Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

UCHAGUZI: Mgombea Chadema aswekwa ndani

82255 Pic+chadema UCHAGUZI: Mgombea Chadema aswekwa ndani

Wed, 30 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mikoani. Wakati watu wengine wanaowania uongozi wa serikali za mitaa Tanzania Bara walichukua na kurejesha fomu, zao kwa amani jana mgombea wa nafasi ya uenyekiti kutoka Kijiji cha Mwataga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, alijikuta akiishia mikononi mwa polisi baada ya kuchukua fomu.

Ilianza kama mchezo wa kuigiza baada ya Lucas Nyangindu anayewania uenyekiti wa kijiji hicho kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuamriwa kuwa yuko chini ya ulinzi na askari mgambo wa Kata ya Mwataga wilayani Kishapu kwa tuhuma ambazo hakuelezwa.

Pamoja na kuwekwa chini ya ulinzi na askari mgambo, Katibu wa Chadema mkoa wa Shinyanga, Zacharia Obadi aliiambia Mwananchi kuwa mgombea wao pia alipigwa na kunyang’anywa fomu alizopewa na msimamizi wa kituo.

“Amri ya mgambo kumwekwa mgombea wetu chini ya ulinzi ilitolewa na Afisa Tarafa ya Kishapu, Even Noah mara baada ya kukabidhiwa fomu na baadae mgambo hao walimshushia kipigo kabla ya kumnyang’anya fomu zake,” alidai Obadi.

Alisema baada ya muda mfupi, askari polisi walifika na kumtia mbaroni mgombea huyo ambaye hadi jana jioni alikuwa anaendelea kushikiliwa.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana, Ofisa Tarafa wa Kishapu, Even Noah alikiri kutoa amri ya mgombea huyo kutiwa mbaroni lakini akagoma kuzungumzia zaidi akidai siyo msemaji wa suala hilo.

“Kweli huyo ndugu (Lucas Nyangindu) amekamatwa, lakini siwezi kuongea zaidi kwa sasa maana mimi siyo msemaji,” alisema Noah.

Alipoelezwa kuwa yeye ndiye anayedaiwa kutoa amri ya kukamatwa na kupigwa kwa mgombea huyo, Ofisa tarafa huyo alihamaki na kusema “Nimesema niache tafadhali; mimi siyo msemaji wa suala hilo. Naomba uniache.”

Kauli za msimamizi, RPC

Akizungumzia tukio hilo, msimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa Wilaya ya Kishapu, Martine Ndamo alisema ofisi yake imepokea taarifa hizo na inaendelea kuzifuatilia huku akielezea kushangazwa na kitendo cha Ofisa Tarafa kuingilia masuala ya uchaguzi ambayo kikanuni hayamhusu.

“Binafsi nimeshtushwa na taarifa za kutokea vurugu katika kituo cha kutolea fomu kwa wagombea zinazodaiwa kuchochewa na amri ya ofisa tarafa ambaye kikanuni hana mamlaka katika masuala ya uchaguzi. Nafuatilia kujua chanzo chake,” alisema Ndamo.

Akizungumzia utoaji wa fomu, msimamizi huyo alisema ukiondoa kasoro ya vurugu zilizotokea kijiji cha Mwataga, maeneo mengine kazi hiyo ilifanyika kwa amani na utulivu kwa wagombea wote bila kujali itikadi zao kutendewa haki kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Richard Abwao alisema anafuatilia suala hilo na kuahidi kutoa taarifa baada ya kuwasiliana na maofisa wake wa Wilaya ya Kishapu.

Maeneo mengine

Katika maeneo mengine ya mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam, uchukuaji na urejeshaji wa fomu ulifanyika kwa amani na utulivu huku wagombea kupitia tiketi za vyama vya ACT-Wazalendo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chadema na Chama cha Wananchi (Cuf) wakionekana kujitokeza kwa wingi kulinganisha na vyama vingine.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi katika mitaa zaidi ya 10 ya Manispaa ya Ubungo, Kinondoni na Ilala jijini Dar es Salaam jana uligundua kuwepo kwa changamoto ya kukosekana kwa fomu namba nne ya tamko la maadili ambayo wagombea wanapaswa kujaza na kurejesha kukidhi sifa za kuwania nafasi za uongozi.

Changamoto hiyo ilibainika katika mitaa ya Mikocheni A na Mtaa wa Bonde la Mpunga Kata ya Msasani ambapo mgombea uenyekiti kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Seif Soud Seif alisema kukosekana kwa fomu hiyo kunawatia hofu ya kukosa sifa na kuenguliwa kugombea.

“Kila mgombea anatakiwa kupatiwa na kujaza fomu hiyo ya maadili; ucheleweshaji huu unaweza kuwa kikwazo na baadaye kutumika kama kigezo cha kutuengua kugombea,” alisema Seif aliyechaguliwa kuongoza mtaa wa Bonde la Mpunga mwaka 2014 kupitia tiketi ya Cuf.

Tatizo la kukosa fomu za tamko la maadili pia liliwakumba wagombea kupitia CCM kwa mujibu wa Katibu wa CCM tawi la Mikocheni A wilaya ya Kinondoni, Joseph Kauje aliyeiambia Mwananchi kuwa wagombea wa chama tawala nao hawakupewa fomu hizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, msimamizi msaidizi wa uchaguzi Mtaa wa Sokoine, Winfrida Mtaita na mwenzake wa Mtaa wa Kimanga, Lidya Bwathondi walisema uchukuaji wa fomu katika siku ya kwanza ulikwenda vizuri huku wagombea CCM na Chadema wakiwa wamejitokeza zaidi kulinganisha na vyama vingine.

Msimamizi akosa mgombea hadi saa 7:00

Wakati wagombea wakimiminika kuchukua na kurejesha fomu katika siku ya kwanza jana, hali ilikuwa tofauti katika mtaa wa Masaki ambapo hadi saa 7:00 mchana jana hakuna aliyejitokeza kuchukua fomu katika mtaa wa Masaki kama ilivyoelezwa na Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi mtaa huo Singo Mdegela.

Wagombea wa CCM pekee wajitokeza

Tofauti na mitaa mingine ambapo wagombea kutoka vyama mbalimbali walijitokeza, mtaa wa Mwangozo Manispaa ya Ubungo ulishuhudia wagombea kupitia CCM pekee wakijitokeza kuchukua fomu.

Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi wa mtaa wa Mwongozo, Abubakary Kumbwani alisema hadi saa 7:00 jana, fomu zilizotolewa zilichukuliwa na wagombea wa CCM huku akisema bado kuna fursa kwa wagombea wa vyama vingine kuchukua na kurejesha fomu hizo siku sita zilizosalia.

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo wa Novemba 24, 2019, uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania nafasi za ujumbe na uenyekiti wa mtaa, kijiji, kitongoji ulioanza jana utadumu hadi Novemba 4, mwaka huu.

Miongoni mwa maeneo ambako mwamko wa wagombea kuchukua fomu ulishuhudiwa ni pamoja na Soweto, Mawenzi na Kiusa ingawa juhudi za waandishi wa Mwananchi kupata takwimu ziligonga mwamba baada ya wasimamizi wasaidizi kukataa kuzungumzia suala hilo.

Akizungumzia siku ya kwanza ya kuchukua na kurejesha fomu, Msimamizi wa Uchaguzi Manispaa ya Moshi, Lain Kamendu alisema shughuli hiyo ilienda vizuri na hadi jana jioni hakupokea taarifa yoyote ya mkwamo.

CCM yatoa agizo maalum

Taarifa kutoka ndani ya CCM zilizothibitishwa na Katibu wa chama hicho mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya zinaeleza kuwa wagombea wote kupitia chama hicho tawala waliagizwa kuhakikisha wanachukua fomu jana bila kukosa.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mabihya alisema “Ni imani yetu kuwa agizo hilo (la wagombea wote kuchukua fomu jana) litafanikiwa.”

Jijini Mwanza, mwenyekiti wa mtaa wa Nchenga kata ya Nyegezi aliyemaliza muda wake, Paschal Joseph (CCM) jana alichukua fomu huku akielezea matumaini ya kutetea nafasi hiyo kutokana na jinsi alivyowatumikia wakazi wa mtaa huo.

Cuf na NCCR-Mageuzi wajipanga

Wakati wenzao wa CCM wakichukua fomu, Mkurugenzi wa Utawala wa Wilaya ya Nyamagana wa CUF, Edward Mboje alisema wagombea wao bado hawajaanza kuchukua fomu kutokana na maandalizi ndani ya chama kutokamilika.

“Tupo tunaendelea na mchakato ikiwemo kuwajazia wagombea taarifa zao muhimu kuepuka makosa katika ujazaji wa fomu watakazochukua,” alisema Mboje.

Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Katibu wa NCCR Mageuzi Mkoa wa Mwanza, Olela Mabula aliyesema “Tayari tunao wagombea mahiri tunaoamini watashinda uchaguzi; tunakamilisha taratibu muhimu za ndani ya chama kabla ya kuwaruhusu kuchukua fomu. Ninachoweza kusisitiza ni kuwa lazima tushiriki kwenye uchaguzi huu.”

CCM Dodoma mambo bado

Wakati wagombea wa CCM katika mikoa mengine wakichukua fomu kuanzia jana, hali ilikuwa tofauti katika baadhi ya wilaya za mkoa wa Dodoma ambapo shughuli hiyo haikufanikiwa kuanza jana kutokana na kutokamilika kwa uteuzi wa wagombea.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Godwin Nkanwa alitaja Wilaya ambazo wagombea wake walishindwa kuanza kuchukua fomu kuanzia jana ni pamoja na Dodoma Mjini, Bahi na Chamwino.

Mkoani Mbeya, wagombea kutoka vyama vya CCM na Chadema walijitokeza kuchukua fomu kuwania uongozi katika mitaa mbalimbali ya jiji la Mbeya huku wagombea Kissa Swilla (Chadema) na Edson Nshiro (CCM) wanaowania uenyekiti wa mtaa wa Ituha jijini humo wakitaja kwa nyakati tofauti utetezi wa haki na maendeleo kwa wote kuwa sababu za kuwania nafasi hiyo.

Msimamizi Msaidizi wa uchaguzi, Mtaa wa Ilomba Kata ya Ilomba, Furaha Malele alisema shughuli za kutoa fomu kwa wagombea iliyoanza jana saa 2:00 ilifanyika kwa amani na kwa kuzingatia sheria, kanuni na haki kwa wote.

Imeandikwa na Godfrey Kahango, Flora Temba, Sharon sauwa, Jesse Mikofu, Sada Amir, Suzy Butondo na Kelvin Matandiko.

Chanzo: mwananchi.co.tz