Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Timu Nchimbi, haya yanawasubiri

Siri Ya Uteuzi Wa Timu Nchimbi CCM Timu Nchimbi, haya yanawasubiri

Fri, 5 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wasomi na wachambuzi wa siasa nchini wameeleza majukumu yaliyo mbele ya viongozi wapya walioteuliwa kwenye sekretarieti ya chama hicho, ikiwamo kukiimarisha ndani na nje.

Juzi, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan ilikaa jijini Dar es Salaam na kufanya uteuzi wa viongozi kujaza nafasi zilizoachwa wazi na baadhi ya viongozi wa sekretarieti walioteuliwa serikalini.

Walioteuliwa na NEC na nafasi zao ni John Mongela, Naibu Katibu Mkuu - Bara, Amos Makalla (Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo), Ally Hapi (Katibu wa Jumuiya ya Wazazi) na Jokate Mwegelo (Katibu wa Umoja wa Vijana), wote wanaunda sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu, Dk Emmanuiel Nchimbi.

Makada wa CCM na wasomi wameeleza majukumu yanayowakabili kila mmoja wao, hasa katika kipindi hiki ambacho Taifa linaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumzia majukumu yaliyo mbele ya Mongella, mjumbe wa NEC, Richard Kasesela alisema ana kazi kubwa ya kusimamia ajira za watumishi ndani ya chama hicho.

“Ajira zote ziko mikononi mwake, na kutokana na uzoefu wake wa kufanya kazi tangu alipokuwa umoja wa vijana na serikalini, nadhani makatibu wa chama sasa watafurahia ujio wake kwa kutambua wamempata mtu anayeweza kuwatetea,” alisema.

Kasesela alisema uteuzi wake katika nafasi hiyo, anaamini atautumikia kwa weledi kwa kujenga ushirikiano na jumuiya zake.

Aliyekuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Angela Akilimali alisema kwa kuwa Mongella ni mtawala na kwa jinsi alivyo na utu uzima wake, anatarajiwa kusimamia misingi ya chama kwa kuhakikisha kila mwanachama anafanya kazi yake.

“Sidhani kama itamshinda kumsimamia kila mmoja atekeleze wajibu wake, kwa kuwa yeye ni mtawala,” alisema Akilimali.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Rukwa, Abdulkarim Halamga alisema Mongella anakabiliwa na jukumu la kujaza nafasi za watendaji, kwa kuwa baadhi ya wilaya hazina watendaji.

“Kuna baadhi ya mikoa na wilaya hazina watumishi wa chama, hata hapa Rukwa katika Wilaya ya Kalambo inaenda mwaka wa pili sasa haina watumishi, tunataka ajaze mapengo ya watumishi,” alisema.

Pia, alisema wanamtaka afikirie mafao ya watumishi wa chama hicho waliostaafu hadi sasa kwa kuwa wanapitia changamoto na hawajapewa stahiki zao.

Makalla na zigo la mafunzo

Aliyekuwa Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Itikadi na Uenezi Zanzibar, Catherine Peter Nao alisema kazi ya kwanza ya Makalla ni kutengeneza uhusiano mzuri na vyombo vya habari kwa kuzingatia nafasi yake. “Tunahitaji aseme, si kufanya maigizo. Aseme yanayofaa ili watu wasikie na tuweze kushinda chaguzi zilizopo mbele yetu, lakini kwa sasa anatakiwa kuanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo,” alisema Catherine.

Alisema wanachama wengi ni wapya na waliopita hawakuendesha utaratibu huo, hasa katika kipindi hiki wanachoelekea kwenye chaguzi.

“Mafunzo ya kwanza ni kwa ajili ya sekretarieti za kata, wilaya na mikoa, ni lazima. Mwaka huu na ujao ni wa uchaguzi, hatutaki akae majukwaani kuongea, aendeshe mafunzo maana kuna watu wengine tangu wamechaguliwa hawajapigwa msasa,” alisema Catherine.

Mchambuzi wa siasa, Gwandumi Mwakatobe alisema ukongwe wa Makalla utamwezesha kuimudu nafasi hiyo kwa sababu amewahi kukaa katika nafasi za kichama mara kadhaa na anajua shughuli zinazotakiwa kufanyika.

“Suala la uenezi si la umri, bali ni ukongwe wa kukijua chama vizuri pamoja na taratibu zake, anaweza kutekeleza majukumu yake, kuwaridhisha na kazi yake na kutangaza sera; na uamuzi wa chama siyo wake,” alisema.

Gwandumi alisema nafasi ya Makalla waliwahi kushika wengi, akiwamo John Chiligati akiwa waziri na umri mkubwa, huku akieleza umri si hoja, bali kinachotakiwa ni uzoefu na kufanya kazi vizuri.

Hapi kuwaamsha wazazi

Akimzungumzia Hapi kwenye Jumuiya ya Wazazi, Akilimali alisema anategemea kijana huyo ataichangamsha jumuiya hiyo na kuwa yenye nguvu na mwonekano mpya.

Nao alisema Hapi amekuwa mjumbe wa sekretarieti ambao ni wapishi, hivyo, kazi yake kubwa ni kuhakikisha jumuiya hiyo inaiwezesha CCM kushinda katika chaguzi zote.

Jokate kusimamia miradi

Gwandumi alisema kazi inayomkabili Jokate ni kwenda kusimamia shughuli za kiuchumi zinazofanywa na Umoja wa Vijana (UVCCM) Majengo, maeneo ya Upanga.

“Jokate ana kazi ya kutangaza sera na kuwahamasisha vijana wengi kukipenda chama na pia ana kazi nyingine ambazo zimeainishwa, lakini kwa maana ya utendaji, wanatofautiana, mwingine anakuwa mzito na mwingine mwepesi,” alisema.

Mchambuzi wa siasa, Emmanuel Makubi alisema vijana ndiyo uhai wa chama, hivyo Jokate ana jukumu kubwa la kuongeza hamasa kwa vijana kujiunga na chama hicho ili kukipatia ushindi kwenye chaguzi zijazo.

Chanzo: Mwananchi