Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tulia atangaza kiaina ubunge 2020

11480 Tulia+pic TanzaniaWeb

Tue, 17 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ametangaza kiaina kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 atagombea ubunge, licha ya kutoweka wazi jimbo atakalowania.

Mbunge huyo wa kuteuliwa alitoa kauli hiyo jana mjini hapa baada ya kuulizwa swali na waandishi wa habari, iwapo atagombea ubunge katika uchaguzi huo.

Siku za hivi karibuni, Dk Tulia ameonekana akishiriki shughuli mbalimbali za kijamii jijini Mbeya, ikiwamo kuandaa mashindano ya mbio ya Mbeya Tulia Marathon.

“Kuna swali limeulizwa hapa kuwa kwa juhudi zinazoendelea ni vyema nikawauma sikio kwamba nitagombea wapi? Aaah, lakini kwa vile nyie (watu) ni watu wa Mbeya lazima mtakuwa wa kwanza kujua nitagombea wapi,” alisema Dk Tulia na kuongeza:

“Ila ambalo ni la uhakika ni kwamba nitagombea, kwa hili linapunguza maswali ya zamani maana zamani nilikuwa sina hakika nitagombea au sitagombea.”

Alisema atagombea ubunge ila kuhusu jimbo atakalogombea kwa sasa hana jibu la moja kwa moja.

“Bado kidogo kwa sababu nafasi inayoweza kugombea ni ya ubunge na ubunge ni uwakilishi wa wananchi lazima uangalie hiyo sehemu wanahitaji mwakilishi mwingine au hapana, au wapo sawa na huyo aliyepo,” alisema.

Alisema unapotaka kugombea lazima upime kwa sababu ni nafasi ambayo wananchi ndiyo wanakutuma kuwawakilisha.

“Kwa hiyo sio suala jepesi kwamba wewe unajichagulia unakwenda wapi. Pia, kuangalia wapi watu wanahitaji mwakilishi, lakini siyo wanahitaji mwakilishi ila wanahitaji wewe ndiyo ukawe mwakilishi,” alisema na kuongeza:

“Kwa hiyo hilo ni jambo ambalo litachukua muda kidogo, lakini mimi ni mbunge wa CCM, chama chetu kina utaratibu wake wa namna ya kuwapata wagombea.”

Alisema kimsingi jambo hilo ni la kuzingatia zaidi na kwamba lazima utaratibu huo ufuatwe.

Chanzo: mwananchi.co.tz