Wadau wa siasa nchini, wametoa mapendekezo 10 kuhusu hali ya demokrasia nchini, ikiwamo kuwapo uhuru wa kisheria wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani.
Mbali na uhuru huo, pia walipendekeza kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi, mgombea binafsi ili kuwapa mwanya wasio na vyama kushiriki hatua hiyo muhimu ya kidemokrasia.
Wadau hao walitoa mapendekezo hayo katika mkutano wa kitaifa kuhusu hali ya demokrasia nchini, ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), uliofanyika kwa siku mbili mfululizo jijini hapa.
Kutungwa kwa sheria hiyo ni kilio cha muda mrefu cha wadau wa siasa, kinachokosoa Katiba ya Tanzania inayominya uhuru wa kuihoji Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais.
Nchi nyingi Afrika, kupitia katiba zao zimeruhusu matokeo ya urais kuhojiwa mahakamani, zikiwemo Uganda, Malawi, Afrika Kusini, Zimbabwe na Kenya.
Akitoa maazimio hayo wakati wa kuhitimisha mkutano huo jijini hapa jana, Mwenyekiti wa TCD, Profesa Ibrahim Lipumba alisema ni muhimu kuwepo uhuru wa kisheria kuruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani.
Pamoja na hilo, lingine lililoazimiwa ni ushindi wa rais uamuliwe kwa kupata kura zaidi ya 50, badala ya ilivyo sasa ambapo hata asilimia 15 zinampa nafasi hiyo ilimradi awe ameongoza.
Alisema azimio lingine ni muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba kuwasilishwa bungeni pamoja na muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa.
Alieleza hatua hiyo ndiyo muafaka wa kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya kufikia uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Awali, kulikuwepo na hofu ya kufikia chaguzi hizo bila kuwa na tume huru ya uchaguzi.
“Kwa sababu muda ni mfupi, tukisema tuanze mabadiliko ya Katiba kisha sheria, hatutaweza kuyakamilisha kwa muda muafaka," alisema.
Azimio hilo kwa mujibu wa Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), liliambatana na lile la kufanyika kwa mabadiliko madogo ya Katiba badala ya kuifumua yote.
“Mkutano ulipendekeza kufanyika mabadiliko muhimu katika Katiba iliyopo sasa, ili kupanua uwepo wa demokrasia na tume huru ya uchaguzi kuelekea uchaguzi ujao,” alisema.
Hata hivyo, msingi wa azimio hilo ni hoja ya Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyesema upo uwezekano wa kufanya mabadiliko ya sheria za uchaguzi kama hatua za awali, huku ule mchakato wa Katiba mpya ukiendelea.
"Ukiendelea mjadala wa nianze hiki, utafika uchaguzi bila hatua yoyote kufikiwa," alisema.
Fomu zitolewe bure
Katika mabadiliko ya sheria ya uchaguzi, Profesa Lipumba alisema wadau wameazimia kuondolewa kwa gharama za uchukuaji na urudishaji fomu ya uchaguzi, katika nafasi mbalimbali ili kuongeza ushiriki wa wananchi kuwania uongozi.
"Nakumbuka kwenye urais, inahitajika ukirudisha fomu upeleke na Sh1 milioni, sasa kuna watu wanataka kugombea urais na hawana hiyo fedha.
"Unaweza kuwa huna Sh1 milioni lakini una mawazo mazuri ya kuwaletea Watanzania, kwa hiyo hiki kikwazo kiondolewe," alisema.
Maazimio mengine ni mabadiliko ya sheria ya utumishi wa umma, ili kutoa mwanya kwa watumishi wa umma wanaoshindwa katika uchaguzi warejee kazini.
Mzizi wa azimio hilo ni kauli ya Mratibu wa Kitaifa wa Ulingo, Dk Avemaria Semakafu aliyesema wanawake wanahofu kushiriki kugombea watapoteza nafasi zao katika utumishi wa umma.
Akisoma azimio hilo, Profesa Lipumba alisisitiza, “Hili linakwaza hasa wanawake ambao wengi ni watumishi wa umma, wanaogopa kugombea kwani wakikosa nafasi hizo watakuwa wamepoteza ushindi na kazi," alisema.
Utaratibu wa sasa, utumishi wa umma wa mgombea utakoma pale tu NEC itakapomtangaza kuwania nafasi ya uongozi.
Maazimio mengine kwa mujibu wa Profesa Lipumba ni Serikali iwezeshe majadiliano baina ya vyama vya siasa, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usimamiwe na tume huru ya uchaguzi badala ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Pia vyama vya siasa viwekewe sharti la kisheria kutoa fursa kwa wanawake na makundi maalumu kushiriki katika ngazi za maamuzi, kufanyike mabadiliko ya sheria ya Jeshi la Polisi ili iendane na mahitaji ya demokrasia. Pia waliazimia kutumika kwa lugha nzuri na za staha katika majukwaa ya siasa.
Kwa upande wa Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle aliwataka Watanzania kuwa na demokrasia inayoendana na mazingira yake, kwa ajili ya watu wake na itakayojengwa na Watanzania wenyewe.