Dar es Salaam. Vyama vya siasa vitaanza kufanya uhakiki kuanzia Machi 27 hadi Aprili 20, 2020 licha ya Msajili wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Jaji Francis Mutungi kukiri vinapitia hali ngumu.
Mutungi ameyasema hayo leo Jumanne Machi 10, 2020 alipokutana na viongozi wa vyama vya siasa kuelezea umuhimu wa uhakiki huo ikiwa ni pamoja na kuwa na fursa ya kuelezea changamoto zinazowakabili.
Amesema kutokana na hali ngumu baadhi ya vyama vimeomba kusogezwa kwa muda wa uhakiki lakini amesisitiza uhakiki huo ufanyike katika muda huo.
“Mimi kama msajili mnaniita mlezi wenu nitaendaje kwenye uongozi serikalini kusema vyama vina shida hii kwa kigezo ni kipi? Ni kwa kigezo cha uhakiki niliofanya,” amesema Mutungi
Mwenyekiti wa chama cha UDP, John Cheyo amesema kutokana na changamoto ya muda kuwa mfupi itakuwa ngumu kwao kujirekebisha.
“Lakini sheria imetungwa mwaka huu, tuna uchaguzi mwaka huu, na uhakiki mwaka huu tutajirekebisha kwa muda gani” amesema Cheyo.
Pia Soma
- Mamia wamlilia baba Kanumba, kuzikwa kesho
- Chadema wachangishana fedha usiku kuwatoa kina Mbowe rumande-VIDEO
- MPYA: Mbowe, wenzake washindwa kulipa faini Sh350 milioni, kulala rumande-VIDEO
Naye Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chadema, Benson Kigaila amesema orodha ya wanachama wa chama cha siasa ni sawa na usajili wa wapiga kura na wanachama wanakuwa hai kama wanatembelewa.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Abdallah Juma Saadala amesema anaunga mkono mchakato huo uendelee huku Mwenyekiti wa Chauma, Hashim Rungwe akiwataka wanachama kukaa tayari kwa uhakiki huo.
Uhakiki huo umekuwa ukifanyika kila mwaka kasoro mwaka 2019 na 2018 kutokana na mchakato wa kuandaa sheria ya vyama vya siasa na watakutana baada ya Aprili 20, 2020 kufanya majumuisho.