Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sumaye: Tusifurahie Bunge la chama kimoja

Sumaye Pic Tztzzz Sumaye: Tusifurahie Bunge la chama kimoja

Tue, 18 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuonyesha ‘madudu’ ya ubadhirifu wa fedha kwenye maeneo mbalimbali, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameibuka akisema Bunge linapaswa kuwa kali katika kuisimamia na kuishauri Serikali.

Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu kwa muongo mmoja kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 katika utawala wa Awamu ya Tatu amesema kwa kawaida hakuna Serikali ya demokrasia inayokataa ushauri wa Bunge.

“Haya mambo yanapojitokeza mara kwa mara lazima tukubali kuna tatizo mahali fulani, kubwa kabisa ni Serikali lakini Bunge nalo halifuatilii,” alisema.

Sumaye anatoa kauli hiyo ikiwa ni takribani wiki mbili zimepita tangu Ripoti za CAG Charles Kichere kwa mwaka 2021/22 zilizowasilishwa bungeni jijini Dodoma.

Katika mahojiano kati ya Sumaye na televisheni ya mtandaoni ya Dar 24, yalijikita katika masuala mbalimbali yanayomhusu Sumaye na ripoti za CAG, alisema;

“Bunge lina kazi kubwa na linatakiwa liwe na ukali zaidi, ndiyo maana tunapenda Bunge lenye vyama mbalimbali kwa sababu ni afya kwa nchi.

“Hiki kitu watu hawakielewi, watu wanafikiri ukiwa na Bunge la chama kimoja, ndio njema, hapana. Ukiwa na Bunge la chama kimoja ndani ya mfumo wa vyama vingi ni tatizo,” alisema.

Ripoti za CAG alizokuwa anadili Sumaye zimeonyesha ubadhirifu katika taasisi na mamlaka za Serikali, hali ambayo imewaibua wadau wakitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan, amekwishaanza kuchukua hatua kwa kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) na kuivunja Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mbali na hilo, Rais Samia ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka kuhakikisha makatibu wakuu na watendaji wakuu wote wa taasisi za Serikali wanapitia kwa kina taarifa ya CAG, wajibu na kuzifanyia kazi kwa haraka hoja zote.

Pamoja na maagizo hayo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akiwa ziarani mkoani Mwanza wiki iliyopita alisema hatua zimekwishaanza kuchukuliwa huku akisisitiza, “watakaothibitika kwenye taarifa za GAG au waliokula fedha zenu watapata cha moto.”

Bunge la sasa ambalo lilitokana na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, lina wabunge wengi wa chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM), zaidi ya asilimia 90 huku upinzani wakiwa wachache tofauti na mabunge yaliyopita na wengine hawatambuliwi na vyama vyao.

Aprili 12 mwaka huu, Spika Tulia Ackson alisema wabunge wanaruhusiwa kuijadili ripoti hiyo kwa namna wanavyoona inafaa lakini watambue kuwa Serikali haitalazimika kujibu kwa kuwa Kamati za Bunge Mashirika ya Umma (PAC) na ile ya Serikali za mitaa (LAAC) itapitia taarifa hiyo na itawasilishwa bungeni.

Katika mahojiano hayo, Sumaye aliulizwa je, waziri mkuu anapaswa kuwajibika kutokana ripoti ya CAG akajibu, “Waziri mkuu anawajibika si kwa kufukuzwa bali anatakiwa kuhakikisha yaliyoelezwa na CAG yanashughulikiwa kwa sababu yeye ndiye mtendaji mkuu wa Serikali.

“Ni jukumu lake haya yametokaje, hili limekwendakwendaje na kwa nini limetokea, kama ubadhirifu umetokea wizara ya fedha, husika anaanza kuangaika, lakini waziri mkuu anashusha nyundo yake ili kupata majibu yanayoridhisha,” alisema.

Ufisadi jambo la ovyo

Sumaye, alisema ufisadi ni jambo la ovyo lisilopaswa kuvumiliwa na wanaoshiriki nao pia wasiachwe wafanye watakavyo.

Sumaye ambaye mwaka 2015 alihamia Chadema kisha Februari 2020 akarudi CCM, alisema yale maeneo yanayoonekana ni tatizo inatakiwa Bunge liyashughulikie pamoja na Serikali ili Watanzania kupata taarifa kamili.

“Unaweza ukakuta ripoti ya CAG ikitoka robo tatu Serikali ikawa na majibu, lakini kutakuwa na robo hakuna majibu, hilo ndilo tatizo. Lakini ripoti zinapotoka Serikali inatakiwa kujibu maswali yaliyoulizwa,” alisema Sumaye aliyewahikuwa mbunge wa Hanang’ mkoani Manyara.

“Ufisadi ni kitu kibaya cha ovyo, ni lazima kipigwe vita na Serikali inatakiwa kuwa kali kwa watu wanaobainika. Lakni tusije tukadhani jinsi taarifa ya CAG inavyotoka kila kitu ufisadi, kuna mengine katika ukaguzi hayakuonekana au yapo njiani,” alisema Sumaye.

Mahojiano hayo ya televisheni mtandao yalijikita katika masuala mbalimbali yanayomhusu Sumaye mwenyewe na ripoti za CAG zilizowasilishwa hivi karibuni bungeni.

Katika ripoti zake, CAG kila mwaka uibua madudu na kuonyesha udhaifu katika utekelezaji wa ushauri anaoutoa, jambo ambalo mara kadhaa limehusishwa na Bunge kutotimiza wajibu wake.

Hata hivyo, kuna kila dalili za Serikali kutaka uwazi katika utekelezaji wa ripoti hizo tofauti na kipindi cha nyuma kwani tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza taasisi na mamlaka za Serikali kuzipitia ripoti hizo, kujibu na hatua zichukuliwe kwa watakaobainika.

Udhaifu katika usimamiaji wa mapendekezo ya CAG uliwahi kuibua mjadala na hadi aliyekuwa CAG kabla ya Kichere, Profesa kukataliwa na Bunge, na hatimaye kuondolewa kwenye nafasi hiyo kabla ya muda wake kwa kuliita Bunge ni dhaifu.

Wakati sakata hilo likitikisa, aliyekuwa Spika Job Ndugai aliweka msimamo kuwa “hakuna wakati wowote ambao Bunge limekataa kufanya kazi na taasisi ambayo ni ofisi ya CAG. Bunge hili limekataa kufanya kazi na mtu anayeitwa Profesa Assad basi.”

Ndugai aliweka msimamo huo ikiwa ni siku ya tatu tangu Bunge kupitisha azimio la kutofanya kazi na Profesa Assad.

Januari 21, 2019, Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ilitumia dakika 156 kumhoji Profesa Assad aliyeitwa mbele ya kamati hiyo kueleza kauli yake kuhusu “udhaifu wa Bunge.”

Aliitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa wakati alipokuwa akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) akiwa New York, Marekani alikokuwa akihudhuria mkutano na akakiri mbele ya kamati kuwa alitumia neno “udhaifu” wa Bunge alipokuwa akieleza sababu za kutofanyiwa kazi kwa ripoti za ukaguzi ambazo zimekuwa zikibainisha ufisadi.

Chanzo: mwanachidigital