Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uchaguzi jimbo la Lissu mwendokasi

65852 Pic+lissu

Mon, 8 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/ Singida. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya uchaguzi wa ubunge wa Singida Mashariki ambayo inaonyesha kuwa kampeni katika jimbo hilo lenye kata 13 na vijiji 50 zitafanyika kwa siku 12 tu.

Siku hizo ni karibu ya nusu ya zile ambazo Tume hiyo ilizotoa kwa chaguzi zingine ndogo za ubunge zilizofanyika katika majimbo mbalimbali tangu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka 2015.

Katika chaguzi tatu zilizopita, NEC ilitoa siku 25 hadi 28 kwa wagombea kunadi sera zao kwa wananchi tofauti na jimbo hilo lililokuwa likiongozwa na Tundu Lissu. Katika uchaguzi uliokuwa ufanyike Mei 19 katika Jimbo la Arumeru Mashariki baada ya aliyekuwa mbunge wake kupitia Chadema, Joshua Nassari kupoteza sifa za ubunge, mchakato wa uchukuaji fomu, urejeshaji na kampeni ulikuwa ni siku 31.

Uchaguzi mdogo wa Ukerewe na Babati Mjini ulitumia siku 27 ambazo zilikuwa za kampeni na ukijiumulisha uchukuaji fomu na uteuzi, zilikuwa siku 34.

Pia katika uchaguzi mdogo wa Ukonga na Monduli, siku za kampeni zilikuwa 25, ukijumlisha siku za uchukuaji fomu na uteuzi zilizotolewa kuanzia Agosti 13 hadi 20 zilitimia siku 33.

Uchaguzi huo unafanyika kujaza nafasi ya Lissu ambaye Juni 28, Spika Job Ndugai alilitangazia Bunge hilo kuwa amepoteza sifa za kuwa mbunge akitoa sababu mbili.

Pia Soma

Sababu ya kwanza ni kutojaza fomu za mali na madeni za maadili kwa viongozi wa umma pamoja na kutokutoa taarifa kwake (spika) ya mahali aliko hivyo kumhesabu kama mbunge mtoro.

Jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema uchaguzi huo utafanyika Julai 31.

Alisema shughuli ya uchukuaji fomu za uteuzi wa wagombea itafanyika kati ya Julai 13 hadi 18. Uteuzi wa wagombea utafanyika Julai 18 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Julai 19 hadi 30.

Alisema ametoa ratiba hiyo kutokana na barua ya Spika Ndudai inayoeleza Lissu kupoteza sifa ya kuwa mbunge.

Jaji Kaijage alisema Spika Ndugai alizingatia matakwa ya kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343, kutoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wa uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki.

Akizungumzia uchaguzi huo, Katibu Mwenezi wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu alisema, “sisi tumetoa msimamo wetu kuhusu Lissu kuwa tumefadhaishwa na uamuzi wa spika na hatutashiriki uchaguzi huo.”

Kuhusu muda wa siku 12, Ado alisema Tume inataka kulikimbiza suala hili upesiupesi ilhali kuna michakato ya kisheria inayoendelea hasa ikizingatiwa kuwa Lissu yuko nje, “hatujajua kwa nini wamewahisha.”

Wakati Ado akisema muda ni mdogo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Juma Kilimba alisema wamejipanga kurejesha jimbo hilo huku akisisitiza kwamba uchaguzi huo hata ungefanyika kwa siku moja tu badala ya siku hizo zilizotangazwa na NEC, chama chake kingeshinda kwa kishindo.

Kuhusu uteuzi wa mgombea, Kilimba alisema chama kitafuata sheria na taratibu zake kumpata mtu sahihi wa kuipeperusha bendera ya CCM.

“Naomba nitumie fursa hii kutoa onyo kwa watakaowania kugombea Jimbo la Singida Mashariki kwamba yeyote atakayethubutu kwenda kinyume na sheria na taratibu za CCM, hatutaangalia uso, tutakata jina lake haraka,” Kilimba alisema alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi huo.

“Vitendo vya rushwa, hata harufu yake hatutaki kuisikia, wanaotarajia kugombe nafasi hiyo kwa usalama wao wajiepushe na vitendo vya rushwa au kuvunja sheria na taratibu za chama.”

Nyongeza na Gasper Andrew (Singida)

Chanzo: mwananchi.co.tz