Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umoja wa vyama vya siasa  watoa pole kwa Watanzania

E9a074f9e057f8728d5a79010dc747ef.jpeg Umoja wa vyama vya siasa  watoa pole kwa Watanzania

Sat, 20 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

UMOJA wa vyama vya siasa mkoa wa Arusha umetoa pole kwa familia na Watanzania kwa kufuatia kifo cha Rais John Magufuli.

Salamu hizo za pole zimetolewa na viongozi wa vyama vya upinzani jijini Arusha ambavyo kwa pamoja wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia yale yote yaliachwa na Rais Magufuli ili kumuenzi na kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati wa juu na kuinua fursa za viwanda .

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini Mkoa wa Arusha, Simon Ngilisho alisema, “ lala salama Rais John Magufuli kwani ulikuwa ni kiboko ya mabepari, mpigania haki za wanyonge hasa wamachinga, tunakuombea kwa mola Mungu apumzishe roho yako mahala pema peponi.”

Alisema, Rais Magufuli amefanya mengi katika uongozi wake hivyo yale aliyoyaacha yaendelezwe kwa usimamizi wa Rais Samia Hassan Suluhu kwani ni mama shujaa, anayejua wananchi wanahitaji nini na kamwe watumishi waliopo madarakani wasidhani kuwa wanawake hawawezi bali wanawake wanaweza kuleta maendeleo kuanzia ngazi za familia na zinakuwa bora sanjari na kumudu majukumu mengine ya kiungozi.

“Tutampa ushirikiano wa kutosha Rais Samia na tunamuombea Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mola ampe nguvu zaidi katika kipindi hiki ,” alisema.

Mwenezi wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) Mkoa wa Arusha, Geofrey Stephen alisema TLP itamuunga mkono Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan kwani awali chama hicho kina imani kubwa na serikali na kinatoa pole kwa msiba huu uliotokea wa kifo cha Rais Magufuli.

“Rais amefanya mengi na ameacha mengine yanayostahili kuendelezwa hivyo ni vema yakaendelezwa kwani serikali ipo thabiti tuenzi uzalendo wetu na kuhakikisha Taifa letu linakuwa na umoja na kushikana mikono ili Taifa lisongembele,” alisema.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Sauti ya Umma(SAU) Mkoa wa Arusha ,Simon Bayo alisema wamempoteza kiongozi shujaa Afrika mwenye uthubutu katika maamuzi magumu na alitoa pole nyingi kwa Rais Samia Suluhu Hassan , Watanzania, viongozi mbalimbali wa dini, serikali na kusisitiza zaidi amani, mshikamano udumu zaidi katika kusimamia serikali.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Madini Tanzania, Sammy Mollel alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Rais Magufuli kwani alikuwa jemedari katika kusimamia biashara ya madini

Mollel aliyasema hayo jana wakati akizungumzia msiba wa Rais John Magufuli na kuongeza kuwa Rais Magufuli alisimama kidete kuhakikisha sekta ya madini inaleta tija kwa wananchi na kuiletea heshima nchi kwa kudhibiti utoroshaji wa Madini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz