Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sugu alivyopanda jukwaani na mafaili kueleza alichofanya jimboni

10286 Pic+sugu TanzaniaWeb

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amefanya mkutano wa kwanza wa hadhara ikiwa ni siku 86 tangu atoke jela na kudai yupo tayari kufa kwa ajili ya watu wa Mbeya na kwamba haogopi chochote.

Sugu alihutubia mkutano wa hadhara Uyole jijini Mbeya juzi ukiwa mkutano wake wa kwanza tangu alipotoka jela Mei 10 huku akipanda jukwaani na faili lenye taarifa za miradi ya maendeleo aliyoitekeleza.

Mbunge huyo alihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela katika Gereza la Ruanda jijini Mbeya baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli. Hata hivyo hakumaliza kifungo kutokana na kupata msamaha wa Rais.

Katika mkutano huo, Sugu alisema hakuna anayeweza kumnunua ili awasaliti wapiga kura wake, akijigamba kuwa mtaji wake ni wananchi na si fedha.

Sugu alisema kazi kubwa aliyonayo ni kuokoa Taifa na upinzani na kwamba yupo tayari kufa kwa ajili ya watu wa Mbeya na haogopi chochote.

“Kwenye mitandao ya kijamii inaelezwa eti imetengwa Sh2 bilioni kwa ajili ya kumnunua Sugu, nawaambia mimi sina bei. Ukitaka kuninunua hakikisha umetupanga foleni wana Mbeya wote na uanze kumnunua wa kwanza nami nitakuwa wa mwisho,” alisema.

Aelezea miradi aliyoitekeleza

Sugu alipanda jukwaani akiwa na faili lenye taarifa za miradi aliyosema ameitekeleza tangu achaguliwe katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Alisema kwa muda mrefu kumekuwa na maneno ya kumchafua kutokana na kile alichokiita ‘siasa uchwara’ kwamba hajafanya jambo lolote la maana na badala yake watu wengine ndio wanaojitoa kuwasaidia wananchi wa Jiji la Mbeya.

“Makamanda msishangae kuniona nimeshika faili mkononi, nipo hapa kwa ajili ya kuwaeleza mambo niliyoyafanya tangu mmenichagua, maana hapa kuna watu wanazunguka mtaani kunichafua kuwa sijafanya kitu,” alisema Sugu.

Alisema tangu aingie madarakani mwaka 2015 na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuwa chini ya Chadema wamefanikisha ujenzi wa madaraja zaidi ya 10 yanayounganisha jiji hilo na vijijini.

Mbunge huyo alisema wamejenga vyumba maalumu kwa ajili ya mafunzo ya kompyuta kwenye shule za kata na kwa sehemu kubwa Jiji la Mbeya limeunganishwa kwa lami kabla ya barabara kuchukuliwa na kuwa chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura).

“Ndugu zangu, nimekuwa mbunge tangu mwaka 2010, lakini 2010/15 wakati halmashauri ikiwa chini ya CCM, nilipambana tukajenga daraja moja la Iyela. Mlipotuamini Chadema mkatupa jiji tumejenga madaraja zaidi ya 10 hadi sasa na leo hii kinamama wanaotoka Mbeya vijijini kuja mjini kuuza bidhaa wanapita kwa raha zao,” alisema.

Sugu alisema watoto yatima na wa familia zisizojiweza zaidi ya 400 amewasaidia kupata elimu tangu mwaka 2010 na baadhi walishamaliza vyuo vikuu.

“Nimefanya vitu vingi, lakini mimi si ‘mtu wa kiki’ wa kuita waandishi kwa kila kitu ambacho nakifanya kama wapinzani wangu wanavyofanya,” alisema.

Alisema katika kata ya Itezi alitoa Sh6 milioni kupaua madarasa manne na kata ya Sisimba ambayo diwani wake, Geofrey Kajigili (Chadema) alifukuzwa uanachama na kuvuliwa udiwani, alitoa Sh4 milioni kwa ajili ya ukarabati wa ofisi ya mtendaji kata.

“Ndugu zangu soko la Sido liliungua, wafanyabiashara zaidi ya 3,500 wameunguliwa bidhaa zao, tumehangaika sasa wamejenga maduka ya maana ambayo siku zote tulikuwa tukiyapigania badala ya kuwa na vibanda vya mbao, lakini eti mtu anakuja kutoa msaada wa Sh10 milioni, sasa hiyo inawasaidia nini wafanyabiashara 3,500,” alihoji Sugu.

Alisema, “Viongozi wa Sido walikuja kwangu nikawauliza kinachotakiwa ni nini baada ya soko kujengwa wakasema ofisi. Nikasema haina shida, leo mambo safi hadi marumaru zimewekwa halafu mtu anatoka Dar es Salaam na kusema eti Sugu hajafanya kitu, sijafanya kitu?”

Awali, mratibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga ambaye alifungwa jela pamoja na Sugu alisema demokrasia inazidi kuporomoka nchini hivyo Watanzania wanahitaji kuamka na kupinga hali hiyo.

Alisema kuanzia Septemba 9 ataanza kuzunguka kwenye majimbo yote ya Chadema ya kanda hiyo kufanya mikutano.

Chanzo: mwananchi.co.tz