Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taarifa ya ACT kuhusu uamuzi wa serikali waliopata ujauzito kurejea shuleni

Mjamzito Taarifa ya ACT kuhusu uamuzi wa serikali waliopata ujauzito kurejea shuleni

Sat, 27 Nov 2021 Chanzo: ippmedia.com

CHAMA cha ACT Wazalendo kimepongeza hatua ya serikali ya kukubali kurejeshwa shuleni na kuendelea na masomo kwa wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa katika shule za msingi na sekondari.

Mapema wiki hii, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akitoa taarifa ya mafanikio ya sekta ya elimu kuelekea miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, alisema serikali itaondoa vikwazo mbalimbali katika upatikanaji wa fursa za elimu.

Kwa mujibu wa Ndalichako, vikwazo hivyo ni pamoja na kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kupata ujauzito.

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake ya ACT- Wazalendo, ilisema hatua hiyo ni ya msingi katika utekelezaji wa haki za watoto pamoja na mikataba ya kimataifa kuhusu watoto.

Alisema suala hilo limo katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 ya chama hicho, hivyo wanaunga mkono uamuzi huo ingawa serikali ya awamu ya tano ilipinga na kufuta jambo hilo kwa wanafunzi wanaokumbwa na matatizo hayo kurudi shuleni na kupata elimu katika mfumo rasmi.

“Hatua hii ilifikiwa kwa matamko ya hadharani yaliyotolewa na viongozi wa serikali wakiongozwa na Rais mwenyewe, Hayati John Pombe Magufuli kwa madai kwamba serikali yake haiwezi kusomesha 'wazazi'.

“Chama chetu, kupitia kwa Kiongozi Mkuu Zitto Kabwe, kilichukua msimamo na hatua kali dhidi ya uamuzi ule wa serikali ya kuwanyima watoto elimu kwa sababu ya ujauzito. Wadau wengine pia walijitokeza na kupaza sauti zao na kupingana na uamuzi wa Rais Magufuli na serikali yake,” ilisema taarifa hiyo.

Hatua hiyo ya Zitto ilisababisha kushambuliwa kukashfiwa na kuitwa msaliti na baadhi ya viongozi wa serikali na ndani ya Bunge na wabunge wa CCM.

Kukashfiwa huko kwa Zitto, taarifa hiyo ilisema, ilitokana na uamuzi aliochukua wa kuishawishi Bodi ya Benki ya Dunia (WB) kutoipa serikali ya Rais Magufuli mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 500 (sawa na zaidi ya Sh. trilioni 1.1 za Kitanzanai) uliolenga kuboresha mfumo na miundombinu ya elimu.

Zitto aliikumbusha Bodi ya Benki ya Dunia inayotoa idhini kutolewa kwa mkopo huo kuwa mkopo huo utakuja kutumika kwa ubaguzi kwa kuwaacha nje watoto wengine kwa kisingizio kuwa wamepata ujauzito wangali shuleni na hivyo hautaweza kufikia lengo lililokusudiwa la kuwakomboa watoto wa Kitanzania kielimu.

 

HAKI ELIMU YANENA

Taasisi ya HakiElimu imeipongeza serikali kwa kuruhusu wanafunzi waliokatiza masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito kurudi shuleni.

Hata hivyo, imeishauri serikali kukazia waraka huo mpya unaowaruhusu kurejea shuleni, kufanyia mabadiliko sera na sheria ya elimu ili iwe rasmi badala ya kuishia hivyo ulivyotolewa.

Taasisi hiyo pia imeiomba serikali kuandaa mwongozo ambao utaeleza bayana namna mwanafunzi anayepata ujauzito akiwa shuleni, anavyoandaliwa kisaikolojia wakati anaondolewa kurudishwa nyumbani kwenda kujifungua na hatua anazotakiwa kufuata wakati anarejea tena baada ya kujifungua.

"Na mwongozo huo ndio utaeleza mambo mengi kwa uwazi, baada ya kujifungua arudishwe kwenye shule ile ya awali au vinginevyo, nani atahusika wakati wa kumpokea wakati anarejea na taratibu nyinginezo,"alisema Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk. John Kallaghe.

"Lakini pia waraka huu ukitumika na ikatamkwa rasmi kwenye sera na sheria inakuwa ndio uhakika na si rahisi hata kiongozi mwingine anapoingia kubadilisha kuliko ikibaki kwenye waraka tu kama hivyo ulivyotolewa," aliongeza.

Dk. Kallaghe alisema uko mwongozo ambao serikali iliwahi kuuandaa mwaka 2009 ambao ulikuwa ukieleza namna wanafunzi hurejea shuleni baada ya kukatiza masomo yao, lakini haukuwahi kutumika wala kutiwa saini na kushauri kwamba endapo serikali itaridhia inaweza kuutumia kwa sasa.

Dk. Kallaghe alisema takwimu za Elimu (BEST 2020) mwaka 2015 zinaonyesha kuwa wanafunzi wa kike 3,439 waliacha shule kwa sababu za ujauzito na idadi iliongezeka hadi kufikia wanafunzi 6,533 mwaka 2019 ikiwa ni ongezeko la asilimia 90.

Chanzo: ippmedia.com