Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Umeya Dar sasa pasua kichwa

91288 Pic+meya Umeya Dar sasa pasua kichwa

Fri, 10 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Umeya wa Jiji la Dar es Salaam umeendelea kuibua mjadala na mvutano baina ya Chadema, Serikali na CCM.

Chadema wanaamini kuna mpango wa kumng’oa meya wa Jiji la Dar es Salaam anayetokana na chama hicho, Isaya Mwita.

Wakati Chadema wakikimbilia mahakamani kuweka zuio ili kusifanyike uamuzi wowote na Baraza la Halmashauri ya Madiwani, Mahakama ya Kisutu leo itatoa uamuzi wa kukubali au kukaa maombi hayo ya zuio.

Hayo yakiendelea, mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana alitangaza kuahirisha kikao maalumu cha baraza la madiwani kilichokuwa kifanyike leo ambacho alikiitisha juzi na sasa kitafanyika kesho.

Hata hivyo, jana usiku Meya Mwita alisema wamepigiwa simu kuwa kikao hicho kitafanyika leo kama kilivyopangwa.

“Wameahirisha hadi kesho kutwa (kesho) kutokana na sababu zisizoweza kuzuilika. Lakini si unajua kuwa meya alienda mahakamani kuweka zuio? Kitafanyika Ijumaa,” alisema Abdallah Chaurembo, Meya wa Manispaa ya Temeke anayetokana na CCM. Hata hivyo, kikao hicho kitafanyika leo kama kawaida.

Diwani wa Tabata (Chadema), Patrick Asenga alisema, “nimeambiwa kikao kimeahirishwa hadi Ijumaa kwa sababu hawajajipanga vyema. Nadhani hii siyo sababu ya msingi wanasubiri uamuzi wa mahakama tu.”

Lengo la kikao hicho cha madiwani ni kupokea taarifa ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za Mwita baada ya tume iliyoundwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuchunguza tuhuma zinazomkabili meya huyo.

Miongoni mwa tuhuma anazokabiliana nazo Mwita ni kutotumia Sh5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda). Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa hisa za Uda.

Tuhuma nyingine ni madai ya kutumia vibaya gari la ofisi ambalo alipata nalo ajali, kushindwa kuongoza kikao cha baraza la madiwani na kusababisha meya wa Ubungo, Boniface Jacob kugombana na meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo na kudaiwa kuwapendelea baadhi ya mameya kuingia kwenye kamati za fedha.

Hata hivyo, Mwita ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema, alishajibu tuhuma hizo akisisitiza hahusiki na jambo hilo bali ni za kutengenezwa ili aondolewe katika kiti hicho alichokitumikia kwa miaka minne.

Jana, Meya Mwita kupitia wakili wake Hekima Mwasipu aliiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu izue kwa muda mchakato wa kumuondoa katika nafasi yake mpaka pale kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Pia, aliiomba mahakama iamuru iwapo kutakuwapo na kikao chochote kisijadili ajenda ya kumuondoa meya huyo kwenye nafasi yake bali kijadili maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mwasipu aliwasilisha hoja hiyo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Janeth Mtega wakati kesi hiyo ya madai namba tatu ya mwaka huu ilipotajwa.

Katika kesi hiyo Meya Mwita ni mleta maombi na wajibu maombi ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hata hivyo, Mwasipu aliiomba Mahakama iwape muda wa kujibu majibu kinzani na kujiandaa na usikilizwaji wa mapingamizi.

Alisema maombi yaliyopo mahakamani hapo yapo chini ya hati ya dharura ili kuzuia wajibu maombi ambao ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wasijihusishe katika mchakato wa kumuondoa meya.

Hata hivyo, Mwasipu aliieleza mahakama kuwa Januari 6, Mwita alipokea barua lakini kabla hajaeleza chochote naibu wakili mkuu wa Serikali, Gabriel Marata aliinuka na kumkatisha.

Alimtaka Mwasipu ajenge hoja kwa nini anataka maombi hayo na kuomba asizungumzie nyaraka ambazo zipo katika hati ya kiapo. Marata aliongeza kuwa Mahakama wala wao hawana hiyo barua inawezekanaje waweze kuitumia kuhalalisha maombi yao.

Akiendelea kujenga hoja, Mwasipu alisema Mwita ambaye ni mleta maombi katika kesi hiyo alipelekewa barua hiyo juzi na kuiomba mahakama isikilize kama kuna uhalali ama la.

Hata hivyo, Hakimu Janeth alimueleza Mwasipu aeleze kwa ufupi anataka nini. Baada ya kuelezwa hayo, Mwasipu aliomba kuzuiwa kwa wajibu maombi hao kumuondoa Mwita katika nafasi yake kwa kuwa wapo katika mchakato huo wakati kesi ipo mahakamani.

Pia, aliomba hata kama kuna kikao chochote wazuiwe kujadili ajenda hiyo ili kumpa hali ya kusikilizwa na kwamba hiyo haitaathiri chochote ili haki iweze kutendeka.

Kwa upande wa wakili Marata alipinga maombi hayo na kusema yamefikishwa mahakamani hapo Januari 6 chini ya hati ya kiapo.

Kuhusu mchakato wa kumuondoa Meya, Marata alisema hakuna kitu kama hicho.

Alidai mahakama wala upande wa mashtaka hawajui iwapo hicho kitu kitatokea ama la, hivyo itawezekanaje kuzuia tuhuma.

“Ni rai yetu mahakama hii ili iweze kutoa oda lazima kuwapo na kitu ambacho kipo kabisa,” alisema Marata.

Alisema Mahakama haiwezi kutoa amri kwa vitu ambayo havipo na kwamba kitu hicho hakipo wala hakiwezi kutokea. Hakimu Janeth aliahirisha kesi hiyo hadi leo atakapotoa uamuzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz