KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewataka umoja wa vijana wa chama hicho kuacha tabia ya kuwa wapambe na badala yake wajikite katika kufanya kazi ya kujenga nchi kwa kujitolea.
"Kwa sasa vijana wengi wa umoja wa vijana wamekuwa wapambe namba moja wa wagombea na waangaikaji wa mambo binafsi ya viongozi na kuacha majukumu yao halisi," amesema Chongolo.
Amesema malengo ya kuanzisha umoja wa vijana haikuwa na maana ya kuwatumia vijana hao kwenye mambo ya kutafuta kura za wagombea bali ni kujenga nchi kwa kujitolea na baadaye kupata fursa ya kwenda kulitumikia Taifa.
Amesema miaka ya nyuma kazi ya umoja wa vijana ilikuwa ni kujiitolea kujenga miundombinu na kufanya mambo mengine ya maendeleo na baadae kupata fursa ya kwenda jeshini kulitumikia taifa kwa faida yao na nchi kwa ujumla.
“Miaka ya 2000 nyuma, asilimia tisini ya vijana ambao walikuwa wanachukuliwa kwenda jeshini walikuwa wanatokana na umoja wa vijana na ni kwa sababu walikuwa wanajitolea kulitumika taifa kwa kupitia umoja huo,” amesema Chongolo.
Katika hatua nyingine, Chongolo amewapongeza Umoja wa Vijana Wilaya ya Muleba kwa kujitolea kujenga vyumba vya madarsa katika shule ya Bukama Wilayani Muleba.
Chongolo amemtaka mwenyekiti wa halmashauri pamoja na viongozi wa Muleba kuendelea kuwatumia vijana hao katika kujenga miundombinu mingine.