Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uenyekiti upinzani unavyomaliza vigogo

Mgogoro CUF.png Uenyekiti upinzani unavyomaliza vigogo

Fri, 12 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Mgogoro ndani ya CUF uliosababisha viongozi saba kufukuzwa uanachama na makada saba kuonywa, umekoleza hoja ya siku nyingi ya jinsi mikakati ya kusaka uongozi katika vyama inavyowaponza wengi kwenye vyama vya siasa nchini.

Nafasi ya uenyekiti imekuwa ikitajwa kama kwanja linalowafyeka vigogo wengi wanaojaribu kushindana na wanaotetea nafasi hiyo katika sura ambayo wengine huitazama kama usaliti dhidi ya viongozi waliopo.

Baadhi ya waliowahi kukumbwa na kwanja hilo ni Profesa Abdallah Safari, Zitto Kabwe, Samson Mwigamba, Profesa Kitila Mkumbo, Frederick Sumaye, Bernard Membe na wengine wengi.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wameliambia Mwananchi kuwa migogoro mingi huibuka nyakati za uchaguzi ndani ya vyama na matokeo yake hudhoofisha vyama, hukimbiza watu na wanaobaki huamua kukaa kimya.

Wamesema migogoro mingine inayotokea kwenye vyama vya upinzani husababishwa na nguvu zilizo nje ya vyama ambazo zikikutana na ukinzani husababisha migogoro isiyokoma.

Mmoja wa wachambuzi hao, Abdul Hamduni, amesema baadhi ya wanaotaka kuwania uenyekiti ndani ya vyama wanakuwa hawana historia nzuri za kuimarisha vyama, hivyo hutuhumiwa kushirikiana na watu kutoka nje kuvuruga vyama husikia.

Alisema wanachama wa vyama vya siasa wanajuana udhaifu na uimara wao, hivyo anapotokea mwenzao kutaka kuwania uenyekiti na kumng’oa aliyepo, huonekana msaliti anayetumiwa kuvihujumu.

Makosa yanayofanyika

Mwanazuoni maarufu nchini, Profesa Issa Shiji akiwa Zanzibar kwenye uzinduzi wa Taasisi ya Maalim Seif wiki iliyopita, alisema miongoni mwa makosa wanayoyafanya viongozi wenye ushawishi nchini ni kutowaandaa warithi wa nafasi zao mapema.

Alisema viongozi hao hulazimika kuongoza kwa muda mrefu kwa kuwa kila wakitaka kuacha madaraka, wanachama wao huwaomba waendelee kwa kuwa hawaoni mtu imara zaidi wa kuimarisha chama husika.

“Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad mwaka 2020 hakutaka kuwania urais wala kuwa makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, lakini wanachama na viongozi wake walimlazimisha aendelee na akalazimika kufanya hivyo,” alisema.

Akijadili suala hilo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Onesmo Kyauke alisema masilahi na kung’ang’ania madaraka ni miongoni mwa changamoto zinazoibua migogoro kwenye vyama vya siasa vya upinzani, hasa vinavyopata ruzuku kutoka serikalini.

Dk Kyauke ambaye ni mwanasheria alisema suala la masilahi, hasa ruzuku ni chanzo cha migogoro ambako baadhi ya wanachama huwa wanaibuka na kuelezea mwenendo usioridhisha wa matumizi ya fedha za ruzuku.

“Angalia vyama vyenye mgogoro ni vile vinavyopata ruzuku, mbona hatusikii vyama vidogo kama UDP au DP. Ung’ang’anizi wa madaraka ni sababu nyingine pia, yaani chama kimekuwa mali ya mtu binafsi, hakuna demokrasia.

“Ikitokea mtu anasema kwenye chama fulani apumzike, basi inakuwa shida na mgogoro. Lazima vyama vijue fedha za ruzuku ni kwa ajili ya uendeshaji wa vyama, pia viimarishe demokrasia, sioni sababu ya mtu kukaa kwenye uenyekiti zaidi ya miaka 10,” alisema Dk Kyauke.

Migogoro ya vyama

Mwaka 2009 CUF iliingia katika mgogoro wa kambi za wagombea uongozi wakati wa uchaguzi wa ndani ambapo Profesa Safari alikuwa anawania uenyekiti na Profesa Ibrahimu Lipumba, ambao uliisha baada ya Profesa Safari kujivua unachama na kujiunga na Chadema.

Vyama vingine vilivyowahi kukumbwa na sintofahamu wakati wa uchaguzi ni NCCR-Mageuzi, UDP na TLP, Chadema na UPDP ambavyo kila kimoja kimewahi kuwafukuza baadhi ya wanachana na wengine kuvihama.

UDP, iliyowahi kupata wabunge wanne mwaka 1994 na 2000, ilikumbwa na mgogoro wa uongozi baada ya mwenyekiti wake, John Cheyo kupinduliwa mkutanoni na nafasi yake kuchukuliwa na Nzugule Amani Jidulamabambasi, ambaye hata hivyo hakudumu kwenye nafasi hiyo kutokana na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kutomtambua.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 1995 ambao Augustine Mrema aliongoza upinzani kupitia NCCR-Mageuzi, ulizuka mgogoro kati ya kambi yake na ile ya aliyekuwa katibu mkuu, Mabere Marando na alipozidiwa alihamia TLP.

TLP nako alikumbana na mshikemshike baada ya kutofautiana na aliowakuta waliotaka apatiwe mpinzani katika nafasi ya uenyekiti. Mwaka 2013 Chadema iliwavua uongozi wanachama wake watatu, Zitto, Profesa Kitila na Mwigamba ambao wanadaiwa waliandaa waraka wa kuupindua uongozi uliokuwa chini ya Freeman Mbowe.

Zitto alikuwa kwenye mtafaruku mkubwa ndani ya chama hicho tangu alipotangaza kuwania uenyekiti akikabiliana na Mbowe, lakini mwishoni aliamua kujiondoa baada ya wazee kumkalisha kikao cha kumtaka amuachie Mbowe.

Februari 28, 2020 aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alifukuzwa uanachama CCM kwa kwenda kinyume cha utaratibu wa chama hicho, ingawa mwenyewe alisema sababu kubwa ya uamuzi huo ni kutokana na dhamira yake ya kumkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM, hayati John Magufuli katika kuwania urais wa 2020.

Desemba 4, 2019 Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye akiwa na miaka minne tangu ajiunge na upinzani akitokea CCM, aliamua kujiondoa Chadema baada ya kushindwa kutetea Uenyekiti wa Kanda ya Pwani akiwa mgombea pekee.

Sumaye pia alikuwa amechukua fomu ya kuwania uenyekiti wa Chadema akikabiliana na Mbowe, lakini alijiondoa katika kinyang’anyiro na kujivua uanachama kwa alichokisema chama hicho hakina demokrasia.

Kauli za waathirika

Katibu mkuu wa zamani wa ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba alizitaja sababu za migogoro kuwa ni umiliki wa vyama na vyama hivyo kuendeshwa kama taasisi binafsi.

“Kumekuwa na hali ya watu kumiliki vyama badala kuviacha kujiendesha vyenyewe kama taasisi, hata tulipoanzisha ACT-Wazalendo, tulijitahidi kisionekane kinamilikiwa na mtu fulani, lakini juhudi hizo ziligonga mwamba. Nyie ni mashahidi kilichotokea baada ya watu fulani kuingia na kundi lao.

“Kulitokea mgogoro na mtafaruku mkubwa na ACT-Wazalendo ilionekana ya mtu fulani, hili ni tatizo kubwa na linaviumiza vyama vya upinzani. Ikitokea umetofautiana na mmiliki au mwenyekiti basi utapata tabu,” alisema.

“Ndiyo maana ukigusa nafasi ya uenyekiti linaibuka tatizo kubwa, mfano Profesa Lipumba ana kitu gani kipya cha kuifanya CUF inyanyuke hapa ilipo? Akiambiwa apumzike ni tatizo, ubinafsi umejaa katika uendeshaji wa vyama. Hapa ndipo CCM inapowapiga bao,” alisema Mwigamba.

Kwa upande wake, Profesa Safari alisema ubinafsi na mtizamano ni miongoni mwa sababu za migogoro ndani ya vyama vya siasa vya upinzani.

“Niliwahi kugombea uenyekiti wa CUF, lakini nilifanyiwa mambo ya ajabu ambayo siwezi kuyataja hapa, CCM wana matatizo lakini wamejitahidi katika suala la demokrasia. Lakini kilichopo kwenye vyama vya upinzani ni ubinafsi na kutokuwa na demokrasia,” alisema.

Chanzo: mwananchidigital