Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCHAMBUZI: Bunge letu lina vurugu? Katiba mpya ndiyo suluhisho

40338 Pic+bunmge UCHAMBUZI: Bunge letu lina vurugu? Katiba mpya ndiyo suluhisho

Wed, 6 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wabunge wa CCM na wanachama wa chama hiki kikongwe nchini wanafikiri Bunge letu limevurugika; kanuni zinakiukwa, hakuna nidhamu na wabunge wanajisemea hovyo. Wabunge hawa wamesikika wakiwatuhumu wenzao wa upinzani kwamba wana “utoto”. Tanzania tulizoea Bunge la chama kimoja. Na wakati mwingine ilikuwa ni vigumu kutofautisha bunge na mkutano wa chama.

Katika mfumo wa chama kimoja wabunge waliogopana, walioneana aibu, waliilinda serikali kwa vile ni ya chama chao na zaidi walilinda heshima ya chama chao. Na bahati mbaya au nzuri kwa wapenda mabadiliko, idadi kubwa ya wabunge wa upinzani ni vijana na si vijana tu, bali vijana makini ambao wakifikia hatua ya kupiga kura ya Ndiyo au Siyo si kwa maslahi ya vyama vyao bali kwa taifa letu.

Tatizo linalojitokeza na kupelekea picha ya vurugu bungeni, ni vijana wanaotaka mabadiliko ya kutanguliza maslahi ya taifa kwa upande mmoja na wabunge wengi wanaotaka kuulinda mfumo wa zamani wa kukitanguliza chama.

Haya ni makundi mawili yanayopambana bungeni na mtu wa kusimama katikati kuhakikisha makundi haya yanafanya kazi kwa pamoja kwa malengo ya kujenga taifa ni Spika.

Bahati mbaya kwa kundi la vijana wa upinzani, na bahati nzuri kwa kundi la CCM, lakini bahati mbaya kwa taifa letu; Spika anatoka CCM, chama chenye wabunge wengi, kinachounda serikali na kinachopambana kufa na kupona kulinda mfumo wa zamani.

Tatizo jingine ni pale wabunge wa CCM wanapofikiri kwamba wao ni bora na wana haki zaidi ya wabunge wa upinzani. Na mbaya zaidi hata spika anafikiri hivyo. Anafanya mambo yanayoonyesha anawapendelea wabunge wa chama tawala na mawaziri.

Vijana wa vyama vya upinzani wanapambana kuonyesha ukweli kwamba wote wana haki sawa. Pale bungeni, hakuna cha waziri wala waziri mkuu, wote ni wabunge na wana haki sawa.

Mapambano haya yanakumbana na nguvu kubwa za spika na nguvu kubwa ya wingi wa wabunge wa CCM; badala ya kuwa mapambano chanya yanaonekana kuwa ni vurugu.

Pamoja na kasoro zake za kibinadamu alizokuwa nazo Spika Samuel Sitta, aliweza kulijengea heshima Bunge la Tanzania. Alijitahidi kadiri alivyoweza kusimama katikati.

Kwa kosa hili kubwa la kushindwa kukipendelea chama chake bungeni, chama chake hakikukubali kumsimamisha tena kugombea nafasi hiyo. Hii sasa ni historia.

Hivyo, kinachotokea bungeni si vurugu bali ni ukomavu wa kisiasa. Sasa tunatambua kosa la Spika wa Bunge kutokana na chama cha siasa na hasa kama chama hicho kina wabunge wengi na kinaunda serikali.

Spika anakuwa sehemu ya serikali, badala ya kukiongoza chombo cha kuisahihisha na kuisimamia Serikali.

Itafika wakati wa kuifanya kazi ya kuandika Katiba mpya, hivyo ni lazima kuwa makini kwa nafasi nyeti ya uspika katika taifa letu.

Ni lazima Katiba mpya iweke wazi kwamba Spika asitokane na vyama vya siasa, Awe Mtanzania mwenye maadili bora, mwenye sifa, msomi na ameelimika, mzalendo na asiyefungamana na chama chochote cha siasa.



Chanzo: mwananchi.co.tz