Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tendega afunguka mazito mchakato Wabunge Viti Maalum CHADEMA

Tendegaaaaa Cdm.jpeg Tendega afunguka mazito mchakato Wabunge Viti Maalum CHADEMA

Sat, 15 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa viti maalumu ayefukuzwa uanachama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Grace Tendega amedokeza mchakato uteuzi wabunge wa viti maalum Chadema, huku akimtaja Katibu Mkuu, John Mnyika kupendekeza majina

Tendega, ambaye ni miongoni mwa wabunge 19 waliofukuzwa Chadema alisema hayo jana, wakati akihitimisha ushahidi wake katika kesi waliyoifungua Mahakama Kuu, Masjala Kuu wakipinga kufukuzwa uanachama kwa utaratibu wa mapitio ya Mahakama.

Shauri hilo namba 36 la mwaka 2022 lilianza kusikilizwa Ijumaa iliyopita

Baada ya kuanza kuhojiwa na wakili wa Chadema Peter Kibatala,Tendega aliomba Mahakama imlinde kwa yale aliyokuwa anatarajia kuyasema kwa kuwa mengine yalikuwa ni siri za chama.

Hata hivyo, Jaji Cyprian Mkeha alimkatalia akimweleza hataruhusiwa kusema jambo nje ya yale atakayoulizwa na mawakili wa Chadema.

Juzi, wakati akihitimisha ushahidi ushahidi wake, alidokeza mchakato wa uteuzi wa wagombea wa ubunge wa viti maalumu ulivyoanza ndani ya chama hicho.

Alikuwa akihojiwa na kiongozi wa jopo la mawakili wao, Ipilinga Panya, aliyekuwa akimuuliza maswali ya kumuongoza kufafanua majibu aliyoyatoa wakati akihojiwa na mawakili wa Chadema.

Tendega alidai kuwa Novemba 7, 2020 walikuwa na kikao cha Sekretarieti ya Bawacha na kupendekeza majina ya wagombea ubunge wa viti maalumu, kisha John Mnyika (Katibu Mkuu) akawasilisha mapendekezo ya majina 10.

“Siku hiyo kulikuwa na vikao vingi. Bawacha tulikuwa tunaandaa kikao cha kupendekeza majina ya wagombea ubunge wa viti maalumu,” alisema Tendega.

“Mheshimiwa John Mnyika, Katibu Mkuu alikuja na majina 10 ya Bavicha (Baraza la Vijana Chadema) na akasisitiza jina la Nusurati Hanje tusiliache.

Hata hivyo, kabla ya kuendelea zaidi, wakili Kibatala alisimama na kupinga jibu hilo akisema lilikuwa nje ya maelezo ya swali alilokuwa ameulizwa na Jaji Mkeha akakubaliana na hoja hiyo.

Jaji Mkeha alisema majibu hayo aliyoyatoa hakuwa ameyatia katika swali la msingi alipoulizwa na wakili Kibatala wakati wa maswali ya dodoso.

Alisema katika swali la msingi kuhusiana na kikao cha tarehe hiyo, shahidi alijibu kuwa alikuwa hakumbuki kuhudhuria kikao hicho na agenda zake.

Hivyo, Jaji Mkeha alimtaka asiingize kitu ambacho hakuwa amekitoa katika jibu la msingi.

Alitoa ushauri kwa mashahidi kutoa ushirikiano wanapokuwa wanaulizwa maswali ya msingi, akisema wakati mwingine mashahidi wamekuwa hawatoi ushirikiano kwa kujibu kuwa hawakumbuki au hawajui, kumbe wanapoteza nafasi muhimu ya kufafanua jambo katika hatua ya pili.

Baada ya Jaji Mkeha kukataa majibu hayo, wakili Panya aliendelea kumuuliza maswali mengine ya ufafanuzi wa maswali mbalimbali aliyokuwa ameulizwa na wakili Kibatala.

Pamoja na mambo mengine, Tendega alidai kuwa hakupewa nafasi ya kusikilizwa kabla ya uamuzi wa kumfukuza uanachama.

Alidai alitumiwa barua ya wito wa kwenda kuhojiwa Kamati Kuu ya Chadema kuhusu tuhuma za kukubali kuapishwa kuwa mbunge wa viti maalumu, kwa njia ya mtandao wa WhatsApp.

Alieleza ingawa Katiba ya Chadema inatambua matumuzi ya teknolojia ya habari, katika mawasiliano, lakini WhatsApp haijatajwa isipokuwa barua pepe tu.

Alisema wakati akiipokea barua hiyo ya Katibu Mkuu wa Chadema, Novemba 25, 2020 ikimtaka afike makao makuu ya Chama Dar es Salaam, Novemba 27 kuhojiwa, alikuwa Dodoma na kwamba aliandika barua kuomba aongezewe muda.

Alisema Novemba 26, Mnyika alimwandikia barua nyingine akimweleza kuwa kikao kingefanyika katika Hoteli ya Ledger na kwamba barua hiyo alipata Novemba 27, 2020 mchana wakati kikao kilitakiwa kufanyika siku hiyo kuanzia asubuhi.

Kutokana na hali hiyo, alisema alishindwa kuhudhuria ndipo siku hiyo hiyo Kamati Kuu ikatoa uamuzi wa kumvua uanachama.

Pia, Tendega alisema alikata rufaa Baraza Kuu, lililokaa Mei 11, 2022 ambako aliitwa lakini pamoja na kuitwa hakupewa nafasi ya kusikilizwa.

Alisema badala yake alipewa nafasi ya kuomba radhi na kuonyeshwa rufaa yake aithibitishe kama ndio yenyewe, kisha akaambiwa atoke na baadaye aliitwa na kusomewa uamuzi wa Baraza Kuu ambalo liliunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu.

“Sasa mtukufu Jaji una-apologize (unaomba radhi) nini wakati hujasikilizwa?” alihoji Tendega na kuelezea Katiba na kanuni za Chadema kuhusu haki za msingi katika kumshughulikia mwanachama kinidhamu kuwa anapaswa kuelezea tuhuma na muda wa kuzijibu na kisha kujieleza.

Pia, Tendega alisema kuwa viongozi wakuu wa Chadema akiwamo Mnyika na mwenyekiti Freeman Mbowe aliodai walitoa kauli za kuwahukumu kabla ya vikao wanajua misingi hiyo ya haki lakini waliipuuza.

Baada ya Tendega kuhitimiaha ushahidi wake, sasa ni zamu ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bawacha, Hawa Mwaifunga kuhojiwa na mawakili wa Chadema kuhusiana na maelezo yake ya kupinga kuvuliwa uanachama aliyoyatoa katika kiapo chake.

Mbali na Grace na Mwaifunga, wengine walioitwa kuhojiwa ni aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, Nusrati Hanje, Ester Matiko, Ester Bulaya, Jesca Kishoa na Cecilia Pareso.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live