Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tulia apewa siri ya kushinda Urais IPU

IMG 4583 Dkt. Tulia.jpeg Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson

Sun, 9 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Baada ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kupitishwa kugombea nafasi ya Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), wanadiplomasia wameitaka Tanzania iongeze ushawishi kwa nchi mbalimbali kupata nafasi hiyo.

Dk Tulia juzi alipitishwa kuwania nafasi hiyo na wajumbe wa Jukwaa la Kibunge la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF), katika mkutano uliofanyika jijini Arusha.

Hoja ya kuungwa mkono Dk Tulia ilitolewa na mbunge wa Bunge la Afrika Kusini, Darren Bergman akiomba mabunge yote kumuunga mkono kiongozi huyo, licha ya uwepo wa wagombea wengine walioonyesha nia kwa Afrika.

Azimio la kumpitisha Dk Tulia lilifikiwa wakati tayari Bunge la Afrika (PAP) na Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EALA) limekwishapitisha jina lake kuwania kiti hicho.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na diplomasia, Abbas Mwalimu alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia hatua hiyo alisema ili Tanzania ipate nafasi hiyo ni muhimu Serikali ipenyeze ushawishi kwa nchi mbalimbali.

“Serikali inatakiwa kupenyeza ushawishi kama ilivyofanya wakati wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete kwenye uchaguzi wa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo Dk Stergomena Tax alishinda, hili ni muhimu lifanyike kwa sababu nchi za Ulaya zina msimamo wa pamoja kwenye jambo linalohusu masilahi yao,” alisema.

Dk Tax, aliyehudumu SADC kama mtendaji mkuu, sasa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mwalimu alisema endapo Dk Tulia atashika nafasi hiyo ya urais, Tanzania itajizolea sifa ya kuwa na mtu ambaye ameaminika kwenye Bunge la dunia.

Alieleza kwamba, kama wagombea wa nchi nyingine wataendelea kujitoa ndani ya kinyang’anyiro hicho, basi Umoja wa Afrika (AU) una jukumu la kumpitisha Dk Tulia.

“Kuna haja ya nchi nyingine za Afrika kuendelea kumuunga mkono Dk Tulia ili tuwe na nafasi hiyo ya pamoja, kwenye mkataba wa kimamlaka wa Afrika unasema lazima Afrika iwe na nafasi kwenye mambo yanayohusu masilahi yao, sasa hii ndiyo umuhimu wake,” alisema.

Hoja hiyo ya Mwalimu, iliungwa mkono na mtaalamu wa masuala ya diplomasia, Dk Kitojo Watengele akisema uungwaji mkono wa Dk Tulia umetokana na utendaji wake na elimu aliyonayo.

“Dk Tulia ana uelewa wa kuendesha Bunge, huwezi kuendesha Bunge kama huna uelewa, tumeona namna anavyosimamia anachokifanya, pia ana uzoefu wa kutosha,” alisema.

Pamoja na hayo, mtaalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa, Profesa Abdallah Safari alisema kitendo cha Dk Tulia kutosimamia Katiba kuondoa wabunge 19 bungeni ambao waliondoshwa uanachama wao na Chadema kitatia dosari nia yake ya kutaka kutwaa kiti cha urais wa IPU.

“Dk Tulia ameshindwa kusimamia Katiba ya Tanzania, sasa anapokwenda kugombea nje sielewi. Mtu ambaye ameshindwa kusimamia Katiba ya nchi ataweza kusimamia ya juu zaidi?” alihoji.

Kwa nini Dk Tulia

Mbunge Bergman alisema ili kuonyesha umoja katika kuwania nafasi hiyo, ni vyema kumpitisha Dk Tulia kutokana na sifa alizonazo kuwa mgombea wa SADC katika uchaguzi huo.

Ili kuhakikisha ushindi unapatikana alipendekeza mabunge ya SADC kuunda timu ya kampeni ya wabunge sita kutokana kanda za Afrika kurahisha kampeni na kuhakikisha mgombea huyo anashinda nafasi hiyo.

Hoja ya mbunge huyo iliungwa mkono na mbunge kutoka Angola, Pedro Sebastiano aliyeeleza kuwa kwa muda mrefu nafasi hiyo imekuwa ikishikwa na wabunge wanaume, hivyo kumpitisha Dk Tulia ambaye ni msomi na kijana kuwania nafasi hiyo alisema ushindi utapatikana.

Akizungumza baada ya hoja hiyo kutolewa, Rais wa Bunge la SADC, Roger Mancienne alitoa fursa ya wabunge kuchangia hoja hiyo, ambapo wabunge kutoka nchi za Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Lesotho, Zambia, Eswatini Namibia, Afrika Kusini na Mauritania walimuunga mkono Tulia.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchaguliwa kuwania nafasi hiyo, Dk Tulia aliwapongeza wabunge wote kwa kumpitisha.

Amesema miongoni mwa mambo ambayo akichaguliwa atasimamia ni kuhakikisha mabunge yanakuwa na uwakilishi wa makundi maalumu katika jamii, wakiwamo wenye ulemavu, wanawake na vijana.

"Lakini kwa kuzingatia sheria na kanuni za Bunge hilo nitajitahidi kutoa demokrasia pana zaidi katika uendeshwaji wa Bunge la Dunia," alisema.

Iwapo Dk Tulia ataukwaa wadhifa huo, atakuwa mwanamke wa kwanza kuliongoza Bunge hilo lenye nchi wanachama 179 na wabunge 705 wanaoziwakilisha nchi zao.

Bunge hilo lililoanzishwa mwaka 1889 kama kundi dogo la wabunge waliopigania amani, kwa sasa Duarte Pacheco, kutoka Ureno ndiye anayeliongoza kwa nafasi ya urais.

Chanzo: Mwananchi