Sintofahamu imeibuka kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kuhusu vibali vya helikopta iliyopangwa kutumiwa na chama hicho katika operesheni +255 Katiba mpya ya kanda ya Nyasa.
Wakati Chadema ikidai iliomba vibali kupitia kwa wakala wao kwa mujibu wa taratibu na kuruhusiwa kisha saa chache kuzuiwa hadi wakati mwingine, TCAA imekana kuinyima kibali ikieleza taratibu hazikufuatwa.
Chadema ilipanga kutumia helikopta hiyo kwenye mikutano yake ya hadhara ya kanda hiyo yenye mikoa ya Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe na Rukwa kuanzia Oktoba 21 hadi Novemba 16 mwaka huu, ikitumiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Hata hivyo, mikutano hiyo ilizinduliwa Tunduma Mjini, Mkoa wa Songwe Oktoba 21 na kuendelea huku Mbowe akitumia gari tofauti na matarajio yao hadi Oktoba 24 mwaka huu alipositisha kupisha mitihani ya darasa la nne na tangu wakati huo haijaendelea.
Gazeti hili, lilikuwa la kwanza kuripoti utata wa helikopta hiyo kukwama kuingia nchini hali iliyomfanya Mbowe kurejea Dar es Salaam kufuatilia vibali hivyo huku mikutano nayo ikiwa imesimama.
Baadhi ya viongozi bado wako Rukwa wakisubiri hatima hiyo na wengine wakirejea maeneo yao kwa muda.
Juzi, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alitoa taarifa kwa umma akikana kuinyima vibali Chadema huku akifafanua hakuna chama chochote cha siasa kilichoomba vibali vya helikopta.
“Hata hivyo, Oktoba 20, TCAA ilipokea ombi kutoka wakala wa vibali vya ndege kwa ajili ya kuanisha maeneo ambayo viongozi wa Chadema watakuwa wakiruka na kutua katika maeneo yasiyo rasmi ili kufanya mikutano ya hadhara. Lakini hakuna nyaraka zozote zilizowasilishwa TCAA kwa ajili ya kuingiza ndege nchini kwa mujibu wa sheria,”alisema Johari.
“Kwa namna yoyote ile, mamlaka haina sababu ya kukataa kibali cha ndege ikiwa ombi na nyaraka zinakidhi vigezo.” Hata hivyo, tofauti na maelezo ya Johari, barua mbili kutoka TCAA za Oktoba 20 mwaka huu zilizosainiwa na S. Msangi kwa niaba ya Johari kwenda kwa Flight Operations, Servair Aviation Company Limited ambazo gazeti hili limeziona, zinaonesha kuruhusiwa na kuzuiwa.
Barua ya kuruhusiwa inaelezwa ilitolewa mchana wa Oktoba 20 mwaka huu, ikimweleza wakala huyo kuweza kuruhusu helkopta hiyo kuanzia Oktoba 20 hadi Novemba 30 mwaka huu kwenye mikoa mitatu huku wakitakiwa kuzingatia usalama wao pamoja na wananchi.
Siku hiyohiyo ya Oktoba 20, barua nyingine iliandikwa kwenda kwa wakala huyo kuzuia kibali kilichokuwa kimetolewa kuwasafirisha viongozi wa chama kwenye mikutano ya hadhara kutokana na sababu za kiusalama hivyo kusitisha kibali hadi wakati mwingine.
Baada ya maelezo hayo ya TCAA na barua hizo, gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ambaye alisema,“sisi tunauzoefu wa kutumia chopa kwa miaka mingi, tunajua taratibu za kuomba vibali, waulizeni TCAA ilikuwaje wakatupa kibali mchana na usiku wa siku hiyohiyo wakakifuta.”
Mrema alisema kuna mambo ambayo TCAA hawataki kuyaweka wazi yakiwamo ya kisiasa ambayo wanajua wenyewe.
“Kwa nini watuzuie, tumewahi kurusha chopa mikoa hiyohiyo ambayo leo wanasema sijui sio salama, hivyo ninyi waulizeni waseme ukweli kwani hata huo ufafanuzi wao unakinzana na barua zao wenyewe,” alisema Mrema.
Alipotafutwa Johari hakupatikana, lakini Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa TCAA, Yessaya Mwakifulefule alisema: Taarifa ya mkurugenzi mkuu imejibu kila kitu, wao walichosema, kibali kinaombwa ndani ya mfumo sio nje ya mfumo. Kibali kinaombwa na mmiliki au wakala ndege sio wewe mteja, ndio kilichoelezwa katika taarifa ya mkurugenzi mkuu.”
Baada ya majibu hayo, gazeti hili lilitaka kujua hizo barua ni kweli zilitolewa na mamlaka hiyo, Mwakifulefule alijibu kwa ujumbe mfupi wa maandishi: “Ukisoma ufafanuzi wa DG (mkurugenzi mkuu) umesema kabisa kwamba maombi yaliombwa nje ya mfumo kwa barua.”
Alipoulizwa kama uliombwa nje ya mfumo, ilikuwaje kibali kikatolewa kuruhusu matumizi ya helkopta hiyo? Baada ya swali hilo meneja huyo wa mawasiliano alisisitiza ufafanuzi wa mkurugenzi mkuu uzingatiwe.