Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzania yang’ara EAC wanawake bungeni

Aad846c8a80c7bd5efa1317cdf5ffca2 Tanzania yang’ara EAC wanawake bungeni

Tue, 22 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hatua za uadilifu katika siasa za kikanda zimeongeza kwa kiasi kikubwa uwakilishi wa wanawake katika mabunge huku Tanzania ikishika nafasi ya tatu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Hayo yalibainika katika ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Wanawake ulioandaliwa na Sekretarieti ya EAC kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru ambapo takwimu zilibainisha kuwa Tanzania inang’ara kwa kushika nafasi ya tatu kwa kuwa na uwakilishi wa asilimia 36.

Mbali na Tanzania kuwa na uwakilishi wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi wa kisiasa, Mkuu wa Nchi, Rais Samia Suluhu Hassan ni mwanamke huku Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson akiwa ni mwanamke pia.

Miongoni mwa wizara nyeti zinazoongozwa na wanawake ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inayoongozwa na Dk Stergomena Tax na Wizara ya Afya inayoongozwa na Ummy Mwalimu.

Kwa mujibu wa taarifa ya EAC kuhusu uwakilishi wa wanawake, Rwanda inaongoza kwa kuwa na asilimia 63.8 katika bunge la wananchi na asilimia 38.5 katika Bunge la Seneti.

“Burundi ina asilimia 36.4 katika bunge la wananchi na asilimia 41.9 katika Bunge la Seneti, Uganda kwa asilimia 35, Tanzania kwa asilimia 36, Kenya kwa asilimia 27.8 na Sudan Kusini, uwakilishi wa wanawake ni asilimia 28.5 ya viti bungeni,” ilisema taarifa iliyolifikia HabariLEO Afrika Mashariki kutoka Sekretarieti ya EAC.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Peter Mathuki alisema wanawake ni zaidi ya asilimia 50 ya wakazi wa EAC na hivyo wanashikilia ufunguo wa mafanikio katika kiuchumi.

Kwa hali hiyo alisema wanapaswa kujumuishwa kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kushirikishwa ipasavyo katika vyombo na ngazi mbalimbali za uamuzi.

"Tunahitaji kujumuisha wanawake kama washiriki hai katika kufanya maamuzi katika ngazi ya kitaifa na kikanda. Madhumuni ya hili ni kuhakikisha uamuzi unakuwa jumuishi na unaakisi matakwa ya wananchi wote,” alisema.

Kwa mujibu wa Mathuki, Ibara ya 5(e) ya Mkataba wa Kuanzishwa kwa EAC inaelekeza uzingatiaji wa jinsia katika juhudi zake kuimarisha nafasi ya mwanamke katika maendeleo ya kiutamaduni, kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia ambapo ibara ya 121 na 122 inasisitiza nafasi ya wanawake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na biashara.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Amon Mpanju, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na nchi wanachama wa EAC kuhakikisha haki sawa kwa wanaume na wanawake katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“Tanzania imepata mafanikio mengi, hayo ni pamoja na sera na mipango inayolenga kusaidia na kukuza uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, uongozi wa wanawake, upatikanaji wa huduma za msingi za kijamii pamoja na mapitio ya sheria. Hii inadhihirisha dhamira thabiti ya Serikali kuendeleza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake,” alisema.

Alitoa mwito kwa nchi wanachama kuhakikisha wanawake wana fursa sawa za kumiliki ardhi na mali, kufanya kazi zenye staha na kukuza ugawanaji bora wa kazi za matunzo zisizolipwa….

“Tunahitaji kushinda changamoto zinazoendelea ili hatimaye tupate uwakilishi wa 50/50 katika nafasi za uongozi, ili kuongeza juhudi za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live