Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Ukombozi Rorya unahitaji mtu makini, mwenye uchungu’

02e71566766f824645dd3c6ca325b4ac.png ‘Ukombozi Rorya unahitaji mtu makini, mwenye uchungu’

Mon, 20 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“NIMEZALIWA na kukulia hapa nikimsaidia mama kubeba na kuuza vyakula kutoka sehemu moja kwenda nyingine hadi sokoni hivyo, nimeona changamoto nyingi, lakini hazina wa kuzisemea kutokana na Rorya kuwa na pengo kubwa la uwakilishi; ndiyo maana nimeamua kukiomba baraka chama changu; Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili nigombee nikichaguliwa, nizitafutie ufumbuzi kupitia uwakilishi wenye tija kwa chama na wanachi kwa jumla.”

Ndivyo anavyosema kada wa CCM, Wambura Sasi; Gazeti hili lilipotaka kujua sababu zake kuwania uteuzi wa kugombea muda mfupi baada ya kuchukua fomu za kuomba CCM kimteue kugombea ubunge katika Jimbo Rorya mkoani Mara katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Sasi ambaye ni msomi mwenye Shahada ya Kwanza ya Utawala katika Biashara na Usimamizi wa Manunuzi na Ugavi (Business Administartion in Procurement and Logistic Management) kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Marogoro na sasa ni mjasiriamali, anasema ameomba kuingia kinyang’anyiro hicho ili kuondoa sumu iliyojengeka kuwa, mbunge wa Rorya lazima awe mfadhili, badala ya kuwa mwakilishi wa jimbo bungeni.

MwanaCCM huyo anasema endapo chama chake kitampitisha kugombea na wananchi wakampa ridhaa kupitia kura, vipaumbele vyake vitakuwa kushirikiana na wananchi na serikali yao, kuhakikisha adha wanazopata wanapotafuta huduma za afya, zinakoma huku akisitsisitiza kutumika vyema kwa rasilimali ya Ziwa Victoria kuwapa wananchi maji safi na salama sambamba na ajira kupitia uvuvi.

Anasema: “Asilimia 77.3 ya ardhi ya Rorya imezungukwa na maji ya Ziwa Victoria, lakini hakuna miradi ya maji safi na salama kutoka katika ziwa hilo hali anayosema akiingia madarakani atapambana nayo ili kuhakikisha Jimbo la Rorya linakuwa na miradi ya uhakika ya maji safi na salama ambayo ni endelevu.

“Hivi Rorya tuna tofauti gani na watu wa Dodoma, Shinyanga na Kahama ambao wako mbali, lakini wana miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria na badala yake, wakati wa mvua tunachangia maji na mifugo huku wakati wa kiangazi inakuwa shida kuyapata.”

Anasema uhaba wa maji hayo katika vijiji jimboni Rorya umesababisha wakazi kutumia muda mwingi kutafuta maji kutoka mbali, badala ya kuzalisha mali na pia, hali hiyo inasababisha migogoro ya kifamilia baina ya wazazi na watoto wao hasa wa kike, au wanawake na waume zao kutokana na wengine kutoaminiana.

“Tutashirikiana na wananchi kuibua miradi ya kuwezesha kuvuna maji ya mvua katika nyumba za bati na kuyatibu ili yasiharibike; hii itasadia ‘kumtua mama ndoo kichwani…” anasema mtiania huyo.

Kuhusu elimu, anasema amenuia kupambana na mateso wayapatayo wanafunzi hususan wa sekondari kwa kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani katika vijiji vyao kwenda katika shule za sekondari za kata hali ambayo ina madhara zaidi kwa wanafunzi wa kike.

“Ingawa kata nyingine hazina sekondari, zile zenye sekondari watoto wengi wa kike hawafanyi vizuri kutokana na umbali mrefu unaowatesa kutoka nyumbani kwenda shuleni; wakifika shuleni wamechoka na wakifika nyumbani, pia wamechoka hivyo hawawezi kufuatilia vyema masomo,” anasema.

Anaongeza: “Kwa mfano, mtoto anatoka Kitongji cha Kyamwame, Kata ya Komuge kwenda Shule ya Sekondari Suba; ni mbali sana. Hayo siyo mazingira rafiki kwa upatikanaji wa elimu bora.”

“Wengine wakiwamo wanafunzi wa kike wanalazimika kupanga na kuishi ‘gheto’ hali inayowaweka hatarini kubakwa na kukumbwa na vishawishi vinavyohitimishwa na mimba au ndoa za utotoni na hivyo, kuharibu ndoto zao za masomo.”

Anaongeza: “Kwa wanafunzi wa umri huo kuwa mbali na wazazi, walezi au walimu na kujitegemea wenyewe, wanapata uhuru wa kupindukia na matokeo yake, wanavutwa na kuingia katika uhuni kama uvutaji bangi, ufuska na hatimaye, kushindwa kuendelea na masomo.”

Sasi anasema: “Nitawekeza nguvu zaidi kujenga hosteli au mabweni ya wasichana ili wakae shuleni katika kata zote na kufuatilia vizuri masomo…”

Mpango mwingine anasema ni kuanzisha utaratibu wa kambi za masomo kwa madarasa ya sekondari yenye mitihani ya kitaifa kama Kidato cha Pili, Nne na cha Sita katika kila tarafa yaani, Suba, Luoimbo, Girango na Nyancha.

Kuhusu ajira, biashara na kipato, Sasi anasema anakusudia kushirikiana na wadau ikiwamo serikali kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vidogo na ufundi mbalimbali ili vijana watumie Ziwa Victoria kuanzisha bustani na mashamba ya kumwagilia katika kilimo chenye tija na kuhakikisha wanapata soko la uhakika la mazao ya kilimo na uvuvi.

Anasema: “Hii itafanya hata wanunuzi kutoka nchini Kenya waje na hivyo, kuiwezesha pia serikali kupata mapato kutokana na ujasiriamali endelevu na pia, kushirikiana na wananchi kuwezesha kila kijiji kuwa na miradi huku wafugaji wakiwa na majosho na mabwawa kwa ajili ya kunyweshea mifugo.”

Anasema: “Hata kukosekana kwa stendi maalumu ya basi na magari mengine kutoka vijiji mbalimbali kunawakosesha mapato Wanarorya kwa kukosa biashara imara ikiwamo ya bodaboda na vibanda vya biashara kuzunguka stendi ambavyo vitaiwezesha hata halmashauri kukusanya mapato huku wananchi wakipata huduma kwa ukaribu.”

Anasema endapo chama kitampa ridhaa na wananchi kumchagua, atashirikiana na wadau wengine ikiwamo Serikali kuvutia wawekezezaji wa viwanda hususan vya samaki ili kuimarisha soko la samaki na kuongeza ajira kwani kwa sasa hakuna kiwanda hali inayofanya mazao mengi ya uvuvi kuuzwa kwa bei ya chini na mengine kuharibika na kuwa hasara kwa wavuvi wa Rorya kutokana na kukosekana kwa miundombinu bora kama barabara.

“Rorya hakuna soko la uhakika la samaki na dagaa hivyo wanauzwa Rorya, Tarime, Musoma na mikoa mingine, lakini soko katika maeneo hayo limejaa kwa sababu maeneo hayo kama Mwanza, Bukoba na Musoma nayo yanavua hivyo soko ni hafifu,” anasema.

“Kutokana na tija ndogo,” Sasi anasema: “Nikipata uwakilishi, nitatumia kipato na nafasi yangu kudhamini upatikanaji wa mikopo benki na hivyo, kuchochea uvuvi wa kisasa wenye tija ili kwa kuanzia, walau tuwe na vizimba viwili ziwani ili kukuzia vifaranga wa samaki na hali itakayoongeza mapato ya watu na kuboresha jimbo kuwa na kipato cha kudumu.”

Kuhusu huduma za afya, anasema ataweka nguvu kubwa kuhakikisha kwa kushirikiana na Serikali na wananchi, kila kijiji kinakuwa na zahanati ili mpango wa bima ya afya unaotiliwa mkazo na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, uwe na tija zaidi hata kwa Wanarorya. Jimbo la Rorya lina vijiji 89, lakini vyenye zahanati ni 39 huku kukiwa na vituo vya afya vitatu vya Utegi, Kinesi na Changuge.

“Hii itaepusha watu kutumia gharama kubwa kutafuta huduma za afya mbali au katika hospitali za taasisi binafsi ambazo zipo Kowak na Shirati maana wengine wanakataa na kuugulia nyumbani kutokana na umbali huku wakunga wa jadi kwa ajili ya kusaidia wajawazito nao wakizidi kupungua, hali hiyo inahatarisha usalama wa wajawazito wanaojifungulia nyumbani.”

Chanzo: habarileo.co.tz