Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa katiba mpya ikipatikana kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ni sawa, lakini isipopatikana haimaanishi kuwa uchaguzi hautokuwa sawa, huku akitolea mfano uchaguzi wa mwaka 2020 ambao amesema ulifanyika vizuri kwa kutumia katiba ya sasa.
Amesema wanaopendekeza suala la katiba mpya waainishe ni nini kipya wanakitaka kwenye katiba hiyo, na sio kutumia hoja kwamba katiba ya sasa ya mwaka 1977 ni ya muda mrefu sana, hivyo wanataka tu ibadilishwe.
"Katiba hii ni ya mwaka 1977 na imeshapitia mabadiliko mengi," amesema huku akieleza kwamba endapo kwenye katiba ya sasa kuna jambo linawatatiza wananchi, yeye anasikiliza maoni ya wanachi na bunge linaweza kurekebisha.