Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tuna fedha nyingi kutekeleza Ilani

Magufuli111 Tuna fedha nyingi kutekeleza Ilani

Wed, 30 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli amesema serikali ina fedha nyingi za kufanya mambo makubwa ya maendeleo ambazo awali zilikaliwa na mafi sadi, lakini waliwabana na sasa zitakwenda kuwahudumia wananchi wakipata ridhaa ya kuongoza nchi kwa kipindi kingine.

Aidha, Magufuli amesema katika kipindi cha miaka mitano kilichopita, Serikali ya CCM iliamua kujenga miundombinu imara ya afya ikiwamo kujenga vituo vya afya nchi nzima na kuongeza upatikanaji wa dawa, wahudumu wa afya na vifaa tiba ili awamu hii ihakikishe kila Mtanzania anapatiwa bima ya afya.

Kutokana na hayo, alieleza sababu kuu mbili zilizomrejesha kuomba ridhaa ya kuongoza tena kwa kipindi cha miaka mitano, ikiwamo namna walivyotekeleza vizuri ahadi katika awamu zilizopita na malengo ya kuifanya Tanzania kuwa kama Ulaya kwa maendeleo.

Akizungumza na wananchi mkoani Njombe akiwa njiani kwenda mkoani Mbeya jana, Rais Magufuli alisema kwa miaka mitano Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa ya kuwabana mafisadi waliokuwa wamekalia fedha za Watanzania, lakini sasa fedha zipo za kufanya mambo makubwa ya maendeleo.

“Fedha zipo hapa hapa za kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, zamani zilikaliwa na mafisadi, tumewabana sasa zinakwenda kuhudumia wananchi,” alisema Rais Magufuli.

Alitumia kampeni hizo kuwaombea kura wagombea wa CCM kwa ngazi ya udiwani na ubunge, ambapo wana CCM wa Njombe kupitia Mwenyekiti wa Mkoa, Jasel Mwamwala waliipongeza CCM na Rais Magufuli kuweka kwenye ilani miradi mikubwa ya Liganga na Mchuchuma ambayo ndio tegemeo la uchumi kwao.

Alisema sababu mbili alizozitaja zinazobeba mafanikio makubwa kwa miaka mitano ya uongozi wake na namna walivyojipanga kuleta mapinduzi ya kiuchumi, ndizo zimemsukuma kuona bado anahitaji kujitoa sadaka kwa Watanzania ili awatumikie na kuifikisha nchi kuwa kama Ulaya kupitia miradi mikubwa ikiwamo Mchuchuma na Liganga.

Kuhusu bima ya afya kwa kila Mtanzania, alisema nguvu kubwa kwa miaka mitano iliwekwa katika kujenga miundombinu ikiwamo vituo vya afya, zahanati, hospitali za mikoa na rufaa, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, wahudumu na kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali itahakikisha kila Mtanzania anapata bima ya afya.

“Tumejipanga kutekeleza utatatibu mzuri kwa Watanzania wote kupata bima ya afya. Tulianza kujenga vituo vya afya 487 nchi nzima, dispensary 1,198, hospitali 10 za mikoa, rufaa ikiwamo ya Njombe,” alisema.

“Tuliongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 hadi shilingi bilioni 270 sasa, tukaimarisha ugawaji wa dawa kupitia MSD (Bohari ya Dawa) na magari ya kusambaza dawa, huduma za vipimo ambapo mashine za X-Ray zimenunuliwa.

Ukishaziimarisha hizi huduma ndio bima ya afya zinakuja, huwezi kupeleka bima ya afya wakati huna hospitali” alisema. Akitolea mifano ya miradi iliyotekelezwa mkoani Njombe, Magufuli alisema, “Ninyi mnafahamu tulipotoka, tulipo na tunapotaka kuelekea.

Mnakumbuka miaka mitano iliyopita mambo mengi tumetekeleza ila machache tu bado.” Alisema serikali imetekeleza miradi ya barabara mkoani humo kwa gharama ya Sh bilioni 498.76 ikiwamo ya Lusitu-Mawengi yenye urefu wa kilometa 50 na Mafinga –Igawa yenye urefu wa kilometa 64.6.

“Hii miradi imerahisisha huduma na safari katika maeneo ya mkoa huu. Tumejenga soko na stendi ya kisasa katika makao makuu ya Njombe, mkoa ni mpya ila mmetangulia mikoa mingine.

Wana Makambako na Njombe tumeleta Sh bilioni 41.1 kuimarisha huduma za afya,” alieleza.

Chanzo: habarileo.co.tz