Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tulia awashangaa wanaojipitisha jimboni kwake

Tulia Atoa Ushauri Ugawaji Wa Magari Ya Wagonjwa Tulia awashangaa wanaojipitisha jimboni kwake

Thu, 13 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameeleza kushangazwa na watu walioanza kujipanga kuwania ubunge katika jimbo lake la Mbeya Mjini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 huku akisema ni mapema kufanya hivyo.

Akizungumza leo Julai 12, 2023 wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu ya vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule ya msingi Iwambi jijini hapa, Dk Tulia amesema atakanyaga watakapokanyaga wao.

“Kuna watu wanapita huko kujipanga kugombea ubunge jimbo la Mbeya mjini, kwa kweli ni mapema mno kwani walipigwa mchana kweupe kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, nawakaribisha, Mbeya iko salama na Tanzania iko salama,” amesema.

Ameongeza: “Mimi niko salama, kama wanakuja karibuni. Mbeya iko salama, Rais Samia Suluhu Hassan yuko Salama, Tanzania na Taifa liko salama watakapo kanyaga tutakanyaga hadi kieleweke.”

Dk Tulia amesema kuna kundi la watu ambao wana kazi ya kuvuta wengine mashati, amewataka wananchi wasikubali Tanzania haiko tayari kuwepo kwa ubaguzi na mgawanyiko.

“Msikubali wala kuwasikiliza wabaguzi wanaotaka kuwagawanya kwa kuwakatisha tamaa hususan katika mradi wa uwekezaji wa bandari mnapaswa kutambua nchi iko salama na mimi kama Spika wa Bunge na Rais Samia tuko salama katika kuwatumikia Watanzania,” amesema.

Katika hatua nyingine, Spika Tulia amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo ikiwepo sekta ya elimu kwa kuhakikisha hakuna uhaba wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na madawati na hakuna mtoto atakayekaa chini.

“Katika shule hii ya msingi Iwambi, Serikali imetoa zaidi ya Sh100 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na ofisi ya walimu kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), nami kama mbunge nachangia Sh2 milioni na mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya uboreshwaji miundombinu ya vyumba vya madarasa,” amesema.

Kwa upande wake, meya wa jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema uwepo wa Dk Tulia mkoa umepokea miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa barabara njia nne ambayo inakwenda kufungua fursa za kiuchumi na kubadili taswira ya mkoa.

“Tunajivunia uwepo wako kwani kazi nyingi unazifanya kuisaidia Serikali ikiwepo halmashauri kupokea miradi mbalimbali ya kimkakati hususan Sh1.5 bilioni za boost kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya za msingi,” amesema.

Mkurugenzi jiji la Mbeya, John Nchimbi amesema uwepo wa miradi kupitia TEA ni mkombozi mkubwa katika sekta ya elimu na kuwataka walimu kutunza miundombinu ya vyumba vya madarasa iliyojengwa kupitia mradi huo.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Iwambi, Elia Kasanga amesema mradi huo utapunguza changamoto ya mlundikano wa wanafunzi kwenye vyumba vya madarasa licha ya kuwepo kwa upungufu wa vyumba vya madarasa.

Ametaja changamoto nyingine ni pamoja na uhaba wa nyumba wa walimu zilizopo tatu upungufu 39 upungufu vyumba vya madarasa 20 vilivyopo 22.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live