Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TLP kumteua Magufuli kuwa mgombea wao wa urais uchaguzi mkuu 2020

98662 Pic+mrema TLP kumteua Magufuli kuwa mgombea wao wa urais uchaguzi mkuu 2020

Wed, 11 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha TLP kitafanya mkutano wake mkuu ambao pamoja na mambo mengine utamteua mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kuwa mgombea wao wa urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2020.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, Magufuli alipata kura milioni 8.8 huku mgombea wa upinzani, Edward Lowassa, aliyeungwa mkono na vyama vinne, akipata kura milioni 6.07.

Katika mkutano huo wa TLP utakaofanyika Mei 9, 2020 jijini Dar es Salaam utafanyika uchaguzi wa viongozi wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Machi 11, 2020 mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema amesema hawatasimamisha mgombea katika uchaguzi mkuu na badala yake watamuunga mkono Magufuli kama akigombea kupitia CCM.

“Nachukua nafasi hii kumpongeza Rais Magufuli kwa hekima na busara yake kwa kufanya maamuzi ya kihistoria ya kuzungumza na viongozi wa upinzani.

“Walikuwa wanamsema hapendi upinzani lakini kitendo chake cha kuwaita Ikulu inaonyesha anapenda demokrasia tena ya kweli, tunampongeza kwa uamuzi huo,” amesema Mrema.

Pia Soma

Advertisement
Amesema hatua hiyo imezidisha vyama vya upinzani kumuelewa Magufuli kuwa ana nia njema hivyo waache kumsema vibaya.

Mrema amesema uamuzi huo wa Magufuli umetoa mwanga kwa wapinzani kuona uchaguzi utakuwa huru na haki.

“Tumemnukuu mwenyekiti wa NCCR Mageuzi,  James Mbatia mara baada ya kutoka Ikulu alisema anaamini uchaguzi mkuu utakuwa huru na haki. Hayo ni maneno yake na sisi hayo tuliyaona mapema sana kwamba tuna Rais muungwana na mkweli lakini walitudhihaki,” amesema Mrema

Chanzo: mwananchi.co.tz