Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UWAJIBIKAJI: Madiwani, DED wavurugana

Sat, 20 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Simanjiro. Mwenyekiti wa halmashauri ya Simanjiro mkoani Manyara, Jackson Sipitieck amevunja kikao cha baraza la madiwani, akisema hana imani na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Yefred Myenzi kwa madai ya kushindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo.

Hali hiyo imejitokeza juzi wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwenye kikao cha baraza hilo lililokutana katika mji mdogo wa Orkesumet.

Sipitieck alivunja kikao hicho bila ajenda nyingine kusomwa baada ya diwani wa kata ya Naisinyai, Kilemp Ole Kinoka kuwasilisha sababu tatu za kumkataa mkurugenzi huyo.

Ole Kinoka alitaja sababu hizo ni mkurugenzi huyo kutotekeleza maazimio ya baraza hilo, kutowapatia wajumbe makabrasha ya vikao kwa wakati na kutowaondoa wananchi wa Tilili waliovamia eneo lisiloruhusiwa.

Naye diwani wa kata ya Terrat, Jackson Ole Materi alidai wanashindwa kufanya kazi na mkurugenzi huyo, hivyo wanaomba Tamisemi imuhamishe na kuwaletea mkurugenzi mwingine.

Hata hivyo, Myenzi akizungumza na waandishi wa habari alisema upo muongozo ambao madiwani hao wangepaswa kuufuata kwani taratibu za kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mtumishi wa ngazi yake haupo katika mamlaka ya halmashauri.

“Mwenyekiti wa halmashauri anatakiwa kuwasilisha tuhuma hizo kwa mkuu wa wilaya ambayo halmashauri ipo na atamjulisha mkuu wa mkoa haraka iwezekanavyo,” alisema Myenzi.

Alisema mkuu wa mkoa atatafakari tuhuma hizo na halmashauri hairuhusiwi kuchukua hatua zozote za kinidhamu dhidi ya mtumishi yeyote.

“Pale itakapoonekana ni lazima kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mtumishi wa aina hii mamlaka yake ya nidhamu itafanya uchunguzi wa awali na kuendelea na taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa umma,” alisema Myenzi.

Baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo wamewaomba viongozi hao waache malumbano na badala yake washughulikie masuala ya maendeleo.

Mkazi wa mtaa wa Njiro mji mdogo wa Orkesumet, Elizabeth James alisema viongozi hao watashindwa kushughulikia masuala ya maendeleo kama watakuwa wakipambana wenyewe kwa wenyewe.

“Umebaki mwaka mmoja wa fedha kabla ya uchaguzi sasa badala ya kukumbatiana na kupambana kwa ajili ya maendeleo, viongozi wanashikana mashati,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz