Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCHOKOZI WA EDO: Namba Moja alipomsalimia Lema Taifa likashusha pumzi

50157 Pic+edo

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Juzi Namba Moja alikutana na Godbless Lema msibani. Jana magazeti yote yakaiweka picha yao mbele. Ni yule Lema ambaye alikaa jela miezi mingi akaikosa Krismasi fulani hivi. Unamkumbuka? Mbunge wa Arusha Mjini.

Namba Moja ndiye ambaye aliyemuita Lema. Hakukuwa na shida. Lema akaenda fasta wakaongea kidogo, wakapeana pole. Mambo yakapita. Dakika moja ilitumika kushusha pumzi nchi nzima. Walau wakati mwingine unapata wasaa ambao unajua kuwa Namba Moja na wapinzani wanaweza kuongea.

Tukifanikiwa kushusha pumzi kila siku inakuwa vyema. Tukifanikiwa kushusha pumzi kama hivi watu wa aina ya Pierre hawawezi kupata umaarufu kirahisi. Hali isipokuwa kama ile juzi Taifa linapatwa na presha. Kila siku kusikia wabunge wanatiwa ndani kunaweka pumzi juu. Kusikia kila siku wabunge wanaongea mabaya tu ya Namba Moja bila ya kuongea mazuri, Taifa linapandwa na presha.

Kila siku kusikia Namba Moja anafoka inaweka pumzi juu. Wananchi wanachanganyikiwa, na jinsi wanadamu walivyo, ukiwaweka karibu wanapunguza makali yao. ‘anko’ JK alikuwa anatumia mbinu hii. Hata hivyo, mwishowe Namba Moja anabakia kuwa Namba moja.

Sio lazima kugongana misibani. Wakati mwingine inaweza kuwa kikao cha dharura pale Magogoni. Namba Moja anaweza kukutana na wapinzani wake wakateta. Hatuhitaji kusikia wameteta nini. Kitu cha muhimu ni kwamba inashusha pumzi kwa Taifa.

Soma zaidi: UCHOKOZI WA EDO: Jumba la kifahari ni uthibitisho wa rushwa?

Nilichogundua ni kwamba licha ya yote yatokeayo Namba Moja anabakia kuwa Namba Moja. Watu wanaweza kupiga kelele kadri wanavyoweza lakini Namba Moja anachukua uamuzi anaoona ni sahihi na kufuata ilani yake. watu wa cheo chake waliopita huwa hawahukumiwi na muda uliopo. Wanahukumiwa pindi wakiondoka. Wakiwa madarakani hawazungumzwi vyema. Wakiondoka wanazungumzwa vyema.

Soma zaidi: UCHOKOZI WA EDO : Maalim Seif anaongezewa umaarufu kwa gharama nafuu

Tuwe na tabia ya kushusha pumzi kila mara. Raia wanajikuta katika mkanganyiko pindi kurasa za mbele za magazeti zinapokuwa na picha za mara kwa mara za wanasiasa wakirudishwa Segerea kutoka Mahakama ya Kisutu. Wanapenda picha za wanasiasa wanaopingana wanapopiga stori. Kama juzi. Taifa linashusha pumzi.

Taifa linapokaa katika presha ndio watu wanaanza kusambaziana video za Pierre. Mara video za Dokta Shika. Mara Mkuu wa Tabora naye anageuka staa mkubwa kama Mbwana Samatta. Ukali mwingi wa pande zote hausaidii sana ingawa mwishowe, sote hatuwezi kukubaliana kwa kila kitu.

Soma zaidi: UCHOKOZI WA EDO :Kuna sababu nyuma ya umaarufu wa Pierre



Chanzo: mwananchi.co.tz