Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukimya ulivyotawala upigaji kura serikali za mitaa

85810 Pic+ukimya Ukimya ulivyotawala upigaji kura serikali za mitaa

Mon, 25 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/mikoani. Upigaji kura kwa ajili ya kuchagua viongozi serikali wa mitaa, vitongoji na vijiji umefanyika katika mikoa mbalimbali, huku ukimya ukitawala maeneo mengi.

Pamoja na ukweli kwamba siku ya kupiga kura huwa haina shamrashamra, harakati za wafuasi wa vyama na mivutano ya mawakala katika vituo vya kupigia kura, huchangamsha siku hiyo.

Lakini hali ilikuwa tofauti jana wakati sehemu kubwa ya nchi ikichagua viongozi wachache baada ya zaidi ya asilimia 90 ya wagombea kutangazwa washindi.

Wakati uchaguzi huo, ukiendelea vitongoji vitatu vya Paris, Rahaleo na Ruheya katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara vimeshindwa kufanya uchaguzi baada ya wagombea kushindwa kujitokeza kuchukua fomu katika mchakato huo.

Kutokana na hali hiyo msimamizi wa uchaguzi wa wilaya hiyo, Ahmed Suleiman alisema mchakato huo umeahirishwa hadi Desemba 15.

Katika vituo vingi vya kupigia kura, mwitikio haukuwa wa kuridhisha na maeneo mengi yalionekana kuwa wazi huku wapigakura wakienda mmoja mmoja.

Wakati hayo yakiendelea, mikoa ya Tanga, Katavi na Rukwa haikufanya uchaguzi huo baada ya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa.

Upigaji kura umefanyika huku vyama vya CUF, ACT- Wazalendo, Chadema, Chaumma, UPDP, NCCR-Mageuzi pamoja na NLD na CCK vilivyokuwa na mzozo, vikiwa vimejitoa kwa madai ya kufanyiwa mchezo mchafu na wasimamizi wasaidizi.

Hata hivyo, vyama vya ADC, TLP, AAFP, DP na Ada Tadea vimeshiriki.

Katika maeneo mbalimbali ambayo wananchi walitakiwa kupiga kura, ukimya ulitawala na hakukuwa na harakati wala mivutano ya mawakala wa misululu ya watu vituoni.

Mwenyekiti waTLP, Agustino Mrema alilalamikia kufanyiwa hujuma na baadhi ya mawakala wake kwenye jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro kuondolewa vituoni.

Mrema ambaye alishiriki katika kijiji cha Kiraracha anakoishi, alidai aliamua kushiriki uchaguzi huo ili kumsaidia Rais John Magufuli lakini hajatendewa haki.

Hata hivyo, msimamizi wa uchaguzi Moshi Vijijini, Juma Tukosa alisema hali inakwenda vizuri na kwamba wakala anayelalamikiwa na Mrema alikuwa anakunywa pombe eneo la kituo na akaambiwa aziondoe ndipo alipoanza kulalamika kuwa anaondolewa kituoni.

Katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga na Arusha, licha ya vyama Chadema na ACT-Wazalendo kujitoa, majina ya wagombea wao yalikuwa katika karatasi za kura.

Mkoani Shinyanga katika kata 17, zilizopo manispaa ya Shinyanga nne ndizo zilizokuwa na upigaji kura huku mwitikio ukiwa wa wastani.

Kwa mkoa wa Dar es Salaam, upigaji kura ulifanyika katika mitaa ya Buguruni Malapa na Mikoroshini kwa ajili ya kuchagua wajumbe baada ya wenyeviti wa mitaa kupita bila kupingwa.

Hali katika Mtaa wa Buguruni ilikuwa shwari na kulikuwa na ulinzi wa polisi, huku watu wakionekana wachache vituoni.

Mkazi wa mkoa huo, Juma Boniventure alisema pamoja na kujitokeza kupiga kura, aliona hamasa ndogo kwa wananchi licha ya baadhi ya vyama vya upinzani kushiriki.

Wilayani Tandahimba vyama vya CCM na TLP ndivyo vilichuana kumpata kiongozi wa kitongoji cha Kiwanjani sambamba na wajumbe mchanganyiko wa Kijiji cha Nahnyanga C.

Chanzo: mwananchi.co.tz