Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukomo wa Kikosi Kazi pasua kichwa

Kikosi Kazi Pic Data Ukomo wa Kikosi Kazi pasua kichwa

Tue, 19 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akitoa wito kwa Kikosi Kazi cha kukusanya maoni kukamilisha majukumu yake kwa wakati ili kisikwamishe utekelezaji wa sera za Rais Samia Suluhu Hassan.

Kufuataia kauli hiyo, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza muda wa kukamilisha majukumu hayo utajulikana baada ya kikosi hicho kutoka Zanzibar.

“Tukishatoka Zanzibar tutaanza kuandika ripoti lakini bado hatujajua ratiba, nafikiri kuanzia kesho (leo) tunaweza kufahamu lakini (wadau) wajue kwamba muda wa kukamilisha utafahamika baada ya kikosi kazi kutoka Zanzibar,” alisema Nyahoza.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akitoa maoni na mapendekezo yake ya kuimarisha demokrasia ya vyama vingi nchini mbele ya wajumbe wa Kikosi Kazi jijini Dar es Salaam, hivi karibuni. Picha ya Maktaba

Kikosi Kazi hicho kiliundwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, baada ya mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa uliofanyika jijini Dodoma Desemba 15 hadi 17, 2021 kikiwa na shabaha ya kupitia hoja zilizojitokeza kwenye mkutano huo ili kuboresha hali ya kisiasa nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye mkutano wake na vyombo vya habari, Profesa Lipumba alisema kwa kutokujiwekea muda wa kukamilisha majukumu hayo, Kikosi Kazi kinamkwamisha Rais Samia katika kutekeleza sera zake ikiwemo kupatikana Tume Huru ya Uchaguzi itakayoendesha uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

“Maneno mazuri hayatoshi, tunahitaji kuona muda wa utekelezaji kwa kuweka mikakati ya kukabiliana na suala hili la Tume turu ya uchaguzi itakayoendesha na kukamilisha mchakato wa kupata Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema kwa namna walivyokubaliana kwenye mkutano wa Dodoma, kikosi kazi hicho kilitakiwa ndani ya mwezi mmoja kiwe kimekamilisha mchakato huo huku lakini anashangazwa kuona kazi hiyo inaendelea hadi sasa.

“Tunataka kurekebisha na kulijenga upya Jeshi la Polisi, liheshimu haki za binadamu na liwe na weledi, Sheria ya vyama vya siasa ya 2019 na kuandaa Dira ya Taifa shirikishi,” alisema Profesa Lipumba.

Malengo mengine alisema ni kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji, kupambana na ufisadi, kujenga utawala bora, kutekeleza Malengo ya Maendeleo endelevu hivyo waweke muda wa kuhitimisha.

Kina kazi nyingi

Alipokutana na kikosi hicho na kupokea ripoti ya awali Machi 21, Rais Samia alisema kazi za kikosi hicho ni nyingi mno na zimepangwa katika muda mfupi, wa kati na mrefu.

“Na mmezipanga katika muda mfupi, wa kati na muda mrefu. Kwa hiyo Kikosi Kazi mmejihalalishia miaka tisa yote iliyobaki na mimi hapa. Na huku ndio kunaitwa kujiajiri wenyewe… lakini lengo ni kuwa na siasa zenye tija,” alisema Rais samia na kuacha wajumbe hao wakiangua kicheko.

Rais Samia alifafanua kazi za kikosi kazi hicho kuwa ni kuchambua masuala yote ambayo hayaleti siasa zenye tija, yanayosababisha kuonekane kuna chuki na kushauri namna ya kuboresha demokrasia nchini.

Wajilaumu wenyewe

Wakati hali ikiwa hivyo, Ali Makame, mchambuzi wa Siasa kutoka Zanzibar, alisema viongozi wa vyama vya upinzani wanapaswa kujilaumu wenyewe baada ya kushindwa kuitumia fursa ya Bunge maalumu la Katiba waliyoipata na matokeo yake wakaunda kitu kilichoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wakawa wamepoteza malengo yao.

“Ni kweli watu wanataka Katiba Mpya, Tume huru toka mwaka 1992, lakini wanapaswa kujua hata dunia haikuumbwa kwa siku moja, Mungu alitumia siku sita, kwa hiyo tunapotaka kupata mabadiliko ya kweli, huwezi kwenda na boksi la asilimia 100 ya mambo yote kutatuliwa,” alisema.

Alisema fursa ya Bunge la Katiba walitakiwa wasiipoteze, walitakuwa kuungana hata kusimamia mambo mawili tu -- Tume huru ya uchaguzi na matokeo ya uchaguzi yakiwa na mashaka yaruhusiwe kufikishwa mahakamani.

“Hata wazee wa Tanzania walipokuwa wanadai uhuru wangedai katiba mpya na tume huru hadi leo wasingefika, lakini wao walilenga umoja waliokuwa nao wakaamini tume na katiba hiyohiyo kwa umoja walionao na wingi utawapa wanachotaka.

Hawatapendezwa wote

Naye Mhadhiri wa UDSM, Dk Richard Mbunda alisema uundwaji wa kikosi kazi na namna kinavyotekeleza majukumu yake ni kama vile vyote vinategemea hisani kutoka kwa Rais na hiyo huenda ikawa sababu ya kushindwa kutoa muda.

“Hakitaweza kuwapendeza wadau wote ndiyo maana hata Chadema walishawahi kusema kikosi hicho kina lengo la kuchelewesha mchakato wa katiba mpya, hiyo inaonyesha namna gani wengine hawatambui, lakini ni vyema wakaangalia msingi wa kuanzishwa kwake,” alisema Dk Mbunda.

“Kiliundwa na nani? Na kwa misingi ipi na pengine kinaenda na namna Rais anavyotaka kushauriwa kwa uendeshaji wa siasa nchini, ndiyo maana hakiwafurahishi wengi kama aliyetoa hoja hizo,” aliongeza Dk Mbunda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live