Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tundu Lissu: Maridhiano hayatuzuii kumkosoa Rais

Tundu Antipass Lissu DDW Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu

Sat, 4 Feb 2023 Chanzo: Mwananchi

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema maridhiano waliyoingia na CCM hayawazuii kumkosoa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake pale wanapokwenda tofauti na matakwa ya Katiba na sheria za nchi.

Lissu alieleza hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika nyumbani kwake Tegeta, Dar es Salaam hivi karibuni kuhusu masuala mbalimbali ya siasa za Tanzania na ujenzi wa demokrasia imara.

Mwanasiasa huyo alirejea nchini Januari 25 akitokea Ubelgiji ambako alikuwa akipata hifadhi ya kisiasa.

Aliondoka nchini mwaka 2020 baada ya Uchaguzi Mkuu akihofia usalama wake na familia yake.

Itakumbukwa kwamba katika uchaguzi huo, Lissu alikuwa mgombea urais kupitia Chadema na alishika nafasi ya pili baada ya Hayati John Magufuli ambaye alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 84 ya kura zilizopigwa huku Lissu akipata asilimia 13.

Kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyokuwepo wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tano, Rais Samia alianzisha mazungumzo na vyama vya siasa nchini huku chama chake kikiwa na mazungumzo na Chadema ambao walisusia mazungumzo ya pamoja.

Chama hicho kinaendelea na mazungumzo na CCM na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Januari 21 chama chake kitaendelea na mazungumzo hayo kwa sababu ni fursa ya kujadiliana mambo wanayoyataka.

Akizungumza na Mwananchi Lissu alisema mazungumzo ya maridhiano haiwazuii kumkosoa Rais na Serikali yake, lengo lao ni kutaka kuondokana na mambo ambayo wamekuwa wakiyalalamikia.

“Maridhiano haina maana kwamba tuzibwa mdomo kuisema Serikali inapokosea, tunapozungumza maridhiano tunataka tuondokane na giza la ukandamizaji, waache kukandamiza watu, waache kutesa watu, waache kufungua kesi za uongo, hayo ndiyo maridhiano,” alisema Lissu.

Alisema hamna mahali popote kwenye Katiba wala sheria za nchi panapoelekeza namna ya kumkosoa Rais kwa staha.

Alisema sheria inasema mtu ana haki ya kutoa maoni yake kwa namna yoyote ile ili mradi havunji sheria

“Ukiwa unajitambua kama raia, utajua kumkosoa kiongozi mkuu katika nchi, ukitaka kumkosoa unatakiwa kumkosoa vikali, usipalaze palaze. Unatakiwa umwambie hapa Rais umekosea na wewe Rais huna ruhusa ya kukosea,” alisema Lissu.

Mwanasiasa huyo aliongeza kwamba ukosoaji kwa Serikali au Rais umekuwa ukitafsiriwa kwamba ni uchochezi, jambo ambalo siyo kweli. Alisema anaamini ukosoaji unasaidia kuimarisha uwajibikaji wa Serikali.

“Dhana ya maridhiano ni kushirikiana na CCM kuhakikisha tunatatua haya matatizo, tushirikiane naye (Rais) na chama chake ili kuyatatua haya matatizo kwa njia za Amani kabla mambo hayajaharibika,” alisema Lissu.

Siasa za kujitambua

Akifafanua kuhusu wakosoaji kuitwa wachochezi, Lissu alisema siyo kosa la jinai kutaka kubadilisha Serikali kwa njia za kikatiba kupitia chaguzi

Alisema yeye kama raia anafanya siasa za kujitambua na kwamba watu wengi hawajitambui kwa sababu wanaamini kumsema Rais ni kosa, hivyo wanaogopa kumwambia ukweli kwa kumkosoa.

“Ukimwambia Rais wewe sio mfalme, wewe ni mtumishi umechaguliwa na wananchi, mamlaka yako ni limited (ina ukomo). Ukimwambia Rais huna mamlaka ya kuamuru watu wafukuzwe katika maeneo yao, huo siyo uchochezi, ni kujitambua na kutambua wajibu wako kama raia.

“Watu wasiokuwa raia, vibaraka ndiyo huwa hawana haki lakini mimi ni raia ninayejitambua. Miaka yote I am a citizen (mimi ni raia), cheo changu kikubwa kuliko vyote ni cheo cha raia. Kwa sababu ni raia, nitamsema yeyote anayetuletea za kuleta,” alisema.

“Watu wamezoeshwa kwamba kumsema Rais ni kosa...wakubwa huwa hawasemwi, Serikali huwa haisemwi, uchafu wake hausemwi hadharani. Tumikia kafiri upate mradi wako, funika kombe mwanaharamu apite. Hiyo ndiyo mentality (kasumba) ya Kitanzania.”

Hana kinyongo na mtu

Kufuatia tukio la kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017, Lissu amesema hana kinyongo na mtu katika kutekeleza kazi zake za kisiasa na hajutii chochote kwa yale yaliyomkuta wakati ule akiwa Dodoma.

Alisema akiwa majukwaani hamfikirii mtu bali anafikiria na kuzungumza aina ya siasa zinazofanyika hapa nchini chini ya viongozi huo huku akitaka kuona mabadiliko yakifanyika katika mfumo wa demokrasia.

“Sijawahi kujutia chochote katika maisha yangu ya kisiasa, kabisa, kwa sababu ninaamini katika mambo yangu yote niliyowahi kufanya katika siasa, sina hakika kama nimekosea kufanya hayo niliyoyafanya na yaliyonitokea kwa sababu ya kuyafanya hayo niliyoyafanya bila kukosea.

“Watu wanafikiri labda nina hasira sana na Magufuli, nina hasira na aina ya utawala ule, aina ya siasa hizo. Mimi ni mzima tunazungumza hapa, kuna wengi wamekufa kwa sababu ya aina hizo za siasa,” alisema Lissu.

“Huwa nashangaa nikiulizwa umewasamehe? Wala huwa siwafikirii hata Magufuli mwenyewe, huwa simfikirii. Simfikirii kwa maana hiyo alinifanya kitu mbaya, siyo hivyo, nafikiria aina ya utawala wake,” alisema.

Ahoji mgawanyo wa majimbo

Lissu alisema Tume ya Uchaguzi ina kazi kubwa ya kutengeneza upya majimbo ya uchaguzi kwa sababu kuna majimbo ambayo hayana sifa za kuwa majimbo ya uchaguzi kwa sababu yana idadi ndogo ya watu.

Alitolea mfano Jimbo la Temeke lina wapigakura takribani 478,000 kwa takwimu za mwaka 2020, lakini Zanzibar yote yenye wapigakura 566,000, ina majimbo 50. Alisema jambo hilo siyo sahihi kwa sababu kigezo kikubwa cha kupanga majimbo.

“Katiba hii haisemi popote Zanzibar iwe na wabunge wangapi. Katiba ya kwanza ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1965 ilitamka wazi Zanzibar iwe na wabunge wangapi, hii haisemi chochote.

“Wabunge wako 50, wapigakura wenyewe wako 566,000 kwa takwimu za mwaka 2020. Kura ya Mzanzibari mmoja ni sawa na ya Watanganyika nane au tisa, ni sawa hiyo? Na mbunge mmoja anyechaguliwa na watu 7,000, ana hadhi sawa na mbunge wa jimbo lenye watu 100,000,” alihoji Lissu.

Chanzo: Mwananchi