Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchaguzi wa wabunge majimbo tisa waja na jambo jipya

10337 Pic+uchaguzi TanzaniaWeb

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Agosti 12 ikiwa ni siku ya kupiga kura kwa wananchi wa Jimbo la Buyungu na kata 37, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imetangaza uchaguzi mdogo katika majimbo mengine matatu na kata mbili.

Hali hiyo imewafanya wasomi kuja na ushauri ambao utasaidia kubana matumizi ya kuendesha chaguzi hizo ndogo.

Tangu ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 hadi itakapofika Septemba 16, mwaka huu, jumla ya chaguzi ndogo tano zitakuwa zimefanyika kwenye majimbo tisa na kata 86.

Uchaguzi mdogo wa kwanza ulifanyika Novemba 26, 2017 katika kata 43; ulifuata mwingine wa Januari 13 mwaka huu katika kata sita na majimbo ya Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido.

Februari 17, ulifanyika uchaguzi mdogo wa tatu kwenye kata nne na majimbo mawili ya Kinondoni na Siha.

Uchaguzi utakaofuata utafanyika Agosti 12 ukihusisha kata 37 na Jimbo la Buyungu ambalo mbunge wake, Kasuku Bilago (Chadema) alifariki dunia.

Nec imeshatangaza uchaguzi mwingine wa tano utakaofanyika Septemba 16 katika kata mbili na majimbo matatu ya Monduli, Korogwe Vijijini na Ukonga.

Kati ya majimbo tisa, uchaguzi mdogo unafanyika kwenye majimbo matano kutokana na wabunge kuvihama vyama vyao hivyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa wabunge.

Waliohama vyama ni Lazaro Nyalandu aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), alijiunga na Chadema; huku Maulid Mtulia aliyekuwa CUF alihama na kujiunga na CCM ambako aligombea tena na kuibuka mshindi.

Aliyekuwa mbunge wa Siha, Godwin Mollel alihama kutoka Chadema na kujiunga na CCM. Aligombea tena jimbo hilo na kushinda.

Wabunge wengine waliovihama vyama vyao ni wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara aliyehamia CCM na aliyekuwa mbunge wa Monduli (Chadema), Julius Kalanga ambaye pia amejiunga na CCM.

Jimbo la Buyungu na Korogwe Vijijini uchaguzi unafanyika kutokana na waliokuwa wabunge kufariki dunia sawa na ilivyokuwa kwa Songea Mjini.

Jimbo la Longido uchaguzi ulifanyika baada ya ushindi wa Onesmo ole Nangole kutenguliwa na Mahakama Kuu.

Gharama za uchaguzi

Alipoulizwa na Mwananchi kuhusu gharama za uchaguzi mdogo, mkurugenzi wa Nec, Athuman Kihamia alisema hawezi kuzitaja kwa kuwa haziihusu tume pekee, bali pia Jeshi la Polisi na vyama vya siasa ambavyo kila kimoja hulipa mawakala wake.

Dk Kihamia alisema gharama za Nec zinategemea vitu vingi ikiwamo idadi ya vituo, umbali kutoka Dar es Salaam, idadi ya kata zinazoshiriki na jimbo, hivyo watazijua baada ya uchaguzi kwisha.

Hata hivyo, mtangulizi wake Ramadhani Kailima aliwahi kukaririwa na Mwananchi akisema kwa wastani, uchaguzi kwenye kata ni kati ya Sh20 milioni hadi Sh150 milioni kulingana na wingi wa watu kwenye eneo husika.

Kailima alisema uchaguzi mdogo wa Novemba 26, 2017 kwenye kata 43 ungegharimu Sh2.5 bilioni.

Kama kata zote zingefanana kwa ukubwa, idadi ya watu, miundombinu na sababu nyinginezo, kiasi hicho ni wastani wa Sh58 milioni kwa kila kata, ambazo kwa kata zote 86 zinazohusika na uchaguzi mdogo wa udiwani ni wastani wa Sh5 bilioni.

Kailima alisema idadi ya wapiga kura ndiyo inatoa bajeti ya mahitaji ya vifaa vya kuendeshea uchaguzi kama vile karatasi za kura na idadi ya vituo ambavyo vinakuwa na watumishi wasiopungua wanne.

“Kwa uchaguzi huu mdogo, bajeti ni Sh2.5 bilioni. Si kwamba kila kata itatumia gharama sawa na fedha hizi, bali kuna kata itatumia Sh20 milioni kutokana na idadi ya vituo vya kupigia kura kuwa vichache na kata yenye vituo vingi kwenye uchaguzi huu itatumia Sh150 milioni,” alisema Kailima wakati huo.

Mbali ya hilo, Desemba 2017 aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alisema ofisi yake iliokoa Sh156 bilioni ambazo zingetumika kwa ajili ya uchaguzi mdogo kama Serikali ingeshindwa na kurudia kufanya uchaguzi katika majimbo.

Katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa ofisi yake, Masaju alisema kiasi hicho kiliokolewa baada ya Serikali kushinda kesi 52 kati ya 53 zilizofunguliwa kupinga ushindi wa wabunge na kutaka uchaguzi urudiwe.

Ingawa inaweza isiwe moja kwa moja, lakini tafsiri ya kawaida gharama za uchaguzi kwa mujibu wa AG kwa jimbo moja ni Sh3 bilioni.

Kama majimbo yote yangekuwa yanafanana kwa idadi ya wapiga kura, miundombinu na mambo mengine, mwelekeo wa gharama zilizotajwa na Kailima na Masaju kwa wakati huo, hadi kufikia Septemba, Serikali inaweza kutumia Sh32 bilioni kwa ajili ya chaguzi ndogo.

Kati ya fedha hizo kwa makadirio Sh27 bilioni ni kwa ajili ya uchaguzi katika majimbo tisa na Sh5 bilioni kwenye kata 86, kama vigezo vyote vitafanana katika kata na majimbo yote. Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakisema kuwa utawala bora na demokrasia vina gharama zake na bajeti yake hivyo hilo si suala la ajabu.

Wasemavyo wadau

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kwa mara kadhaa amekuwa akieleza hamahama ya wabunge na madiwani wanaotoka upinzani kwenda CCM kuwa ni suala la utawala bora na si kweli kwamba kunaharibu bajeti nyingine.

“Pesa ya uongozi bora ipo, si kweli kwamba tunapofanya uchaguzi pesa ya elimu inapunguzwa, hapana. Ndiyo sababu Tume ya Uchaguzi ina bajeti yake ila tatizo linakuja hapa ikiwa upande wa CCM, ila wakifanya vyama vingine inaonekana ni sawa,” alisema Polepole alipohojiwa na kituo kimoja cha redio juzi.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu gharama za uchaguzi mdogo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Benson Bana alisema kuna haja ya kutafuta utaratibu mzuri utakaowawezesha watu kuhama vyama bila gharama zozote.

Dk Bana anapendekeza mtu aliyeshika nafasi ya pili kwenye Uchaguzi Mkuu ndiye atangazwe kuchukua nafasi ya kiongozi anayehama chama bila kujali chama chake.

Alisema hilo litapunguza gharama zisizo za msingi.

“Hili linahitaji mjadala mpana, lazima tukae na kuangalia namna bora ya kuwapata viongozi ambayo haitakuwa na gharama kubwa. Tunaweza kukubaliana aliyefuata kwa kura ndiye achukue nafasi iliyo wazi,” alisema Dk Bana.

Mwanazuoni huyo alisema suala hilo ni la Kikatiba, hivyo Rais John Magufuli na CCM waweke suala la mabadiliko ya Katiba kwenye Ilani kama moja ya ajenda ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akiwa na mtazamo kama huo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alipendekeza mshindi wa pili kwenye chama ambacho mbunge amefariki dunia, amejiuzulu au kuhama chama ndiye achukue nafasi yake.

Profesa Mpangala alisema ili kuondokana na chaguzi ndogo, sharti Katiba ibadilishwe na kuweka mfumo mwingine wa kuziba nafasi zilizo wazi badala ya kuruhusu kufanyika kwa uchaguzi mpya mara kwa mara.

“Zamani tulizoea kuona chaguzi ndogo zinafanyika baada ya mbunge au diwani kufariki dunia, siku hizi chaguzi ndogo zinatengenezwa, fedha nyingi za walipakodi zinatumika na hizo ni gharama za uchaguzi tu,” alisema.

Nyongeza na Ibrahim Yamola

Chanzo: mwananchi.co.tz