Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UDASA yataka wagombea waache matusi

3470304cdc187ab830ea6dd219e208de UDASA yataka wagombea waache matusi

Mon, 21 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JUMUIYA ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) imewataka wagombea wa urais, ubunge na udiwani, waache ubinafsi na watumie muda wa kampeni kunadi sera badala ya matusi ili wananchi wawaamini.

Mwenyekiti wa UDASA, Dk George Kahangwa alitoa tamko hilo jijini Dar es Salaam jana. Aliwataka wagombea wawe wastaaratibu na waangulize maslahi ya Tanzania, badala ya maslahi yao na ya vyama vyao.

“Ni takribani mwezi mmoja sasa umepita tangu kampeni za uchaguzi zianze, na tulitoa tamko la awali tukitaka wagombea wote waheshimu na kufuata kanuni za uchaguzi na kufanya kampeni kistaarabu na kuvumiliana ili tufanye uchaguzi kwa amani, lakini tumeshuhudia kwa kipindi hiki mambo kadhaa yakiendelea katika kampeni, yanayotulazimu kutoa tamko jingine kwa kuwa tunawajibu kwa jamii,”alisema Dk Kahangwa.

Alisema wameona kuna wagombea wanaotanguliza ubinafsi na kutaka kupata madaraka kwa nguvu yoyote, hata iwe ya kuumiza watu wengine au kuhatarisha amani na usalama na kuwataka waache kufanya hivyo, wanadi sera za vyama ili wananchi wawaelewe.

“Wagombea watambue kwamba hawatapigiwa kura kwa uhodari wao wa lugha chafu na zisizo na staha, bali kwa kunadi na kueleweka kwa sera za vyama vyao. Awali tuliwaasa wagombea kufanya kampeni za kistaarabu, zenye lengo la kunadi sera zao, na sio lugha za matusi, na kejeli zenye viashiria vya kuchochea machafuko”alisema Dk Kahangwa.

Alisema kuna baadhi ya wagombea wanatumia lugha za matusi, kubezana na hata kutishia kwa namna moja au nyingine na kwamba kufanya hivyo hakuna tija kwa taifa.

Dk Kahangwa alisema wagombea wanapaswa kutambua kuwa wapiga kura hawatawapigia kura kwa uhodari wao wa lugha chafu na zisizo na staha, ila kwa kunadi na kueleweka kwa sera za vyama vyao.

Katika hatua nyingine, UDASA imesema ni kosa kisheria kwa wagombea kushawishi wafuasi wao kuiba vitambulisho vya kura vya wenza, ndugu, jamaa na marafiki iwapo wanashabikia vyama vingine tofauti na vyao na kusema jambo hilo halitakiwi kufumbiwa macho.

Kuhusu kufanya vurugu kwenye kampeni za wagombea wasio wagombea wa vyama vyao, UDASA wamewataka kuacha mara moja huku wakikumbusha kwamba mila na desturi za Tanzania ni upendo, umoja na mshikamano.

UDASA wamevisihi vyombo vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi, kuongeza nguvu katika kipindi cha kampeni na kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa weledi, usawa na haki.

Chanzo: habarileo.co.tz