya kitaifa na kimataifa, hawajadili mambo ya kuoa au kuolewa, hivyo hakuna jambo lolote litakalomshinda mgombea endapo atachaguliwa kuwa mbunge.

Mkurugenzi wa uchaguzi Chadema, John Mrema alisema chama imemwamini mgombea huyo kwa vile ana uwezo wa kuwawakilisha wananchi na kuwaletea maendeleo.

Licha ya kwamba hajaoa, Eliya ameaminiwa na kwa sasa ni diwani wa Kata ya Gwalama, mwenyekiti wa madiwani wa Chadema katika halmashauri ya wilaya Kakonko, mkoa wa Kigoma na Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi.

Akijinadi katika mkutano huo, Elia allisema akichaguliwa ataibua mradi wa maji uliohujumiwa miaka iliyopita licha ya kutengewa zaidi ya 60 milioni.

Mradi huo ulianza kutekelezwa kabla ya uchaguzi mwaka 2015.

Chanzo: mwananchi.co.tz