Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sumaye kukataliwa uenyekiti Kanda ni mchezo mchafu au amechuja kisiasa?

86632 Pic+sumaye Sumaye kukataliwa uenyekiti Kanda ni mchezo mchafu au amechuja kisiasa?

Mon, 2 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuna wanaosema siasa ni mchezo mchafu kutokana na mambo mabaya wanayotendeana wanasiasa, lakini wengine wanasema siasa si mchezo mchafu kwa kuwa majukumu anayobeba mwanasiasa ni ya kitaifa kwa masilahi ya Taifa.

Wanaosema siasa ni mchezo mchafu wanajenga hoja kwamba kinyang’anyiro cha kuwania madaraka, iwe ndani ya chama au mamlaka ya kiserikali huwafanya wanasiasa wachafuane kwenye kampeni na kufanyiana rafu wakati wa upigaji kura.

Lakini, mwanafalsafa Plato kwenye moja ya maandiko yake anasema siasa si mchezo mchafu kwa kuwa usiposhiriki siasa kuna hatari ya kutawaliwa na watu dhaifu.

Plato anasema hivi; “Moja ya adhabu kwa kukataa kushiriki siasa ni kuishia kutawaliwa na mtu dhaifu.” Kauli yake hiyo anaitetea kwa hoja kwamba jukumu la wanasiasa ni kushughulikia masuala muhimu ya kuboresha uchumi, fedha na kuimarisha jeshi la nchi.

Hivyo, mwanasiasa awe wa chama tawala au wa upinzani hawezi kukwepa jukumu la kushughulikia mambo muhimu ya maendeleo kwa kuisimamia ipasavyo Serikali ndani ya Bunge na kutumia majukwaa ya kisiasa kuileza Serikali shida za wananchi.

Kura nyingi zilizomkataa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye wakati akitetea nafasi yake ya mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani inaweza kuwa ni mchezo mchafu au amechuja kisiasa.

Hata hivyo, Sumaye amesema kushindwa kwenye uchaguzi huo kumetokana na kitendo chake cha kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho ambayo kwa sasa inashikiliwa na Freeman Mbowe. Kwa maana nyingine amelalamikia mchezo mchafu.

Sumaye si mara ya kwanza kulalamika kufanyiwa mchezo mchafu kwenye siasa. Baada CCM kumpitisha Jakaya Kikwete kuwania urais mwaka 2005, Sumaye alitangaza kutogombea ubunge Hanang na kujiweka pembeni na siasa.

Hata hivyo, mwaka 2012 alijitokeza kuwania ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM lakini akashindwa na mrithi wake wa ubunge katika jimbo la Hanang, Mary Nagu.

Baada ya Sumaye kushindwa na Nagu, alipaza sauti kuhusu kuchezewa rafu.

Ukiangalia historia ya Sumaye, ni mkongwe katika siasa aliyeingia bungeni akiwa kijana mwenye umri wa miaka 33. Alichaguliwa kuwa Mbunge wa Hanang mwaka 1983.

Mbali na kuwa mbunge kwa miaka 12, vilevile alikuwemo kwenye Baraza la Mawaziri kwa miaka 10, yaani kipindi chote cha utawala wa Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi.

Miaka miwili ya mwisho ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tayari Sumaye alishakuwa mbunge.

Sifa ambayo amekuwa nayo Sumaye kwenye utendaji wake serikalini hakuwa na usumbufu kikazi, wala kumbukumbu za kuropoka ropoka hovyo, ukaidi, ubishi wala kujiamini kupita kiasi.

Pia, rekodi zinaonyesha kuwa Sumaye ni mwanasiasa mtulivu, anayeangalia wajibu wake na kuutimiza. Hana mambo mengi kwa sababu hapendi makuu na ndiyo maana wakati anateuliwa kuwa waziri mkuu, alishakuwepo bungeni kwa miaka 12 lakini jina lake halikuwa kubwa.

Hii ndiyo sababu Rais Mkapa alipopeleka jina la Sumaye bungeni kutaka apitishwe kuwa waziri mkuu wake, watu walishangaa, waliulizana, ndiye nani huyo? Hata wabunge, hususan wale wapya, hawakuwa wakimjua.

Kikatiba waziri mkuu ndiye mshauri mkuu wa Rais kiutendaji na msimamizi mkuu wa utekelezaji sera na mipango ya kila wizara na kila taasisi ya umma.

Waziri Mkuu ndiye msimamizi wa rasilimali za umma, ndiye mtendaji mkuu wa shughuli za kila siku za Serikali. Kwa maana hiyo, huwezi kusifia mafanikio ya Mkapa, lakini ukawa hutaki kumpa thamani yake Sumaye ambaye alikuwa waziri mkuu wake kwa kipindi chote cha uongozi wake.

Hata hivyo, kuna wakati alitoka hadharani na kuisema CCM wakati huo akiwa bado mwanachama wake, kwamba ina wajibu wa kujibu mashambulizi yanayotolewa na Chadema dhidi ya Serikali.

Pia, wakati huo huo aliwaeleza vijana wa CCM kwamba hakuna wa kumzuia kugombea urais, iwapo ataamua kufanya hivyo.

Sumaye alikuwa akijibu kile alichoita, “matamshi ya hovyo” yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wakuu wa chama chake na viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM).

UV-CCM mkoani Pwani na taifa walimtuhumu Sumaye kutafuta urais pale aliposema kuwa hoja zinazotolewa na Chadema, zijibiwe na CCM na siyo kuacha jukumu hilo kwa Serikali.

Sumaye alitaka chama chake kuacha kulalamika badala yake kufanya kazi za kisiasa katika kukabiliana na Chadema.

Agosti 22, 2015, Sumaye alitangaza kujiondoa CCM na kujiunga na Ukawa iliyojumuisha vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD wakimuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.

Sumaye alijiunga Ukawa kwa hoja kwamba anakwenda kuimarisha upinzani kwa kuwapa uzoefu na kwenye kampeni za urais alikua msemaji mkuu kwenye mikutano yote iliyohutubiwa na Lowassa.

Wakati Lowassa ametangaza kurudi CCM, Sumaye ambaye ana maumivu ya kunyang’anywa mashamba na Serikali alisema hatorejea CCM na ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Chadema.

Mbali na kusema hatarejea CCM, pia Sumaye wakati alipochukua fomu ya kugombea uenyekiti wa kanda alikuwa akihubiri wagombea kukubali matokeo na kutochafuana.

Sumaye, kama Waziri Mkuu mstaafu hakupaswa kuangushwa namna ile. Katika siasa inafahamika kuwa hilo ni kosa kubwa, kwamba hupaswi kuwa na malengo ya kugombea ubunge, halafu unaanza kugombea udiwani au uenyekiti wa kijiji na ukashindwa.

Kitendo cha Sumaye kuchukua fomu ya kugombea uenyekiti wa Chadema Taifa, lakini wakati huo huo akaamua kugombea uenyekiti wa Kanda lilikuwa ni kosa la kiufundi kisiasa.

Kushindwa wadhifa mdogo ndani ya chama au serikalini kunaashiria kwamba hutakubalika katika ngazi kubwa; huna ufuasi mkubwa ndani ya chama kwani inaonekana huna ushawishi hata unakotoka.

Kete aliyobakia nayo Sumaye ni fomu ya uenyekiti wa Chadema Taifa kama atairejesha kuwania nafasi hiyo na kama atacheza karata zake vizuri na kushinda nafasi hiyo, kisiasa atakuwa anaendelea kutakata.

Lakini, kama atashindwa kurejesha fomu hiyo inaweza kutafsiriwa mwanzo wa kuchuja kisiasa kwa Sumaye na hata kama atahama chama hicho, mvuto wake utaendelea kuwa hafifu.

Kitendo cha Chadema kumnyima kura Sumaye ni kielelezo kwamba ana safari ndefu kisiasa, aliwahi kuwakebehi wanaCCM waliokuwa wakikimbilia upinzani, lakini kitendo cha wanaCCM wengine waliokwenda upinzani kwa mafuriko na baadaye kuamua kuunga mkono juhudi kwa kurejea CCM, kinaweza kuwa pigo kwa Sumaye hata kama msimamo wake ni kubaki upinzani.

Chanzo: mwananchi.co.tz