Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UWANJA WA HOJA: Sakata la maalim Seif na kisa cha Mrema NCCR-Mageuzi

49641 SEIF+PI

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Habari ya mjini katika siasa kwa sasa Maalim Seif Sharif Hamad alivyoiacha CUF na kutimkia ACT-Wazalendo akiwa na wafuasi wake.

Katibu mkuu huyo aliamua kubwaga manyanga baada ya mahakama kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF, licha ya kujiuzulu nafasi hiyo na kuirejea mwaka mmoja baadaye.

Sakata hili lilisababisha upande wa Maalim Seif kufungua kesi zaidi 36 mahakamani, lakini ilipomalizika moja na Lipumba katambuliwa, Seif akaona hana lake. Hivi ndivyo ilitokea wakati wa Augustine Mrema alipohama NCCR-Mageuzi kwenda TLP mwishoni mwa miaka ya 1990.

Sakata la Mrema

Mrema aliyewahi kuwa waziri mambo ya ndani na baadaye waziri wa kazi, katika Serikali ya Ali Hassan Mwinyi, alipohamia NCCR-Mageuzi mapema 1995 alipishwa kwenye nafasi ya uenyekiti na Mabere Marando ambaye alichukua ukatibu mkuu wa chama.

Maada ya Uchaguzi Mkuu 1995 uliompatia kura milioni 1.8 lakini ushindi ukaenda kwa Mkapa aliyepata kura milioni 4.0 na baadaye 1996 akashinda ubunge wa Temeke kupitia uchaguzi mdogo, ndani ya chama uliibuka mgogoro wa uongozi kati ya kambi ya Marando aliyekuwa akiungwa mkono na wajumbe wengi wa kamati kuu dhidi ya Mrema aliyekuwa akiungwa mkono na wajumbe wengi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Aprili 1997 chama hicho kiliitisha mkutano wa NEC mkoani Tanga ili kujaribu kumaliza mgogoro huku kila upande ukivutia kwake.

Wakati Marando ameandaa mkutano wa kamati kuu kwenye ukumbi wa Hoteli ya Splendid, Mrema alikuwa ameandaa mkutano wa NEC kwenye hoteli ya Fourways kwa wakati uleule.

Juhudi za kina Marando kumwelewesha Mrema kwamba kikao kinachotakiwa kuanza ni kamati kuu, ziliekea kugonga mwamba. Marando na wajumbe wake walilazimika kumfuata Mrema Fourways alikokuwa akiwasubiri ili afungue mkutano wa NEC.

Kete ya Mrema ilikuwa ni wajumbe wa NEC akitaka kuwatumia kuwafukuza uongozi kina Marando.

Alipoanza tu hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano, kabla hata hajamalizia eneo la salamu, Naibu Katibu mkuu, Daniel Nsanzugwako aliyekuwa meza kuu alisika akisema, “Mrema unaua chama, Mrema unaua chama.”

Kauli hiyo ilipokewa na wengine, Anthony Komu na Marando waliopaza sauti wakimwambia Mrema ‘unaua chama’. Bila kujali Mrema aliamua kuendelea na hotuba lakini ilizuka tafrani nyingine ikiwamo wajumbe kusimama mbele yake na kufanikiwa kukatisha hotuba.

Marando alipata furasa ya kusema kwamba mkutano huo umekiuka taratibu kwa kuruka mkutano wa Kamati Kuu. Hivyo walikubaliana kwenda kwenye kamati kuu na wajumbe wa NEC walitakiwa kukutana tena hapo mchana.

Wajumbe wa kamati kuu wakiongozwa na Mrema, makamu mwenyekiti Haidary Maguto, katibu mkuu Marando walikwenda kwenye ukumbi wa Raskazone.

Katika mkutano huo ambao waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia, takriban wajumbe watano wa waliokuwa wakimuunga mkono Mrema walitoka mmojammoja, na kila aliyetoka aliita waandishi wa habari na kutangaza kujivua ujumbe wa kamati kuu.

Sababu za kujiuzulu kwao hazikutofautiana sana, kubwa waliona mkutano huo ulikuwa na nia ovu ya kumng’oa Mrema kwenye uongozi.

Haikupita muda, wajumbe wote wa mkutano ikaelezwa umeahirishwa hadi jioni, na kuwa mkutano wa halmashauri kuu ungefanyika siku iliyofuata.

Muda wa mkutano ulipofika, mmoja wa viongozi aliyekuwa upande wa Marando aliita waandishi na kusema hawangeruhusiwa kuingia kwa sababu zingeweza kutokea vurugu.

Hata hivyo waandishi walitaka kushuhudia namna itakavyokuwa na kumsihi awaruhusu kuingia. Kiongozi huyo aliruhusu lakini aliwataka wakae viti vya mbele jirani na meza kuu na ikitokea purukushani waende alikokuwa Marando kwa usalama wao.

Mkutano wa kamati kuu uliendelea kwa baadhi ya wajumbe kutoa shutuma dhidi ya Mrema huku yeye akiwa kimya. Ilipofika usiku kama saa nne aghafla taa zilizimwa, ukasikika mlio wa chupa, waandishi walianza kumtafuta Marando bila mafanikio kwa sababu ya giza, baadaye kila mmoja alitumia mbinu zake kujikoa.

“Zilisikika kelele “Mrema ameuawa” ... na nyingine “mjumbe amerushwa nje kupitia dirishani”. Baada ya hapo ndani ya ukumbi kulikuwa kimya kwa dakika kadhaa, Mara taa zikawashwa. Mrema alionekana chini ya meza na kofia yake ilikuwa imevaliwa na mlinzi wake.

Marando na Maguto walikuwa ukutani huku walinzi wao wakiwa wamewaziba kwa migongo. Mrema alikuwa wa mwanzo kutoka ukumbi na kupokewa nje na wafuasi wake. Marando alitolewa na mlinzi wake.

Siku iliyofuata asubuhi zikapatikana taarifa kuwa viongozi wote wa chama wameondoka Tanga kurejea Dar es Salaam. Mrema alifikia ofisi ya Manzese. Marando na timu yake walikwenda kuanzisha ofisini mtaa wa Lugoda na baadaye wakahamia eneo la Kisutu kwenye kontena, walikodai ndiko makao makuu ya chama.

Msajili wa vyama vya siasa kwa wakati huo, George Liundi alifanya juhudi za kuwapatanisha lakini juhudi zake ziligonga mwamba, aliendelea kutoa ruzuku kwa upande wa Marando.

Juhudi zingine za usuluhishi zilifanywa na Askofu Elinaza Sendoro wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Alikutana nao mara kadhaa lakini mazungumzo hayakuzaa matunda.

Baadaye Marando aliitisha mkutano wa NEC kwenye hoteli ya Bwawani, Zanzibar.

Mrema alihudhuria mkutano huo, lakini wakati wa hotuba yake ya ufunguzi alimshutumu Mapando kupandikiza wajumbe feki 14, pia akadai wajumbe halali 36 wamezuiwa kuhudhuria mkutano huo ili kumng’oa.

Baada ya hotuba hiyo, Mrema alitoka mkutano na wafuasi wake na kupanda boti na kurejea Dar es Salaam.

Timu ya Marando ilimteua Maguto kukaimu nafasi ya mwenyekiti na wajumbe 56 wakapiga kura ya kutokuwa na imani na Mrema na kuamua kumsimamisha uongozi kusubiri mkutano mkuu.

Mrema naye baada ya siku chache aliitisha mkutano mwingine wa NEC kuu Dar es Salaam na Marando na kumweka Prince Bagenda.

Malumbano hayo yaliishia kufunguliana kesi mahakamani. Marando alishinda na kurejeshwa madarakani. Hali hiyo ilimfanya Mrema na wafuasi wake wahamie Tanzania Labour Party (TLP), ambako alipishwa nafasi ya uenyekiti na Leo Lwekamwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz