Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCHAMBUZI: Miaka 42 ya CCM itikadi yake imebaki vitabuni

40335 PIC+CCM UCHAMBUZI: Miaka 42 ya CCM itikadi yake imebaki vitabuni

Wed, 6 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Novemba 2018 mkutano wa tisa wa makatibu wakuu wa vyama vya ukombozi Kusini mwa Afrika ulifanyika Windhoek, Namibia ambapo wajumbe walisisitiza umoja na mshikamano kwa watu wa Palestina na Sahara Magharibi ambao wako katika mapambano ya kutafuta uhuru na haki ya kujitawala.

Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho jana kimetimiza miaka 42 tangu kuasisiwa kwake Februari 5, 1977, kilihudhuria mkutano huo, kikiwakilishwa na Katibu wa itikadi na uenezi, Humphrey Polepole.

Vyama vingine vilivyoshiriki ni ANC (Afrika Kusini), Frelimo (Msumbiji), MPLA (Angola) ZANU-PF (Zimbabwe) na Swapo (Namibia).

Ilipofika wakati wa kupiga kura ya kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina na Sahara Magharibi, CCM haikupiga kura hiyo, kama ambavyo taarifa ya pamoja ya viongozi hao ilionyesha.

Hatua hii ya CCM, ambayo katiba yake inaitambulisha kama chama cha kijamaa, na chenye historia ndefu ya kuunga mkono harakati za ukombozi wa nchi mbalimbali ndani na nje ya Afrika, ilishangaza wengi hasa wale ambao wameifahamu muda mrefu.

Kwa wengine, hatua hiyo ilikuwa si kitu kipya bali uthibitisho wa kuzorota kwa itikadi ndani ya chama na serikali yake.

Miezi michache kabla ya mkutano huo, viongozi wa vyama hivyo walikutana Dar es Salaam chini ya mwavuli wa Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) kujadili changamoto za maendeleo na jinsi vyama hivyo vinaweza kushirikiana kuzitatua.

Katika mkutano huo, Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliwaambia washiriki kwamba vyama vingi vimeacha kufanya kazi kama “tanuri za maarifa na fikra za kimapinduzi” badala yake vimekuwa “mitambo ya kutafutia kura.”

Akiwa ndiyo kwanza amechukua nafasi hiyo ya ukatibu mkuu, Dk Bashiru alisisitiza dhamira ya chama chake ya “kuendeleza mageuzi ya kuwakomboa wanyonge kutoka kwenye dimbwi la unyonyaji na ukandamizaji.”

Oktoba 2016, Mfalme Mohammed VI wa Morocco alifanya ziara nchini na kupokewa na mwenyeji wake, Rais John Magufuli. Katika ziara hiyo, Mfalme Mohammed VI ambaye nchi yake inaikalia kwa maguvu Sahara ya Magharibi, alisaini mikataba 21 ya ushirikiano katika maeneo ya kisiasa, utalii, usafiri wa anga na maeneo mengine.

Baada ya ziara hiyo, wadau wa masuala ya diplomasia waliikosoa serikali kwa kuwasaliti wananchi Sahara ya Magharibi kwa kigezo cha maslahi ya kiuchumi.

Serikali ilifafanua ikisema ziara hiyo haikuhusiana na masuala ya kisiasa na wala haitobadilisha msimamo wa Tanzania katika uungaji wake mkono wa watu wa Sahara ya Magharibi.

Miaka miwili baadaye, ukweli wa ziara hiyo ulidhihiri baada ya CCM kutopiga kura ya kuimarisha mshikamano na watu wa Sahara ya Magharibi.

Mei mwaka jana, serikali ya CCM pia iliandika historia yake upya kwa kufungua ubalozi nchini Israel wa Tanzania kwa kile serikali ilidai ni utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kikanda, Dk Augustine Mahiga pia alihudhuria sherehe za ufunguzi wa ubalozi wa Marekani ambao nchi hiyo iliamua kuuhamisha kutoka mjini Tel Aviv kwenda Jerusalem, uamuzi ambao ulipingwa vikali na mataifa kadhaa na Umoja wa Mataifa (UN. Wakati kuna watu wanahusisha matukio haya na kudhoofu kwa itikadi na misingi ya kifalsafa ndani ya CCM, kada mkongwe wa chama hicho Pius Msekwa anaamini kwamba tofauti na maoni hayo, chama hicho kinazidi kuimarika lakini “mambo ya itikadi ni mambo ya kizamani”.

Spika huyo wa zamani wa Bunge anasema suala la itikadi halina nguvu tena na kwamba kilicho muhimu kwa sasa ni kuangalia ni kwa namna gani chama kinaimarisha nguvu katika kukabiliana na ushindani kutoka kwa vyama vya upinzani.

Anasema itikadi ya masikini ni kuondoa umasikini, ujinga na maradhi. “Itikadi hazina nafasi tena. Kinachotakiwa kutoa miongozo ni mipango na wala siyo itikadi.” Kuhusu suala la kusaidia ukombozi wa watu wanaojitafutia haki yao ya kujitawala, Msekwa anasema hayo yalikuwa ni mambo ya zamani na kwamba taifa haliwezi kuendelea kwa kuishi katika historia.

Akizungumzia kuhusu itikadi ya ujamaa ambayo CCM inajinasibisha nayo, Dk Hamad Salim wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anasema: “(Iko) katika maandiko lakini kivitendo hakuna, ujamaa wa mtu kupata mshahara milioni 40 huku mwingine anapata laki tatu? Ndio maana nasema, CCM na Serikali ilikwisha kuondoka huko.”

+255 716 874 501



Chanzo: mwananchi.co.tz