Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tamko la Dr. Mpango kuhusu makundi na migogoro ndani ya CCM

Fd06997e9ef7eca6125490d8c752ee96.jpeg MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango

Thu, 7 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameagiza wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani wajiepushe na makundi na migogoro ndani ya chama.

Alisema hayo mjini Kibaha alipozungumza na viongozi na wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya mkoa. Dk Mpango ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Pwani.

Alisema makundi na watu wanaogombana ndani ya chama kabla na baada ya uchaguzi ni adui na saratani inayotakiwa kutibiwa mapema

“Tuepuke siasa za makundi ili kuweza kujenga chama imara na kama kuna changamoto zitatuliwe ndani ya chama kupitia vikao kwa kuwekana sana na baada ya kutoka tuwe kitu kimoja badala ya kuongelea sehemu zisizostahili,” alisema Dk Mpango.

Alisema kama kuna tofauti na zimeshindikana ni bora kuwatumia wazee ndani ya chama ili kupata busara zao na kutatua changamoto zilizopo.

“Tiba ipatikane mapema na kuwe na mahusiano mazuri kati ya viongozi wa chama na serikali ili kuwaletea maendeleo wananchi ambapo mahusiano mabaya yanasababisha kuzoofisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya elimu,afya,maji,barabara na mingineo,” alisema Dk Mpango.

Alisema katika uchaguzi wa chama na jumuiya zake unaotarajiwa kufanyika mwakani lazima wachaguliwe viongozi wenye sifa hasa akina mama na vijana kwa kuwatambua na kuwaandaa.

“Mwaka 2025 nasikia wanawake mna jambo lenu hivyo viongozi wapeni nafasi pikeni vyema viongozi waadilifu na waaminifu na wenye uwezo mkubwa na mdikubali kubebwa kikubwa ni kujiamini kwani uwezo mnao,” alisema.

Alipongeza chama mkoa kwa kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia uchaguzi kwa kuwa ni bila hivyo baadhi ya wanachama wenye uchu wa madaraka wanaweza kuulipia uchaguzi kisha kujinufaisha.

“Chama kikigharamia uchaguzi kitasaidia kuondoa wale wanaotaka uongozi kwa kutaka kunufaisha matumbo yao hivyo tusikubali hilo, chama kujiimarisha kiuchumi ambapo siasa bora zinaendana na uchumi hivyo viongozi wanapaswa kusimamia kwa kuwa na mipango ya kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuwa na chama imara kisicho kuwa ombaomba,” alieleza.

Alikipongeza chama mkoani humo kwa ushindi walioipata kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita kwa kushinda kwa asilimia 100 ambapo yeye anakotoka walipata ushindi kwa asilimia 77.

Chanzo: www.habarileo.co.tz