Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ukifanya haya, unamnyang’anya kura mgombea unayemtaka

EjEbMqvXcAApEW Ukifanya haya, unamnyang’anya kura mgombea unayemtaka

Wed, 30 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

OKTOBA 28, 2020 inazidi kusogea ili Tanzania ifanye Uchaguzi Mkuu wa sita katika mfumo wa siasa wa vyama vingi ulioanza nchini mwaka 1992 kuchagua rais, wabunge, wawakilishi na madiwani.

Uchaguzi mkuu wa kwanza katika mfumo huo ulifanyika mwaka 1995 na kumweka madarakani Benjamin Mkapa kuwa Rais wa Awamu ya Tatu.

Mchakamchaka wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu unazidi kushika kasi kwa vyama mbalimbali.

Katika mikutano mbalimbali ya kampeni, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli, anawahimiza Watanzania akisema: “Niwaombe kwa dhati, ikifika tarehe 28 mwezi wa 10 (mwaka huu) mwende mkapige kura kuichagua CCM, utaona picha na jina langu Magufuli na Mgombea Mwenza, Samia Suluhu… na wabunge na madiwani wa CCM, weka vema kwenye jina langu.”

Anasisitiza: “Msifanye kosa la kuacha kwenda kupiga kura eti kwa kusema tu kuwa tayari Magufuli ameshinda. Hilo ni kosa nendeni mpige kura mnichague na mchague wagombea wa CCM (siyo nukuu halisi).”

Hiyo, inanikumbusha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 ambapo aliyekuwa mgombea urais wa NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema alivuma kiasi cha baadhi ya wafuasi wake, kumbeba na kusukuma gari leke. Hali hiyo ilimfanya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuwataka askari polisi wasiwazuie wafuasi wa Mrema waliokuwa wakimbeba na kusukuma gari lake.

Ikawa asubuhi, ikawa jioni. Siku ya uchaguzi ikawadia. Mrema ‘akaangukia pua’.

Hii ikaashiria kuwa, kumbe waliokuwa wakimshangilia, kumbeba na hata kusukuma gari lake, wengi hawakuwa wapigakura,bali wapigadebe maana walikuwa vijana wadogo watu wengine wasio na sifa za kupiga kura maana kwenye msafara wa mamba, kenge hawakosekani.

Watu wengi katika mijadala tofauti, walisema hata wafuasi hao waliokuwa na sifa za kupiga kura, wengi walibweteka wakidhani umati ule kwa Mrema ndio ulikuwa ushindi tosha, hivyo hawakuona sababu ya kujitokeza siku ya kupiga kura ili wampigie, ‘wakalala usingizi’ na kusubiri ushindi wa miujiza.

Hali ilikuwa tofauti kwa mgombea wa CCM (Mkapa) ambaye licha ya kuwa na wafuasi na wapigakura wengi wenye sifa, waliojitokeza walikuwa wapigakura halisi na walijitokeza siku ya uchaguzi na kuchagua vema kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za ushindi.

Mkapa akaibuka mshindi na kuliongoza taifa kwa miaka 10. Makamu wa Rais ambaye pia ni Mgombea Mwenza wa CCM, Samia Suluhu yeye anasisitiza watu kujitokeza kupiga kura kwa umakini akisema: “…Kutokana na namna alivyotumikia Watanzania, ni wazi Dk Magufuli ameshinda, lakini lazima kupiga kura kwa wingi ili apate ushindi na hasa zaidi, apate ushindi wa heshima zaidi… (siyo nukuu halisi).”

Kimsingi, kumnyima kura mgombea unayemtaka na kuchagua mgombea usiyemtaka kunaweza kujitokeza kwa namna mbalimbali ikiwamo ya uzembe wa kutojitokeza kupiga kura; pamoja na kukiuka taratibu za upigaji kura, hivyo kusababisha kura yako kuharibika.

Ndiyo maana ninasisitiza kuwa, kutojitokeza kupiga kura kwa usahihi, ni sawa na kumchagua na kumpa ushindi mgombea usiyemtaka na kumnyang’anya kura mgombea unayemtaka.

Hapo, wakati wa matokeo, usishangae kusikia ‘usiyemtaka kaja’ na mgombea ubunge au udiwani uliyemtaka amekwama maana amekwama kwa kazi ya mikono yako.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ili kuepuka kunyang’anya kura mgombea unayemtaka kwa kuharibu kura yako, weka alama ya vema kwa mgombea unayetaka kumchagua na zingatia kuweka alama hiyo kwenye chumba maalumu kilichowekwa kwa ajili ya mgombea wako.

Kimsingi, Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 uoneshe umakini na ukomavu wa Watanzania kwa kila mmoja kutumia hekima na akili zake kuhakikisha anajitokeza siku ya kupiga kura, anapiga kura na kura yake haiharibiki.

Vyanzo mbalimbali vinataja namna ya kura inavyoharibika kuwa ni pamoja na mpigakura kupiga kura yake kwa wagombea zaidi ya mmoja kwa nafasi moja ya uongozi.

Kwa mujibu wa Nec, kura huharibika pia unapoweka alama au maandishi yoyote yanayokutambulisha mfano, kuandika jina lako wewe mpigakura, au kumpigia kura mgombea aliyejitoa.

Kuharibika kwa kura pia kunaweza kutokea kwa kufanya mambo mengine kadhaa bila kujua kuwa kwa kufanya hivyo, unamnyang’anya kura mgombea unayetaka apate ushindi ili akuongoze kuelekea maendeleo na mafanikio mnayoyataka.

Haya ni pamoja na kumwekea alama ya vema unayemtaka na kisha kukata au kuchafua usiyemtaka.

Hilo ni kosa; ni kumdhulumu na kumnyang’anya kura mgombea unayemtaka. Namna nyingine inayoharibu kura ambayo ingempa ushindi mgombea wako, ni kumwekea alama ya vema unayemtaka kisha kwa kudhani unampenda, ukaongeza kuweka maneno mengine kama maandishi au michoro kitu ambacho ni kinyume na taratibu za kupiga kura; ni kuharibu kura.

Hiyo nayo, ni moja ya njia wanazotumia watu bila kujua, hivyo wapigakura wengi kujikuta wamewanyang’anya kura wagombea wanaowapenda na kuwapa wagombea wasiowataka. Kwa kuepuka hilo, CCM wanajitahidi kutoa elimu ya mpigakura katika kila mkutano wa kampeni ili wapigakura wao waelewe na kuepuka makosa.

Namna nyingine ya kufanya kosa la kuharibu licha ya madhara yake kuwa makubwa kwani mnaweza kupata kiongozi anayejitumikia na kutaka kutumikiwa, badala ya kiongozi anayetumikia watu, ni kujiamini kupita kiasi hadi kufikia hatua ya kuchukua karatasi ya kupigia kura, ukaiacha bila kuweka vema mahali popote hasa kwa mgombea unayemtaka.

Hiyo, nayo inahesabiwa imeharibika. Ndiyo maana ili kumpa ushindi mgombea unayemtaka, nenda kapige kura siku ikiwadia, piga kura kwa mgombea mmoja kwa kila nafasi, usiweke alama au maandishi mengine mbali na alama ya vema inayotakiwa kuwa katika kisanduku maalumu na usiache karatasi ya kura bila kuweka alama moja ya vema kwa mgombea unayemtaka.

Kumbuka kuwa, kwenda kinyume na utaratibu wa kupiga kura, ni kuharibu kura na kuharibu kura maana yake ni kumchagua na kumpa ushindi mgombea usiyemtaka na kumpora ushindi mgombea unayempenda

Chanzo: habarileo.co.tz