Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Uamuzi wa mahakama na mgogoro mpya wa wadhamini CUF

44016 Pic+cuf Uamuzi wa mahakama na mgogoro mpya wa wadhamini CUF

Wed, 27 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ni wiki moja sasa tangu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilipotengua uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka kambi ya Mwenyekiti wake anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa; Profesa Ibrahim Lipumba.

Ingawa uamuzi huo ulitarajiwa kumaliza mvutano wa uhalali wa wajumbe wa bodi ya chama hicho, kati ya pande mbili zinazovutana, lakini ni dhahiri pande hizo zitarudi tena mahakamani kuomba iingilie kati kwani mvutano huo umeanza upya.

Uamuzi huo uliotokana na kesi namba 13 ya mwaka 2017, iliyofunguliwa na mbunge wa Malindi, Ally Salehe, kutoka kambi ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, dhidi ya Wakala wa Usajli, Udhamini na Ufilisi (Rita).

Saleh alikuwa akipinga wajumbe wa bodi walioidhinishwa na Rita kutoka kambi ya Profesa Lipumba kwa madai hawakuwa halali kwa kuwa hawakupatikana kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Hivyo alikuwa akiiomba mahakama hiyo itamke kuwa wajumbe waliokuwa wamependekezwa na kambi ya Maalim ndio halali.

Katika uamuzi wake Jaji Dk. Benhajj Masoud, Februari 18 mwaka huu, alitengua utezi wa wajumbe hao kutoka kambi ya Profesa Lipumba, akisema kuwa haukuzingatia Sheria ya Muunganiko wa Wadhamini.

Pia, alisema kwamba hata wale waliokuwa wamependekezwa na kambi ya Maalim Seif hawakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa bodi kwani nao hakuwa wamekidhi matakwa ya Sheria ya Muungano wa Wadhamini, kifungu cha 17.

Matakwa hayo ni kuwapo muhtasari wa kikao halali kilichopendekeza majina husika na kwamba kikao hicho ni lazima kiwe kimesimamiwa na mamlaka halali ya kiserikali.

Jaji Masoud alisema kuwa katika ushahidi wa pande zote hakuona muhtasari wa kikao cha kupendekeza majina hayo, ambao ungemwezesha kubaini kuwepo kwa kikao na uhalali wake na kwamba majina yaliyopendekezwa na makundi yote hayakustahili kuteuliwa.

Kauli na hatua zilizochukuliwa na viongozi wanaoongoza kambi hizo baada ya uamuzi huo, zinaonesha kuendelea kwa mvutano huo na kurudishana tena mahakamani kwa jambo hilo.

Kambi ya Maalim Seif iliuona uamuzi huo kama ushindi kwake na kuwa na matumaini ya kupata usajili wa wajumbe wapya wa bodi, hatua ambayo awali walikataliwa na Rita.

Maalim Seif aliwaeleza wanahabari kufurahishwa na uamuzi huo kwamba umekata mzizi wa fitina kuhusu madai yao dhidi ya Rita kuhusu bodi hiyo.

“Kwa ufupi Mahakama Kuu imetamka kuifuta rasmi bodi ‘feki’ ya Lipumba na kikundi chake na kuitanabaisha Rita kwamba ifanye kazi zake kwa kuzingatia sheria,” alisema Maalim Seif.

Kwa upande wake kambi ya Profesa Lipumba nayo iliutafsiri uamuzi huo wa mahakama kuwa iwapo wakirekebisha kasoro zilizoainishwa na mahakama ni dhahiri wajumbe wake watasajiliwa.

Siku hiyo hiyo ilianza harakati za uteuzi tena kwa kuzingatia uamuzi huo, ambapo ilipeleka barua ofisi ya Msajili ikimjulisha na kumwalika kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Taifa kesho yake kwa ajili ya uteuzi wa wajumbe wapya.

Hivyo kesho yake, Februari 19, siku moja baada ya uamuzi wa mahakama, kambi ya Profesa Lipumba ilifanya uteuzi wa wajumbe walewale waliotenguliwa lakini mara hii kikao cha utezi kikihudhuriwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza.

Februari 20, kambi ya Maalim Seif nayo iliitisha kikao cha Baraza Kuu lake la Taifa na kufanya uteuzi.

Katika kutimiza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, walimwalika Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), James Mbatia.

Huu pia unaweza kuwa utata mwingine kuhusu mamlaka ya kiserikali inayotajwa na sheria hiyo kama ni viongozi wa kisiasa au ofisa wa taasisi ya kiserikali, yenye dhamana na vyama vya siasa au usajili wa bodi. Siku hiyo hiyo kambi ya Maalim ilitangaza uteuzi huo kwa vyombo vya habari, huku ikieleza inaamini mara hii Rita itawasajili kwa kuwa wametimiza matakwa ya kisheria.

Profesa Lipumba licha ya kutangulia kufanya uteuzi lakini aliutangaza kwa vyombo vya habari siku mbili baadaye akitanguliwa na Maalim kwa siku moja.

Kambi zote tayari zimeshawasilisha Rita fomu zikiwa na majina ya walioteuliwa kuwa wajumbe wapya wa bodi, ili waweze kuidhinishwa. Ingawa kila upande unatamba kuwa majina iliyoyateua ndio yanayostahili kusajiliwa na Rita kuwa wajumbe wapya wa bodi ya chama hicho, huku wote wakirejea uamuzi wa Mahakama Kuu, lakini uamuzi huo, ukisomwa ndani ya mstari unaonyesha kuisafishia njia kambi ya Profesa Lipumba.

Kwanza, Jaji Masoud katika uamuzi wake hakusema amekubaliana na ushahidi kwamba wajumbe wa bodi waliokuwapo muda wao ulikuwa haujaisha na kwamba unaisha mwaka huu kama Maalim alivyowaeleza waandishi wa habari.

Ushahidi wa upande wa mwombaji (Saleh) ulikuwa na mkanganyiko ambao hauwezi kufumbiwa macho, akibainisha kuwa katika hati yake ya madai alidai muda wa wajumbe wa awali uliimalizika mwaka 2017. Wakati akitoa ushidi wake mahakamani alidai kuwa muda wa wajumbe hao unakwisha mwaka 2019 na kwamba majina yaliyopendekezwa yalikuwa ni kujaza baadhi ya nafasi zilizokuwa wazi.

Hata hivyo, akirejea vielelezo mbalimbali hususani fomu za maombi ya usajili kutoka kambi ya Maalim, barua ya Rita kwenda kwa Maalim na nyinginezo zinaonesha kuwa muda wa wajumbe wa awali ulikuwa umekwisha.

Akihitimisha hoja hiyo, Jaji Masoud alisisitiza kuwa kwa maana hiyo chama hicho kitakuwa hakina wajumbe wa bodi ya wadhamini lakini akasema hilo si lake bali linaihusu mamlaka husika.

Jaji Dk. Masoud alisema kuwa kwa mujibu wa barua ya Rita kwenda kwa Katibu Mkuu, Maalim Seif inatambua kuwepo kwa kambi hizo mbili na kwamba kambi moja ndio inayotambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Rita katika barua yake ya Juni 12, 2017 kwenda kwa Maalim Seif, inamjulisha kupokea majina kutoka makundi mawili ya chama kimoja (aliyoyawasilisha yeye Maalim na aliyoyawasilisha Kaimu Katibu Mkuu, Mgdalena Sakaya).

Ilieleza kuwa baada ya kupokea majina ya makundi mawili ilifanya mawasiliano na Ofisi ya Msajili wa Vyama ili kupata ufafanuzi, kwani kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Msajili ndiye anatambua viongozi halali wa vyama vya siasa.

Jaji Dk Masoud alisema kuwa mawasiliano baina ya Rita na Ofisi ya Msajili (kupata ufafanuzi wa viongozi halali wa chama hicho waliostahili kuwasilisha mapendekezo ya wajumbe wapya) ndicho kilikuwa kigezo cha usajili wajumbe wa kambi hiyo. Alisema hana tatizo na mawasiliano hayo na kwamba kwa mtazamo wake makusudio ya sheria katika kubaini wanaostahili kuwa wajumbe halali yanalenga wale walioko katika kitabu cha msajili na si walioko nje.



Chanzo: mwananchi.co.tz