Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sumaye atoa somo kwa Nec, Serikali

15107 Ic+sumaye TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ameeleza mambo matatu muhimu ya kuzingatia wakati nchi ikielekea kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika Septemba 16.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana, Sumaye alisema mambo hayo ni utawala bora, matumizi sahihi ya vyombo vya dola na kutambua umuhimu wa uchaguzi.

Alisema mambo hayo kama yasipozingatiwa katika uchaguzi huo, huenda yakaibuka machafuko.

Sumaye ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani alitoa kauli hiyo wakati akieleza mwenendo wa kampeni za uchaguzi zinazoendelea jimbo la Ukonga.

Alisema uchaguzi huo unapaswa kuwa wa haki na uwazi na ushindani wa halali.

Kuhusu utawala bora, Sumaye alieleza kuwa Tume ya Taifa ua Uchaguzi (Nec) inapaswa kuwa huru kwa kuwa ndiyo mhimili kwenye uchaguzi.

Pia, Sumaye aliiomba tume hiyo kuweka ratiba mapema ya yakiwamo majina ya wapiga kura, siku saba kabla ya uchaguzi ili kuondoa usumbufu.

Alivitaka vyombo vya dola kutofuata maagizo ambayo yanalenga kupendelea upande mmoja.

Sumaye alisema jukumu la mhimili huo ni kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa amani bila vurugu ambazo zilijitokeza katika uchaguzi uliopita.

“Siyo kuwapiga watu au kuwakamata bila makosa, hii inasababisha chuki kwa wananchi kwa hiyo wao wahakikishe amani inakuwapo na siyo kutumika vibaya,” alisema.

Kuhusu kutambua umuhimu wa uchaguzi, Sumaye alisema hakuna jambo linaloweza kuingiza nchi katika machafuko kama uchaguzi, hivyo kuwataka wananchi waachwe wachague kiongozi wanayemtaka, si kinyume chake.

“Tunashuhudia mara kwa mara nchi nyingi duniani zinaingia kwenye machafuko kwa ajili ya uchaguzi ambao haufuati sheria, haki na usawa hivyo tunaamini amani tuliyonayo haitaingia mashakani kwa ajili ya uchaguzi tutendee haki,” alisema na kubainisha kuwa wapo tayari kupokea matokeo ya haki.

Chanzo: mwananchi.co.tz