Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tume huru, Katiba Mpya mnyukano

Katibapicc Data Tume huru, Katiba Mpya mnyukano

Tue, 28 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Ni malumbano ya hoja. Ndivyo unavyoweza kuelezea mjadala unaoendelea baina ya wasomi, wanasiasa na viongozi wa dini kuhusu nini kitangulie kati ya kuandika Katiba Mpya na Tume huru ya uchaguzi.

mjadala huo, lipo kundi la wanasiasa likiongozwa na Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe linalotaka Taifa liende na mambo machache likiwamo hilo la Tume huru kwamba badala ya kuifumua Katiba na kuiandika upya.

Hata hivyo, hoja hiyo inapingwa na wanasiasa wenzake, viongozi wa dini, wanasheria nawasomi akiwemo Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia anayesema kuanza na upatikanaji wa Tume huru badala ya Katiba Mpya “ni sawa na mtoto kumzaa mama”.

Mbatia anaungwa mkono na mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), mkoa Kilimanjaro, David Shillatu akisema kuwa “hoja ya kurekebisha kwanza Tume ya uchaguzi ndani ya Katiba ya sasa, ni sawa na kutanguliza mkokoteni mbele ya punda.

Mchakato wa Katiba Mpya ulioanza mwaka 2011 ulikwama baada ya Bunge la Maalumu Katiba kupitisha Katiba Inayopendekezwa mwaka 2014, ambayo hata hivyo inapingwa na baadhi ya wanasiasa na wasomi kuwa haikuzingatia maoni mengi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Inaelezwa kuwa kutokana na wingi wa wajumbe waliotokana na chama kimoja ndani ya Bunge hilo, kulisababisha rasimu ya Jaji Warioba iliyokuwa imebeba maoni ya wananchi, kufumuliwa na baadhi ya vipengele kuondolewa kwa masilahi ya watu wachache.

Advertisement CCM iliingiza suala la kukamilisha mchakato huo kwenye ilani yake ya 2015-2020, lakini ilibadili gia angani na kueleza mchakato huo si kipaumbele, na katika Ilani ya 2020-2025 halikugusiwa kabisa.

Juni mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alirithi mikoba ya hayati Magufuli, aliwaomba Watanzania kumpa muda wa kushughulikia kukuza uchumi ndipo baadaye ataangalia mengine likiwemo la Katiba.

Hii imesababisha baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani, wanaharakati, wanasiasa na viongozi wa dini kupaza sauti wakitaka mchakato wa kuandika Katiba Mpya ufike mwisho wengine wakitaka uanzie rasimu ya Jaji Warioba.

Takribani wiki moja iliyopita, wadau wa vyama vya siasa walikutana Jijini Dodoma katika mkutano uliofunguliwa na Rais Samia na walitoka na maazimio 80, likiwamo la kuchukua mambo machache ya kuanza nayo likiwemo la Tume Huru.

Sambamba na hilo, wanaharakati wa haki za binadamu nao wametangaza mkakati wa kukusanya saini milioni tano za watu wanaounga mkono mabadiliko ya Katiba na kuyapeleka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mnyukano wa Zitto, wakili Jebra

Katika mitandao wa Twitter hoja ya kipi kianze kati ya Tume Huru ya Uchaguzi au Katiba mpya imeshika kasi baada ya kuibuliwa na Zitto.

Desemba 25, Zitto katika ukurasa wake wa Twitter aliandika “Tume Huru ya uchaguzi itakupa Bunge ambalo lina uwakilishi wa watu ili waweze kuleta Katiba Mpya ya watu.”

“Kutaka Katiba Mpya na Bunge hili lenye wabunge asilimia 97 wa CCM) ni sawa na kufunga safari ya kwenda Sumbawanga kutokea Dar es Salaam kwa kupanda boti ya Azam Marine (hakuna usafiri wa maji Dar-Shinyanga)” alisisitiza Zitto.

“Tunataka kutoka kwenye kutegemea utashi. Tume huru iajiri wasimamizi wake wa uchaguzi na si kutegemea ma- Ded (wakurugenzi wa halmashauri na majiji) ambao ni makada. Katiba Mpya ni lazima. Usipokuwa na Tume huru hiyo katiba tutakuwa tunadanganyana tu,” alisema.

Hoja hiyo imejibiwa na wakili Jebra Kambole akisema “uchaguzi ni mfumo sio tume. Tume haiwezi kuwa huru bila kurekebisha mfumo mzima. Ni sawa na gari lenye pancha matairi yote ukaamua kuziba moja (tairi) ili ufike Kigoma.”

Wakili Kambole akaongeza, “Tume huru ya uchaguzi bila Katiba Mpya ni sawa na kuziba mashimo ya panya kwa mkate! Maana Tanzania uchaguzi ni mfumo sio Tume. Nguvu ya Rais na wateule wake, polisi, Tume, Tamisemi na wengineo lazima viangaliwe kwa pamoja.”

Wankyo Nethya akaandika “Tanzania haiwezi kupata Tume huru yenye mamlaka ya kuendesha michakato ya uchaguzi bila kuingiliwa na Rais ambaye ni mgombea na taasisi nyingine za kiserikali kwa Katiba ya 1977.”

Mjadala nje ya Twitter

Akifafanua hoja yake, Shillatu alisema kwa sasa kama nchi, hakuna uchaguzi hivyo kuwepo umuhimu wa kuandika Katiba mpya kwanza kwa kuwa hii ya sasa inaonekana kukosa uhalali miongoni mwa wengi.

“Ni maoni yangu kuwa kurekebisha kwanza Tume huru ndani ya Katiba ya sasa (ya 1977) ni sawa kabisa na kutanguliza mkokoteni mbele ya punda na wewe kuamini kwamba punda atavuta ule mkokoteni. Haiwezekani,” alisema.

“Kwa kuwa rasimu ya pili ya Jaji Warioba ipo, naamini Watanzania wengi wanaamini tunaweza kujenga kuanzia hapo. Jitihada zozote za kuzuia maoni ya watu yasitokee kwenye Katiba wanayoitaka wao utakuwa ni uhaini,” alisisitiza.

“Twende na Katiba Mpya ambao ndio mkataba wa watawala na watawaliwa badala ya kung’ang’ania Tume huru ambayo ni kijisehemu kidogo cha Katiba,” alisisitiza.

Rwezaura Kaijage, Mhadhiri katika Kitivo cha sheria cha Chuo Kikuu Ruaha (Rucu), alisema muhimu ni kuifumua Katiba ya sasa na kubadili mifumo kwa kuwashirikisha wananchi wanataka nini na sio viongozi wanataka nini.

“Katiba ndiyo sheria mama. Yaani utacheza kote namba tano katikati lazima uikute Katiba. Ukipata Tume ya uchaguzi ambayo itasemekana ni huru kama Katiba haiilindi itakuwa ni kazi bure. Ili tuweze kwenda ni lazima tufumue Katiba,” alisema.

Hoja hizo zimeungwa mkono na Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), aliyesema Tanzania kuna utitiri wa kinga za watawala wenye nguvu kuliko Tume huru, hivyo Katiba ndio msingi wa yote.

“Hivi sasa tuna Bunge lenye wabunge wasio na chama. Maamuzi yake ni batili. Nani atapitisha muswada wa Tume huru?” alihoji Bagonza na kudai licha ya Zanzibar kuwa na Tume huru, lakini bado kuna nyakati uchaguzi ulivurugwa.

“Zanzibar kuna Tume Huru lakini haikumzuia Jecha (mwenyekiti wa Tume) kuvuruga uchaguzi na Rais Karume (Aman Abeid Karume-mstaafu) juzi alikiri uchaguzi wa 2020 ulikuwa na kasoro nyingi,” alisema Askofu Bagonza.

Wanasiasa watofautiana

Akijenga hoja, Mbatia alisema wanaochagiza Watanzania waanze na Tume huru wanakosea na yuko tayari kutetea msimamo huo.

“Kwa analysis (uchambuzi) kinachopaswa kuanza ni Katiba ambao ni utaratibu wa kuweka mifumo imara yenye kulinda utu wa wanadamu. What is (ni kitu gani) Tume huru? Tume Huru inapewa maelekezo yote na Katiba,” alisema .

“Kwa Katiba hii iliyopo ambayo ni ya chama kimoja. Katiba ndio uhai wa taifa lolote, katiba ni kila kitu. Kwa hiyo wanaosema eti Tume Huru ndio ianze wanakosea. Niko tayari kwenda kwenye mdahalo popote pale.

Hata hivyo, Renatus Muabhi, katibu mkuu wa CCK, alisema Tume huru ni muhimu kwa sababu ndiyo msingi wa mfumo wa kujenga viongozi wa kisiasa kupitia uchaguzi na kushika madaraka.

“Kwa hiyo kutokana na ubovu wa Tume isiyokuwa huru kunasababisha madhara makubwa matatu ambayo ni kupata viongozi ambao hawakuchaguliwa na wananchi na kupata Serikali isiyo na ridhaa ya wapiga kura na tatu kuleta matatizo au vurugu za kisiasa na pengine uvunjifu wa amani,” alisema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz