Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TLP, CCM wachuana Tandahimba kuwania kitongoji na kijiji kimoja

Mon, 25 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tandahimba. Jumla ya vyama viwili vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Tanzania Labour Party (TLP) wilayani Tandahimba mkoani Mtwara vimeshiriki uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika leo Jumapili Novemba 24, 2019 kwa ajili ya kumchagua kiongozi wa kitongoji cha Kiwanjani kata ya Tandahimba na wajumbe mchanganyiko wa serikali ya kijiji cha Nahnyanga C.

Hatua hiyo ya ushiriki wa vyama viwili imekuja baada ya baadhi ya vyama vya  upinzani kujitoa na baadhi ya wagombea wa CCM kupita bila kupingwa.

Mwandishi limepita katika baadhi ya vituo vya upigaji kura na kuona baadhi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura wengi wao wakiwa ni wakina mama na wazee wa jinsia zote.

Hadi kufikia majira ya saa tano asubuhi kasi ya upigaji kura ilianza kupungua na mtu mmoja mmoja kuanza kwenda katika kituoni kupiga kura na kuangalia kama jina lake lipo katika orodha ya wapiga kura na kisha kupiga kura na kuondoka katika hali ya utulivu.

Mmoja wa wapiga kura Aisha Mzee amesema amejitokeza kupiga kura ili kutimiza haki yake ya kikatiba kumchagua kiongozi wanayemtaka kuongoza kitongoji cha Kiwanjani na kuwatatulia changamoto zinazowakabili.

“Kitongoji chetu kina changamoto, mitaa yetu hata tukisema masuala ya usafi ni kero kwa hiyo ndio maana mimi binafsi nimejitokeza kupiga kura kumchagua ninayemuhitaji,” amesema Mzee

Ismail Rashid amesema amejitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi anaowataka kutokana na umuhimu uliopo.

“Mwitikio upo sio mkubwa sana ni mdogo kwa sababu wengi hawakujiandikisha kupiga kura kila mmoja ana matakwa yake mfano mimi nilijiandikisha kwa sababu niliona umuhimu wa kupiga kura,” amesema Rashid

Msimamizi wa uchaguzi halmashauri ya wilaya ya Tandahimba, Ahmed Suleiman amesema halmashauri hiyo ina uchaguzi wa nafasi mbili ambazo ni nafasi ya mwenyekiti wa kitongoji cha Kiwanjani kata ya Tanadahimba ambapo vyama vinavyoshiriki ni TLP na CCM.

Nafasi ya pili ni uchaguzi wa nafasi mchanganyiko katika kijiji cha Nahnyanga C ambapo nafasi kumi zinagombewa na wagombea 12 kati yao kumi wakitoka CCM na wawili TLP.

“Kijiji cha Nahnyanga C vituo vya kupigia kura viko saba na vituo vimefunguliwa ndani ya muda tangu asubuhi na uchaguzi unaendelea vizuri kwa wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wakiendelea kuratibu zoezi hilo,na tunawashukuru wananchi tangu asubuhi wameendelea kujitokeza ili kutimiza haki yao ya kimsingi,”amesema Suleiman

Amesema halmashauri hiyo ilikuwa na nafasi ya vijiji 142 na nafasi zote hizo baadhi ya vyama vilijiondoa katika uchaguzi baada ya kuchukua na kurejesha fomu na hivyo CCM kupita bila kupingwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz