Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tulia asisistiza ushirikiano wa watu wa dini zote

2b563a890bf08c1cc498a36c070966b2.png Tulia asisistiza ushirikiano wa watu wa dini zote

Sun, 17 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MBUNGE wa Mbeya mjini Dk Tulia Ackson amesisitiza wakazi jijini hapa kuendelea kushirikiana pasipo kujali tofauti zao za imani za kidini na kuwa mshikamano utawezesha kupiga hatua ya kimaendeleo kwa kasi.

Alisema ushirikiano wa waumini wa dini zote wakati wa shida na raha kwa wakazi unatakiwa pia katika shughuli za kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba za ibada kama makanisa na misikiti.

Dk Tulia ambaye pia Naibu Spika aliyasema hayo alipokuwa akifanya harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti mpya wa Qadiriyya Uyole uliopo katika kata ya Itezi jijini Mbeya shughuli iliyohudhuriwa na waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini za kiislamu na kikristo waishio jirani.

“Sisi tunaamini shughuli ya ujenzi wa msikiti huu inakwenda kukamilika hivi karibuni kwa michango hii ambayo imechangwa na iliyoahidiwa siku ya leo.Tumezungumza na wadau mbalimbali na tunaendelea kuzungumza nao kwa sababu msikiti huu unahitaji kama milioni 390 ili uweze kukamilika kabisa.

“Tumekuwa watu wa kushirikiana na kushikamana katika mambo mengi, hatubaguani na ushirikiano huu unapaswa kuwa endelevu inawapo tunahitaji kupiga hatua ya kimaendeleo kwa haraka. Kama wanavyofanya waislamu katika ujenzi huu ikitokea na wakristo mna jambo lenu washirikisheni wenzenu kwa kuwa lengo letu ni moja yaani kuyafikia mafanikio,” alisisitiza.

Katika harambe hiyo ambayo Dk Tulia aliiendesha kwa namna ya wadau waliohudhuria kuchangia kwa kupiga picha naye kwa kulipia kiasi cha Sh 600,000 zilitolewa ahadi Sh milioni 1.3 sambamba na mifuko ya saruji 64 na tofali za kutosheleza ujenzi wote wa jengo hilo.

Mchango wa Dk Tulia aliukabidhi baada ya harambee ulikuwa wenye thamani ya Sh 4,000,000 ukilenga kukamilisha sehemu ya ujenzi wa jengo ambalo ni nguzo za kati pia alikabidhi vifaa ikiwa ni pamoja na nondo, mbao, kokoto, mchanga, saruji mifuko 60,misumari na milunda.

Akizungumza kwenye harambee hiyo, Meya wa jiji la Mbeya, Shekhe Dulu Issa Mohamed alisema ushirikiano katika shughuli za kimaendeleo baina ya wakriso na waislamu ni muhimu huku akisisitiza kuwa kinachohubiriwa na dini zote ni upendo na mshikamano na hakuna dini inayohubiri chuki.

“Kilichopo ni kuwa kila mmoja anaona njia inayomfaa kuipita kufikia ufalme wa mbingu.Wote mnakwenda Chunya mwingine anapita njia ya Mbalizi na mwingine anapita ya mkato lakini mnakokwenda ni kumoja hivyo hata makanisa na misikiti waumini wake hawapaswi kutengana bali kushirikiana kwa umoja,” alisisitiza Meya huyo.

Diwani wa kata ya Itezi,Sambwee Shitambala alisema ujenzi wa msikiti huo ni alama kubwa kwa kuwa ndiyo utakuwa msikiti pekee katika eneo lote la bonde la Uyole hivyo ni muhimu kwa wadau kuchangia ili ukamilike kwa wakati.

Akitopa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Katibu wa Kamati ya Ujenzi Mwalimu Rashid Tindwa alisema ujenzi umesuasua kwa miaka nane sasa lakini kwa msukumo unaoonekana kutoka kwa Dk Tulia upo uwezekano sasa ujenzi kwenda kwa kasi ambapo hadi kukamilika zaidi ya milioni 390 zitatumika.

Chanzo: habarileo.co.tz