Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sugu ataja sababu nne za kutong’oka ubunge Mbeya

61440 Pic+sugu

Thu, 6 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ametaja sababu nne alizosema zinamsukuma kubakia kuwa mwakilishi wa wananchi katika jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Msanii huyo wa muziki wa kizazi kipya amesema sasa anasubiri muda ufike ajue CCM itamsimamisha nani kugombea katika kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi juzi, Sugu alitaja sababu hizo kuwa ni hali ngumu ya uchumi, Mbeya kuwa ngome ya upinzani, kuwafanya wananchi kujiona ni sehemu ya uongozi wa mkoa huo na mtaji wa kura alizopata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Kwa sasa tunajadili jinsi ya kulinda kura sio ushindi tena maana upo tu. Binafsi ninamsubiri atakayepitishwa na CCM siangalii anayetajwa ndio maana huwa siwezi kuzungumzia mtu kivuli maana ni kitu ambacho hakipo,” alisema Sugu.

Sugu alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kuhusu hatima ya ubunge wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Katika siku za hivi karibuni, wabunge na viongozi mbalimbali wa CCM wamekuwa wakitajwa kutaka kuwania ubunge katika jimbo hilo akiwamo naibu spika, Ackson Tulia.

Pia Soma

Wakati wa ziara ya Rais John Magufuli jijini Mbeya hivi karibuni mkoani Mbeya, Sugu alipewa nafasi na kiongozi huyo wa nchi kuzungumza kuwa siasa si uadui, akitaka watu kushirikiana katika masuala ya maendeleo bila kujali itikadi zao.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli aliambatana na Dk Tulia jambo ambalo lilizua mjadala hadi bungeni ambako mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa aliomba mwongozo akihoji sababu za naibu spika huyo kukacha vikao vya Bajeti na kwenda katika ziara hiyo.

Hata hivyo, mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alisema Dk Tulia ni mteule wa Rais hivyo anaweza kuitwa wakati wowote na mamlaka za juu.

Katika mikutano ya Rais, Dk Tulia alikuwa akizungumzia masuala mbalimbali ya maendeleo ya Mbeya, likiwemo suala la kuwaombea wamachinga eneo la uwanja wa zamani wa ndege kuwa sehemu ya kufanyia biashara zao.

Lakini, katika mahojiano na Mwananchi, Sugu alisema “Suala la Mbeya si binafsi wala si Sugu kuwa mbunge, wananchi wa Mbeya wana ajenda yao ya mageuzi na hainipi wasiwasi kabisa kwamba nini kinakwenda kutokea 2020.”

“Mtu yeyote ambaye hata kama si mpenda siasa akija Mbeya atajua hali halisi. Pamoja na yote wanayotufanyia bado Chadema iko juu Mbeya,” alisema Sugu.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka 2015 alipata kura 60,000 zaidi ya mgombea wa CCM jambo ambalo linampa nguvu ya kuwa na mtaji wa kura.

“Ni mwendawazimu pekee anaweza kudhani CCM itaishinda Chadema Mbeya, ndio maana hatuzungumzi tunapata ngapi, tunazungumzia tumejiandaaje kulinda kura,” alisema Sugu.

Alisema waliolinda kura mwaka 2015 walikuwa na maduka na magari zaidi ya mawili, “Kama ni duka basi kwa sasa hawana, waliokuwa na magari manne kwa sasa wanayo mawili au moja kutokana na hali ya uchumi. Hawa watalinda kura vyema kabisa...”

Akizungumzia mikutano ya hadhara kuzuiwa na vyama vya upinzani kujijenga kwa kusaka wanachama wapya alisema, “Siku hizi mikutano ya hadhara imehamia katika mitandao ya kijamii, baa na katika vikundi vya watu.”

“Wamezuia upinzani kufanya mikutano, lakini umesababisha mjadala. Hii mijadala ya watu kukaa maeneo mbalimbali na kuelezana hali ilivyo sasa kuhusu maisha yao haihitaji sayansi ya siasa kujua kuwa 2020 mambo ni mazuri.”

Waziri kivuli huyo wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pia aligusia jinsi wafanyabiashara wanavyoeleza mazingira magumu ya kufanya biashara pamoja na wafanyakazi kutoongezewa mshahara kwamba ni mambo ambayo yataongeza kura za upinzani si Mbeya pekee.

Alipoulizwa nini alichokifanya Mbeya hadi sasa alisema, “Utawala bora na uongozi sahihi. Ninawatetea wananchi ambao wanajiona kuwa sehemu ya uongozi wa Mbeya.”

Alisema mbunge kupigania ujenzi wa majengo mbalimbali si hoja kwa kuwa ni wajibu wake kufanya hivyo.

“Mwaka 2015 niliwaambia wananchi sina ahadi mpya kwa sababu mimi ni mbunge wa awamu ya pili na nilivyoingia awamu ya kwanza niliwapa ahadi kwa sababu walikuwa hawajui uwezo wangu katika uongozi na niliwapa vitu vya kunipima na mwaka 2015 nilisema nilivyoweza na nilivyoshindwa ni kwa sababu gani.”

“Nikawambia wananchi kuanzia sasa watakuwa wakisema ajenda na mimi nashughulikia na milango ipo wazi na ndio maana ninaishi Mbeya.”

Aliongeza, “niliwaeleza sina ahadi mpya isipokuwa kama jengo la maabara ya kisasa hospitali ya rufaa ya kanda Mbeya halitakamilika sitoomba kura 2020 maana ubunge utakuwa mgumu, kwa sasa hospitali hiyo imejengwa na ina vifaa vyote.”

Chanzo: mwananchi.co.tz