Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ugomvi mwingine wanukia sakata la umeya wa Dar es Salaam

92053 Meya+pic Ugomvi mwingine wanukia sakata la umeya wa Dar es Salaam

Thu, 16 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kikao cha Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kimeitishwa leo na huenda kukatokea mwendelezo wa mvutano wa kugombea umeya wa jiji la Dar es Salaam.

Meya aliyeng’olewa, Isaya Mwita, ambaye anang’ang’ania kuwa yeye bado anashikilia kiti hicho atakuwa na nafasi ya kupima upepo wa nafasi yake wakati atakapojaribu kuongoza kikao hicho.

Kwani tayari Naibu Meya wa jiji hilo, Abdallah Mtinika ameiambia Mwananchi kuwa yeye ndiye atakayeongoza kikao hicho baada ya Mwita kuondolewa nafasi yake.

Hata hivyo, Mwita, ambaye ni diwani kupitia Chadema kwa upande wake amesisitiza leo atakwenda kuongoza mchakato huo.

Kwa mujibu wa barua ya wito ambayo Mwananchi imeiona, kikao hicho kitafanyika katika ukumbi wa Karimjee kuanzia saa 8.00 mchana.

Miongoni mwa ajenda za kikao ni pamoja na kusoma na kuthibitisha muhtasari wa kikao cha kamati ya fedha na uongozi kilichofanyika Desemba 23 mwaka jana na taarifa ya mapato na matumizi ya mwezi huo.

Pia kikao hicho kinatazamiwa kupitia taarifa ya wito iliyotolewa na Mkurugenzi wa jiji, Sipora Liana.

Kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, mwenyekiti wa kikao hicho ni meya lakini hadi sasa bado kuna sintofahamu na utata wa nani atakayeongoza mkutano huo leo.

Sintofahamu hiyo inatokana na utata uliojitokeza katika mkutano mkuu maalum wa baraza hilo uliofanyika Januari 9 mwaka huu ambao wajumbe 16 wa CCM walipiga kura ya kutokuwa na imani na Mwita kutokana tuhuma zinazomkabili.

Miongoni mwa tuhuma anazokabiliawa nazo Mwita ni kutotumia Sh5.8 bilioni za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Udart).

Fedha hizo ni asilimia 51 ya hisa zilizotolewa na kampuni ya Simon Group kama sehemu ya ununuzi wa asilimia 51 ya hisa za Uda.

Wakati tuhuma nyingine ni matumizi mabaya ya gari la ofisi ambalo liligongwa wakati likiwa na dereva wake.

Hata hivyo, kwa nyakati tofauti Mwita amekana kuhusika na tuhuma hizo akidai si za kweli na kwamba zina lengo la kumwondoa katika nafasi hiyo aliyohudumu kwa miaka minne.

Hata hivyo, wafuatiliaji wa siasa za jiji la Dar es Salaam wanadai huenda suala la fedha za Udart likajadiliwa kwenye kikao hicho.

Madiwani walioongoza harakati za kumng’oa walimtupia lawama Mwita kwa kuzuia kutumika kwa fedha hizo.

Jana Mwananchi lilimtafuta Naibu Meya wa jiji hilo, Mtinika kutaka kujua nani atakayeongoza kikao hicho ambaye alijibu, “Mimi ndiye nitakayeongoza na si mwingine nawakaribisha watu wote,” alisema Mtinika ambaye ni Diwani wa Kibondemaji Mbagala.

Wakati Mtinika akieleza hayo, Mwita ambaye ni Diwani wa Vijibweni licha ya kutopewa barua ya wito wa kikao hicho yeye amedai bado ni meya na kwamba leo ataongoza kikao hicho kama mwenyekti akidai yeye ndiye mtu sahihi ya kukiongoza.

“Inawezekana wamepeleka barua ya wito ofisini, maana leo (jana) sijaenda, nipo nyumbani. Kesho (leo) nitakwenda kuongoza kikao hicho kwa sababu ndiye mwenyekiti,” alisema Mwita, ambaye amedai kwa sasa ameamua kufanyia shughuli za umeya nje ya ofisi kutokana na kuhofia usalama wake.

“Nimeamua nitawatumikia wakazi wa Dar es Salaam nje ya ofisi, pale Karimjee. Ndani siwezi kuingia hadi mambo yatakavyokuwa shwari,” alisema Mwita.

Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho, Patrick Assenga alisema amepewa barua ya wito, huku akisema endapo mwenyekiti wa mchakato huo hatokuwa Mwita hakuna kitakachofanyika.

“Ninachojua mwenyekiti wa kikao ni Mwita si mtu mwingine. Tunakwenda tukijua mwenyekiti wetu ni Mwita vinginevyo hatutaelewa,” alisema Assenga, ambaye ni diwani wa Tabata.

Chanzo: mwananchi.co.tz